WAZIRI JAFO AELEZEA FURSA ZA BIASHARA YA KABONI











Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema kuna fursa kubwa ambayo Tanzania itanufaika katika biashara ya kaboni.

Amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo Aprili 19, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbeya Vijijini Mhe. Oran Manase Njeza aliyetaka kufahamu kama kuna fursa na changamoto gani kwa Tanzania kushiriki kwenye biashara ya kaboni.

Dkt. Jafo amesema kuwa miongoni mwa fursa ambazo nchi inafaidika nazo kutokana na biashara hiyo kuwa ni pamoja na uhifadhi wa bionuai na ongezeko la Pato la Taifa.

Amesema hivi karibuni halmashauri mbalimbali zimepokea fedha zilizotokana na biashara ya kaboni kutoka katika kampuni mbalimbali ambazo zinatumika kujenga miundombinu ya kusaidia jamii katika halmashauri hizo.

Ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa biashara hiyo katika hifadhi ya mazingira Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa Kanuni za Usimamizi wa Biashara ya Kaboni za mwaka 2022 ambapo hadi sasa takriban miradi 42 imesajiliwa.

Hata hivyo, amesema pamoja na fursa zilizopo bado kumekuwa na changamoto kadhaa katika biashara ya kaboni ikiwemo uelewa mdogo wa jamii katika utekelezaji wake.

Pamoja na changamoto hizo, amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wote ili kuhamasisha uwekezaji wa miradi ya biashara ya kaboni katika sekta mbalimbali pamoja na biashara ya kaboni kwa wadau mbalimbali ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu biashara hii.
Previous Post Next Post