Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amekabidhi kadi za CCM kwa wanachama wapya 76 kutoka katika chama cha waendesha pikipiki maarufu boda boda wa wilaya ya Ilemela
Akizungumza katika shughuli hiyo ya kupokea wanachama wapya iliyofanyika katika ukumbi wa Mihama kata ya Kitangiri MNEC Dkt Angeline Mabula amesema kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan anathamini na kutambua mchango wa makundi mbalimbali katika jamii na ndio maana hivi karibuni amepunguza gharama za makosa ya barabarani kwa boda boda kutoka elfu thelathini kufikia elfu kumi pamoja na kusisitiza askari wa usalama barabarani kutoa elimu zaidi kwa watumiaji wa vyombo vya moto badala ya kutoa adhabu hata kwa makosa yasiyolazima kufanya hivyo
'.. Lengo la Serikali sio kuwakandamiza ni kuwafanya kuwa pamoja na kujikwamua kiuchumi, Serikali ya awamu ya sita inajali makundi yote, nenda kwa mama lishe, nenda kwa machinga, hakuna kundi lililoachwa sababu anajua makundi yote yana mchango wake ktk jamii ..' Alisema
Aidha Dkt Mabula amewataka waendeshaji wa pikipiki hao kuhakikisha hawatumiki na watu wasioitakia mema nchi na chama huku akiwaasa kutumia vyema fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri kupitia mapato yake ya ndani itakayoanza kutolewa upya mapema mwezi Julai baada ya kusisimama kwa muda kuruhusu uwekwaji mzuri wa taratibu ili watu wote waweze kunufaika
Kwa upande wake Katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Ndugu Hasan Milanga mbali na kuwapongeza wanachama wapya waliojiunga na chama hicho, amefafanua kuwa CCM ndio inayotoa fursa wanazoziona ikiwemo ajira huku akimpongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela MNEC Mhe Dkt Angeline Mabula kwa namna anavyoshirikiana na kundi hilo pamoja na kutatua kero na changamoto zinazowakabili sanjari na kuwasisitiza kuridhika na kushirikiana na viongozi wanaoshirikiana nao
Akisoma taarifa ya kikundi hicho cha boda boda wilaya ya Ilemela Ndugu Maiga Malegesi amesema kuwa wanatambua kazi nzuri zinazofanywa na Mbunge huyo ndio maana wakaamua kushirikiana nae pamoja na kutaja changamoto zinazowakabili ikiwemo pango la ofisi, samani za ofisi na vifaa ikiwemo kompyuta na printa ambapo Mbunge Dkt Angeline Mabula aliwakabidhi papo hapo kiasi cha shilingi laki tano kwaajili ya kulipa pango kwa ofisi ya wilaya na laki moja na nusu kwa ofisi ya mkoa
Jimbo la Ilemela mpaka sasa tangu kuingia madarakani Kwa Serikali ya awamu ya sita limeshapokea kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 67.7 kwaajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu msingi Bilioni 16, Elimu sekondari bilioni 6, Tasaf bilioni 5, afya bilioni 3 na barabara, masoko.