TANZANIA YASISITIZA UMOJA WA MATAIFA KUWA HAINA WATU WA ASILI

 Na Mwandishi Wetu


Serikali ya Tanzania imesema kuwa watu wake hakika haina asili wanasimama katika mshikamano na Watu wa Asili duniani kote ambao ni wakazi wa mwanzo kabisa wa maeneo yao ya asili ikiwa ni pamoja na yale yaliyovamiwa na kutawaliwa na walowezi wa kutoka nchi na tamaduni zingine.

Ujumbe huo umetolewa na Katibu Mtendaji Mkuu Profesa Hamis Malebo katika Mkutano wa 23 wa Jukwaa la kudumu la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Watu wa Asili (UNPFII) uliomalizika jijini New York nchini Marekani.

Amesema kuwa ujumbe huo uliukumbusha mkutano huo kuwa, Tanzania ilikuwa ni koloni la Wajerumani na baadaye Koloni la Waingereza lakini ilipata uhuru wake mwaka 1961.

Profesa Malebo amesema kuwa Watanzania wanaojumuisha zaidi ya makabila 120, waliishi katika eneo ambalo sasa linajulikana kama Tanzania, zaidi ya miaka 5,000 iliyopita.

Hata hivyo amesema hali ya kujenga taifa moja lenye umoja na amani, juhudi za makusudi zilifanywa na waasisi wa taifa letu kuhakikisha watu wetu wanaishi kwa maelewano na bila ubaguzi.

Profesa Malebo amesema ujumbe wa Tanzania ulibainisha kuwa, katika suala la Watu wa Asili kwa mujibu wa Katiba yetu na sheria za kitaifa, hatuna kundi mahususi la Watu wa Asili nchini.

Amesema Mtanzania yeyote mwenye asili ya Kiafrika kisheria ni raia na ni Mtanzania na hakuna kabila lenye haki zaidi ya lingine.

"Watu wa Tanzania kutoka katika makabila zaidi ya 120 wameunganishwa na tamaduni, urithi wa pamoja, maadili na desturi pamoja na lugha ya Kiswahili inayoadhimishwa duniani kote

Kadhalika, Ujumbe wa Tanzania ulifafanua kuwa, kwa kuzingatia haki ya kujitawala"amesema

Profesa Malebo amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapenda kusisitiza msimamo wake na imani thabiti katika Umoja wa Mataifa na kukemea juhudi zozote hasi zenye lengo la kuvuruga mafanikio yaliyofikiwa ya kujenga taifa la watu walio sawa na huru. Ujumbe huo ulilieleza jukwaa hilo kuwa, hakuna kabila au kundi la watu linaloweza kuwa kubwa kuliko taifa letu.

Amesema tuhuma mbovu na zilizoenea dhidi ya Tanzania, zinazoenezwa na watu na makundi machache, ambao wameamua kupuuza ukweli ambao tumeueleza mara nyingi katika Umoja wa Mataifa na tunapenda kusisitiza kwa mara nyingine kuwa Tanzania ni nchi inayoongozwa na utawala wa sheria, kuheshimu sheria, haki za binadamu na misingi mikuu ya utawala bora.

Aidha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake kwa usawa na kwa kuzingatia utu, haki za binadamu, mila, desturi na tamaduni za wananchi.

Profesa Malebo wakati akihitimisha alilisisitiza Kwa ujumbe kwa kuweka mambo katika muktadha, Waamasai hawawezi kuchukuliwa kuwa ni Watu wa Asili wa Hifadhi ya Ngorongoro kwani walifika Ngorongoro takriban miaka 200 iliyopita na kuwakuta Wahadzabe waliokaa hapo kwa zaidi ya miaka 3,000 iliyopita na Wadatoga waliokuwa hapo kwa zaidi ya miaka 400 kabla ya kuwasili kwao. Waamasai waliwashambulia na kuwafukuza Wahadzabe na Wadatoga kutoka katika ardhi waliyoishi kwa miaka zaidi ya 3,000 na 400, mtawalia.

Amesema Waamasai baada ya kuwafukuza Wahadzabe na Wadatoga, walilikalia eneo hilo huku akiongeza suala suala la kabila moja kuvamia na kuondosha kabila lingine katika eneo la asili si jambo geni nchini Tanzania, lilitokea pia kwa Wandendeule ambao walishambuliwa na kufukuzwa katika eneo lao na Wangoni walioingia Songea kutokea Afrika Kusini, vile vile Wamakua ambao nao walipigwa vita na kufukuzwa katika eneo lao huko Mtwara na Wayao na Wamakonde kutokea Msumbiji.

Prof. Malebo alisisitiza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikubaliani na dhana ya Watu wa Asili kwa vile haitendi haki kwa muktadha wa hali ya makabila ya Tanzania na takribani kila kabila lililotangulia nchini kabla ya ujio wa Waamasai kimsingi ni la asili zaidi na hivyo Watanzania wote wenye asili ya Kiafrika ni raia na ni Watanzania. Kwa hiyo, siyo sahihi kuchagua kabila moja kati ya makabila zaidi ya 120 ya Tanzania yenye sifa stahiki na kuliita moja kuwa ni la asili.

Prof. Malebo alihitimisha kwa kusisitiza katika Kikao cha Jukwaa la Watu wa Asili na kuwaomba kuuelewa msimamo wa Serikali ya Tanzania pia kuwa mfumo wa umiliki wa ardhi nchini Tanzania hautambui ardhi za mababu au ardhi za kimila wala ardhi za makabila. Ardhi inamilikiwa na umma na imekabidhiwa kwa Rais kama mdhamini kwa niaba ya Watanzania wote. Mtu anapewa haki ya kumiliki ardhi kwa kufuata utaratibu wa kisheria na kwa muda maalum. Alisisitiza kuwa ni makosa kudai kwamba Waamasai au kabila lolote wanafukuzwa katika ardhi yao au ardhi ya mababu zao au ardhi ya kimila kwa vile jambo hilo halipo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wala katika sheria za nchi yetu na hakuna mwananchi yeyote aliyefukuzwa Loliondo wala Ngorongoro. Alilisisitiza Jukwaa hilo kutambua kwamba zoezi linalofanyika Loliondo ni kunusuru uhifadhi wakati kwa Ngorongoro ni kuwasaidia Jamii ya Wafugaji kuhamia kwa hiari maeneo salama zaidi kwa manufaa yao, usalama wao na kujipatia maendeleo kama Watanzania wengine.

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Prof. Hamisi M. Malebo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wajumbe wengine wa Tanzania waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Dkt. Agnes Gidna, Kaimu Meneja wa Urithi wa Dunia katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Bw. Pellage Kauzeni, Afisa Mhifadhi Mkuu wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Erick J. Kajiru, Afisa Mwandamizi Mkuu katika Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi. Zuleikha Tambwe, Afisa Mambo ya Nje Mwandamizi katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Bi. Hindu Zarooq Juma, Afisa Mambo ya Nje Daraja la Pili kutika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, na Bw. Edward Kutandikila, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

Previous Post Next Post