VIONGOZI WA SERIKALI NA VYAMA WATUMA SALAMU ZA POLE KWA ASKOFU SANGU KUFUATIA KIFO CHA PADRE MAKOLO


Viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali, wameendelea kutuma salamu za pole kwa Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, kufuatia kifo cha aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Ndala Padre Emmanuel Makolo.

Viongozi hao ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa mkoa wa Shinyanga Emmanuel Ntobi, Katibu tawala wa Wilaya ya Rorya Mkoani Mara Boniphace Chambi na aliyewahi kuwa Mbunge wa viti maalum mkoa wa Shinyanga kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Bi. Azah Hilal.

Viongozi hao  kwa pamoja wameeleza kumfahamu vyema Marehemu Padre Makolo, kutokana na ushiriki wake katika shughuli mbalimbali za  Serikali na za kijamii enzi za uhai wake.

Wameonyesha kusikitishwa kwao ni kifo cha Padre Makolo na kubainisha kuwa, licha ya kuwa kiongozi wa kiroho, alikuwa akishiriki kwa ukamilifu kwenye shughuli za maendeleo, kiserikali na kijamii na kwamba, siku chache kabla ya kifo chake alishiriki kikao maalum cha maandalizi ya mapokezi ya mbio za mwenge katika mkoa wa Shinyanga.

Viongozi hao kwa umoja wao wametoa pole kwa Askofu wa Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, Mapadre, waamini ndugu jamaa na marafiki na wameahidi kumwombea ili Mungu ampokee katika makazi yake ya Milele.

“Pumzika kwa amani Baba Paroko Makolo maana wewe ni mavumbi, na mavumbini utarudi (Mwanzo 3:19) Salamu zangu za rambirambi kwa Mhashamu Baba Askofu Sangu, Familia, Mapadri, Waamini, na Kanisa kwa ujumla. Hakika ni pigo kubwa si kwa Kanisa pekee bali kwetu sote kama familia ya Mungu na Wanashinyaga. Mwamba umetangulia, Mshua umezima ghafla katikati ya giza. Tunamshukru Mungu kwa zawadi ya uhai wa Mzee wetu. Tangulia tutaona Father Makolo"  Amesema Emmanuel Ntobi Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Shinyanga.

“Nimepokea Kwa mshituko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha Pd. Emmanuel Makolo. Kweli Sisi ni wa Mungu na kwake tutarejea. Mwenyezi Mungu awafariji familia, Kanisa, wanashinyanga na aipumzishe roho ya mpendwa wetu pema peponi..Amina. Nakumbuka ushirikiano aliokuwa nao mtumishi huyu wa Mungu Kwa serikali wakati wote niliowatumikia wananchi wa wilaya ya Shinyanga. Hakika alikuwa mtu wa kuigwa. Majitoleo yake yatakumbukwa daima”  Amesema Boniphace Chambi Katibu tawala wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara ambaye pia amewahi kuwa Katibu tawala wa Wilaya ya Shinyanga.

“Hakika kila Nafsi itaonja Mauti, Pole sana Baba Askofu,Mapadri,Familia,ndugu,jamaa na marafiki wote Ucheshi wake,Upole, Upendo aliokuwa nao   hakika vinabaki kuwa historia. Apumzike kwa Amani Fr.Emmanuel Makolo”   Amesema Mh.Azah Hilal aliyekuwa Mbunge wa viti maalum (CCM) mkoa wa Shinyanga.

Padre Makolo amefariki dunia siku ya Alhamisi tarehe 25.04.2024, katika Hospitali ya rufaa ya  kanda Bugando Jijini Mwanza, wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

Mazishi yatafanyika Jumanne tarehe 30.04.2024, katika makaburi ya Mapadre yaliyopo Kanisa kuu Ngokolo mjini Shinyanga.
Previous Post Next Post