SERIKALI KUENDELEA NA KIPAUMBELE CHA UJENZI WA MABWENI YA KIDATO CHA TANO NA SITA

 

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mhe. Zainab Katimba amesema kwasasa Serikali itaendelea na kipaumbele cha ujenzi wa mabweni ya kidato cha Tano na Sita kwa lengo la kuhakikisha Wanafunzi wote wanaofaulu kidato cha Nne wanapata fursa ya kusoma elimu ya sekondari ya ngazi ya juu.

Mhe. Katimba ameyasema hayo leo Aprili 23,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Regina Qwaray Mbunge wa Viti Maalum aliyetaka kujua kuna mkakati gani kuhakikisha Shule zote za Sekondari nchini zinajengewa Mabweni.

“Serikali imeweka kipaumbele katika ujenzi wa Mabweni kwenye shule za Sekondari za kidato cha Tano na Sita nchini ili kuwawezesha Wanafunzi wote wanaofaulu mtihani wa kidato cha Nne waweze kupata fursa ya kujiunga Kidato cha Tano,”amesema.

Amesema katika mwaka 2022/23 Ofisi ya Rais – TAMISEMI ilifanikiwa kujenga jumla ya mabweni 683 kupitia fedha za mradi wa SEQUIP, Barrick Tanzania na Serikali Kuu huku katika mwaka 2023/24 Ofisi ya Rais TAMISEMI iliidhinishiwa fedha kiasi cha shilingi bilioni 7.41 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 57 yanayoendelea kukamilishwa.

“Aidha, Serikali kupitia Halmashauri itaendelea kuhamasisha Wananchi kujenga na kuziendesha hosteli katika shule za sekondari za kidato cha kwanza hadi cha Nne,”amesema.

Previous Post Next Post