SHUWASA TUMEENDELEA KUTEKELEZA MIRADI MBALIMBALI YA KUONGEZA MTANDAO WA MAJISAFI KATIKA MAENEO YA MANISPAA YA SHINYANGA – MHANDISI KATOPOLA

 

Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) Mhandisi Yusuph Katopola akisoma taarifa ya miradi ya uboreshaji huduma ya majisafi na usafi wa mazingira iliyotekelezwa, inayotekelezwa na itakayotekelezwa na SHUWASA katika Manispaa ya Shinyanga.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuongeza mtandao wa majisafi katika maeneo ya Manispaa ya Shinyanga kupitia vyanzo mbalimbali vya fedha ikiwa ni pamoja na mapato ya ndani ya mamlaka, serikali kuu pamoja na wafadhili.

Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola wakati akizungumza  Aprili 30,2024 kwenye baraza la madiwani Manispaa ya Shinyanga

Mkurugenzi huyo Mhandisi Katopola ametaja miradi mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa kupitia fedha za ndani huku akitaja kata zilizonufaika na miradi ikiwemo kata ya Ibadakuli, Mwawaza, Kitangili pamoja na Kizumbi.

Amesema SHUWASA kwa kutumia mapato yake ya ndani imetumia Milioni 81.9 katika kipindi cha Mwaka wa fedha 2023\2024 kwa lengo la kuongeza mdandao wa majisafi katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Shinyanga.

“Kwa kutumia mapato ya ndani SHUWASA tumetumia kiasi cha shilingi 81,983, 290.20 kwa ajili ya kuongeza mtandao wa majisafi katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Shinyanga kwa Mwaka wa fedha 2023\2024 kata zilizonufaika na miradi hii ni pamoja na kata ya Ibadakuli (Kilomita 1.37), Mwawaza (Mita 580), Kitangili (Kilomita 1.43), kata ya Kizumbi (Mita 996).

“Katika kata ya Kata ya Ibadakuli eneo la Buweto wamenufaika kwa urefu wa mtandao wa bomba ambao tuliongeza Kilomita 1.37 ambapo Bomba za urefu wa mita 707 zimelazwa na wananchi wanapata huduma ya majisafi lakini pia katika kata hiyo bomba zenye urefu wa mita 600 mradi unaendelea na utekelezaji”.amesema Mhandisi Katopola

“Kata ya Mwawaza eneo la Mwantini urefu wa mtandao wa bomba tuliongeza kilomita 0.85 ambapo bomba zenye urefu wa mita 580, mradi unaendelea na utekelezaji”.

“Kata ya Kitangili eneo la Iwelyangula urefu wa mtandao wa bomba tuliongeza kilomita 1.43 ambapo utekelezaji wa mradi umekamilika kwa asilimia mia moja mpaka sasa wananchi wanaendelea kupata huduma ya majisafi”.

“Pia kata ya Kizumbi eneo la Nhelegani urefu wa mtandao wa bomba tuliongeza kilomita 0.996 ambapo kazi ya uchimbaji wa mtaro inaendelea na bomba za mradi husika ziko eneo la mradi”.amesema Mhandisi Katopola

Kwa upande wa miradi inayotekelezwa kupitia fedha za nje amesema mamlaka hiyo inaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa kupitia fedha za mkopo wa riba nafuu kutoka shirika la maendeleo la Ufaranza (French Development Agency; AFD) kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania.

SHUWASA inatekeleza mradi wa majisafi na usafi wa mazingira Manispaa ya Shinyanga na miji ya Tinde, Didia na Iselamagazi.

Mhandisi Katopola amefafanua kuwa mradi huo wenye thamani ya Euro milioni 76 ambapo ni takribani bilioni mia mbili (200) na kwamba mradi huo unahusisha kazi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa mitambo miwili ya kuchakata tope kinyesi pamoja na ukarabati mkubwa wa mtambo wa kutibu majisafi Ning’hwa.

“SHUWASA tunaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa kupitia fedha za mkopo wa riba nafuu toka shirika la maendeleo la Ufaransa AFD kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania, mradi huo unahusisha kazi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa mdandao wa majisafi wenye urefu wa kilomita 280, ukarabati wa mdandao wa mtandao chakavu wa majisafi unaofikia kilomita mia moja (100)”.

“Pia mradi huo unahusisha ujenzi wa tangi moja la kuhifadhi maji lenye ujazo wa mita za ujazo 1,500 katika kata ya Kolandoto, ujenzi wa mitambo miwili ya kuchakata tope kinyesi eneo la Ihapa na Mwagala lakini kuna ukarabati mkubwa wa mtambo wa kutibu majisafi Ning’hwa na tathimini ya ufanisi wa bwawa la Ning’hwa pamoja na ujenzi wa jingo jipya la ofisi ya SHUWASA”.amesema Mhandisi Katopola

“Lakini zabuni tatu zimetangazwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi ambapo mhandisi mshauri kwa kazi ya tathimini na usimamizi wa mradi ( Consultancy Services for Design and Supervision, Mhandisi mshauri wa kazi ya ushauri na msaada wa kitaaluma katika usimamizi wa mradi ( Technical Assistance na Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa mradi”.amesema Mhandisi Katopola

“Pia SHUWASA kwa kushirikiana na mamlaka zingine za serikali imefanikiwa kulipa fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya mradi na sasa SHUWASA tunaendelea na zoezi la kupata hati za maeneo husika”.amesema Mhandisi Katopola

Baadhi ya madiwani wa kata mbalimbali za Manispaa ya Shinyanga wameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) kwa utekelezaji mzuri  wa miradi ambao unashirikisha viongozi, wadau na wananchi wa enei husika.


Previous Post Next Post