Ticker

6/recent/ticker-posts

BIASHARA YA NGONO WAKATI WA MAVUNO CHANZO CHA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO SHYDC


Wananchi wa maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wameziomba Mamlaka za Serikali za mitaa wakiwemo watendaji wa Kata na Maafisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya Kata, kuendelea kuweka mikakati ya kukomesha biashara ya ngono, ambayo hushamiri kwenye maeneo yao katika  kipindi hiki cha mavuno.

Wananchi hao wametoa ombi hilo wakati wakichangia maoni kupitia Kipindi cha Mwanamke na Maisha kinachoandaliwa na Redio Faraja kwa kushirikiana na Mfuko wa Ruzuku kwa Waanawake Tanzania (WFT-T) kwa lengo kufanikisha Mpango wa taifa wa MTAKUWWA, ambao umelenga kutokomeza Vitendo vya ukatili kwa wanawake wa Watoto.

Wamesema ni kwa miaka mingi sasa kumekuwa na makundi ya wanawake kutoka mijini ambao wanakwenda kupanga kwenye nyumba za wageni katika maeneo mbalimbali ya vijijini wakati wa msimu wa mavuno, kwa lengo la kukusanya Mpunga kupitia biashara ya ngono. 

Wanawake hao wanaelezwa kwenda katika maeneo mbalimbali yanayostawisha zao la Mpunga kwa wingi mara tu msimu wa mavuno unapoaanza, ambapo hutumia biashara ya kuuza miili yao kukusanya mpunga kutoka kwa wanaume wanaowahitaji kimapenzi, hatua ambayo inasababisha baadhi ya wanaume kuzitelekeza familia zao ikiwemo kutumia chakula kilichopatikana kwa anasa na wanawake hao.

Hali hiyo imeelezwa kuchangia ukatili kwa kiwango kikubwa, kwa kuwa  baadhi ya wanaume huuza chakula chote bila kujali mahitaji ya familia na kuhamia Senta kwa ajili ya kutumia  fedha zinazopatikana kwa anasa na wanawake hao, huku Mama na watoto ambao ndiyo hushughulika kwa kiasi kikubwa wakati wa kilimo wakiachwa wanahangaika bila msaada na kukosa mahitaji muhimu ikiwemo chakula cha kujikimu.

Aidha, baadhi ya wanawake wanapojaribu kuzuia suala hilo hukutana na ukatili mwingine wa kipigo, hatua ambayo imekuwa ikisababisha migogoro mingi ya kifamilia huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake na watoto.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Tinde Bi.Eva Mlowe licha ya kukiri kuwepo kwa hali hiyo na hasa kwa miaka ya nyuma, amesema kwa sasa imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa ikiwemo zoezi walilolifanya katika Kata yao la kupita katika nyumba za kulala wageni kuwabaini wanawake hao na kuwaondoa, pamoja kuwaonya wamiliki wa nyumba zilizokuwa zinawahifadhi.

Amesema kabla ya hatua hizo kuchukuliwa, wanawake hao walikuwa wakishuhudiwa wakiondoka na magunia ya Mpunga kwenye magari ambayo waliyapata kama ujira kutokana na biashara ya ngono waliyokuwa wakiifanya, ambapo walikuwa wakilipwa  magunia kuanzia mawili mpaka ishirini na wanaume wanaowaruhusu kuwashika sehemu mbalimbali za miili yao, kuishi nao kwa muda au kushiriki nao tendo la ndoa.

“Wanawake hao walikuwa wanakuja kwenye maeneo yetu msimu wa mavuno wakidai kwamba wanakuja kufanya biashara hali ambayo ilikuwa inawafanya wazee wengi wa familia kuacha familia zao na kuhamia mitaani kwenda kuishi nao kwa masharti kwamba, ukitaka kukaa na mimi labda siku mbili unipe gunia tano za Mpunga, ukitaka kunishika tu nipe gunia mbili na kwenda kushiriki tendo la ndoa mimi unipe gunia ishirini za Mpunga na baadhi ya wanaume walikuwa wakitekeleza masharti hayo na tukawa tunashuhudia hawa wanawake wanaondoka na magari yamejaza Mpunga, huku  akina Baba wakiwa wamezidanganya familia zao  kuwa wameweka Mpunga kwenye Maghala kuhifadhiwa na baadaye wanakuja kuwaambia wake zao umeibiwa hali iliyokuwa ikileta migogoro mikubwa”

Bi. Mlowe ameziomba Mamlaka za juu za Serikali kuwaongezea nguvu katika kudhibit hali hiyo na hasa kipindi hiki cha mavuno, kwa kuwa mafanikio yaliyofikiwa hivi sasa wamechangiwa kwa kiasi kikubwa na msukumo uliotolewa na viongozi wa ngazi za juu wakiwemo wakuu wa Wilaya na wakuu wa mikoa.

Kwa upande wao Afisa Mtendaji wa Kata ya Didia Bw. Hussein Majaliwa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Usule Bw. Shimba Waziri Masesa wamesema hali hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa kwa sasa ikilinganisha na miaka ya nyuma, kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa dhidi ya wahusika.

Wamebainisha mikakati mbalimbali waliyoweka kuzuia ukatili huo pamoja na visa vingine vya ukatili, kuwa ni pamoja kutoa elimu kwa jamii, kuvishirikisha vyombo vingine kama Kamati za MTAKUWWA ngazi za Vijiji, Jeshi la Jadi Sungusungu, Wahudumau wa afya ngazi ya jamii na Jeshi la Polisi.

Visa vya namna hiyo vimekuwa vikiripotiwa pia kwenye maeneo mengine ya mkoa wa Shinyanga ikiwemo Wilaya ya Kishapu, pamoja na Wilaya jirani za Igunga na Nzega mkoani Tabora.

Post a Comment

0 Comments