WAZIRI MKUU AONYA KUHUSU RUSHWA KITEGA UCHUMI CHA STENDI YA KANGE

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameonya viongozi wanaogawa maeneo kwenye kitega uchumi kipya cha Dkt. Samia Suluhu Hassan Business Centre kilichopo stendi ya Kange, nje kidogo ya Jiji la Tanga wajiepushe na vitendo vya rushwa.


“Viongozi wote mnaosimamia mchakato wa kuwapata wapangaji wa jengo hili, jiepusheni na vitendo vya rushwa kwa kisingizio cha kutokidhi vigezo. Mkuu wa Mkoa upo hapa, wewe pamoja na watendaji wako hakikisheni mnachukua hatua stahiki. Fanyeni uhakiki wa vigezo vilivyopo ili kuwezesha wananchi wengi wenye nia kunufaika,” amesema.

Ametoa onyo hilo leo (Jumatatu, Aprili 22, 2024) wakati akizungumza na viongozi na wananchi, mara baada ya ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa kitega uchumi kilichopo eneo la Kange ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania ambapo kilele chake ni April 26, 2024.

“Kwenye ugawaji wa maeneo kama haya, kuna watu huwa wanadai rushwa, mtu hata biashara yenyewe hajaanza, unataka atoe chochote, mtaji utabakia kweli?,” alihoji na kuwataka wananchi wakati wakifanya maombi yao wasisite kutoa taarifa iwapo wataombwa rushwa na maafisa wa Serikali ili wahusika wakamatwe.

Amesema azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa halmashauri zote zinajiendesha na zinajisimamia kwa kutumia mapato yake ya ndani. “Ili kufanikisha azma hiyo, Serikali iliweka mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuzigharimia halmashauri ambazo zilibuni miradi ya kimkakati yenye lengo la kutoa huduma bora zaidi na zenye uhakika kwa wananchi. Mradi wa kimkakati wa kitega uchumi wa Jiji la Tanga, ambao leo hii nimeuwekea jiwe la msingi ni moja ya miradi hiyo,” amesisitiza.

Amewapongeza viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa kutumia kikamilifu fursa za kimapato zilizopo ili kuongeza uwezo wa kujitegemea kwa kubuni na kuandaa mradi huo wa kimkakati wa Jengo la Kitega Uchumi katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi na viongozi wafuatilie kwa makini maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano na hasa hotuba ya kitaifa ambayo itatolewa kwenye vyombo vya habari na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Alhamisi hii, Aprili 25, 2024 kuanzia saa 3 usiku.

Pia amewataka wajitokeze kwa wingi na kutoa maoni yao kuhusu dira ya Taifa waitakayo pindi kamati za kukusanya maoni zikianza kutembelea maeneo yao ili nchi iweze kuwa na Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ambayo ni jumuishi na shirikishi.

“Serikali imeanzisha mchakato wa kuandaa Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ambayo inatarajiwa kutoa mwongozo wa mwelekeo wa nchi kwa kipindi cha miaka zaidi ya 25 ijayo. Mheshimiwa Rais alisema vijana ni wengi hivyo washirikishwe kwa wingi. Kama ni afya, semeni mnataka iweje, kama ni biashara, semeni mnataka iweje.”

“Halmashauri zenu na Jiji la Tanga watatoa rasmi siku ya kutoa maoni ili mwende mkatoe maoni yenu. Kama ni michezo au kilimo sema unatamani nini kiwemo. Na je mawazo yako ni yapi. Tunatamani kuona kila Mtanzania akitoa maoni yake kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050,” amesema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Mkuu w Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Burian amesema katika kipindi cha miaka mitatu, zaidi ya sh. trilioni 2.6 zimepokelewa katika mkoa huo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Amesema kati ya fedha hizo, sh. bilioni 159 zimetumika kwenye elimu, ambapo wameweza kujenga shule mpya 77, kwenye maji walipokea sh. trilioni 1.2, kwenye afya walipokea sh. bilioni 36 ambazo zimetumika kujenga hospitali sita mpya za wilaya na majengo ya dharura.

Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Mkuregenzi wa Jiji la Tanga, Fred Sagamiko alisema kitega uchumi hicho kimejengea jirani na stendi kuu, kituo cha daladala, bodaboda na kituo cha maegesho ya malori.

Alisema mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimi sh. bilioni 8.7 na kwamba hadi sasa wameshatumia sh. bilioni 7.4 kumlipa mkandarasi na sh. milioni 544.7 ambapo hadi sasa kiasi kilicholipwa ni sh. bilioni 7.9 ambayo ni sawa na asilimia 90.7 ya gharama za mradi.

Naye, Mhandisi wa Jiji, Issa Rajab Mchezo alisema ndani ya kitega uchumi hicho kutakuwa na ofisi 42 za wakata tiketi za mabasi, eneo la wasafiri kupumzika, maduka, migahawa, vyoo na ukumbi mkubwa wa kufanyia shughuli mbalimbali.

Previous Post Next Post