KINANA ATAKA WATANZANIA WASIKUBALI KUGAWANYWA KWA HOJA DHAIFU


Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Abdulrahman Kinana akizungumza na wanachama wa CCM na Wananchi wa Mkoa wa Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
 
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amewaomba Watanzania kutokubali hoja za kejeli, chuki na kufarakanisha watu ambazo zimekuwa zikitolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
 
Amesema viongozi wa CHADEMA kwa nyakati tofauti katika mikutano yao ya hadhara wamekuwa wakieneza chuki, uongo na kuzusha kauli za uchoganishi dhidi ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa hoja dhaifu kwamba anatoka Zanzibar.
 
Akizungumza jana jijini Dodoma mbele ya viongozi, wana CCM pamoja na wananchi wakati wa mkutano maalumu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Kinana alisema CHADEMA imepata uhuru mkubwa kufanya maandamano, mikutano ya hadhara, kuzunguka sehemu mbalimbali
 
“Katika mizunguko yao CHADEMA wamesema mengi, wametutuhumu CCM, serikali, wamemtuhumu Rais kwa mambo ya uongo. Hatukatai kukoselewa, hatukatai kusahihishwa, lakini hatukubali kuzuliwa au kushutumiwa kwa mambo ambayo hayapo.
 
“Kubwa ambalo wamefanya ni kujenga chuki miongoni mwa Watanzania, kujenga mifarafakano. Wakaenda mbali zadi wakaanza kuzusha jambo ambalo wanataka kuifanya ajenda, wanasema nchi ina Rais ambaye ni Mzanzibari na anaihujumu Bara, lakini ajenda hiyo imeshindwa,” alisema.
 
Akifafanua zaidi alisema CHADEMA wanazungumza kuhusu Rais Samia ni Mzanzibar, hana huruma na Bara, hana jema analofanya kwa Bara, hana msaada.
 
“Wanataka kumtenganisha Rais na Watanzania, nani amekataa kwamba Rais Samia sio Mzanzibari. Ni Mzanzibari na ametokana na Katiba ambayo inaeleza mgombea urais akitoka Zanzibar basi mgombea mwenza anatoka upande wa pili…
 
“Ndivyo tulivyokubaliana na huyu ni mgombea mwenza ana nafasi sawa na mgombea urais. Ikitokea mgombea mwenza hayuko uchaguzi unaahirishwa. Mwaka 2005 uchaguzi uliahirishwa kwa sababu mgombea mwenza wa CHADEMA alifariki dunia.
 
“Halafu leo wanakejeli kiongozi kutoka Zanzibar, wametafuta namna ya kushughulika na Rais (Dk. Samia) lakini wakiangalia barabara zinajengwa, bwawa la mwalimu Nyrere limefika pazuri, ujenzi wa mji wa Dodoma unaendelea kwa kasi.
 
“Reli ya mwendo kasi sasa imefika Dodoma na ujenzi unaendelea sasa wanakosa hoja wanakuja na maneno ya kuzusha kwamba Rais hafai kwa sababu anatoka Zanzibar. Rais Samia ni Rais wa katiba amechukua uongozi baada ya Rais Dk. John Magufuli kufariki dunia,” alisema.
 
Aliogeza “Rais Samia alikuwa Mgombea Mwenza akawa Makamu wa Rais, na awamu ya pili Magufuli akamteua tena lakini oooh… huyo Mzanzibar ili watu baadae polepole waanze kusema tunatawaliwa na Mzanzibari.”
 
Kinana aliwaomba Watanzania kupuuza uzushi huo na kushauri wasimame na Rais Samia kwani anafanya kazi nzuri. Tangu awamu mbalimbali zilizopita kuna sera iliyoanza baada ya Mzee Mwinyi (Hayati Rais mstaafu) kuchukua nchi kwa kuanzisha sera ya sekta binafsi kushiriki kukuza uchumi.
 
“Leo CHADEMA wanasema Rais Samia anauza kila kitu, kauza nini?. Awamu ya Tatu Rais mstaafu Benjamin Mkapa alibinafsisha mashirika zaidi ya 200 kwani alikuwa Mzanzibar? Lakini alifanya hivyo kwa maslahi ya taifa.
 
“Wakati TICS wanapewa bandari ya Dar es Salaam nchi haikuuzwa, lakini baada ya kupewa DP World nchi inauzwa. Hivi mnaamini kweli Rais anaweza kukaa na kufanya jambo ambalo halina nia njema na nchi yetu.
 
“Rais haamui peke yake kuna vyombo ambavyo vinakaa na kuangalia mambo na kisha vinamshauri Rais. Kataeni juhudi zinazofanyika za kujenga chuki dhidi ya Rais. Kuna wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilikabidhiwa kwa RITES (kampuni) kutoka India? Alikabidhi Rais Samia?”
 
Kinana alisema hayo mambo yanafanyika kwa malengo na hasa kuleta tija na ufanisi, hivyo Watanzania wasikubali kusikiliza hoja rejareja, hoja za msimu.
 
“Wanakwenda wanakaa katika kiwanda cha kutengeneza uongo na uzushi na kisha wanaanza kuituhumu CCM na serikali yake. Hatukatai kukoselewa, hata Rais Samia hakatai, sisi si malaika tunakosea. Tunasahihishwa, lakini kudharauliwa na kutukanwa hapana.
 
“Hata mkiwasikiliza wanapokosoa sera zetu lakini mkiuwaliza wao watafanyaje hawana majibu. Hoo maisha magumu sana ukiwasikiliza watafanya nini hawana la kujibu.
 
“Hawasemi nini watafanya kuhusu afya, miundombinu, umoja wa kitaifa wanachozungumza ni kwamba kuna matatizo, ukiuzali matatizo yapo nasema yapo na ndio maana unatafutwa ufumbuzi wa matatizo.
 
Kinana alisema kuwa Rais Samia ambaye wanamsema ndiye ameleta uhuru wa kusema, kushutumu, kuandamana. Mikutano ya hadhara wanaweza kusema iko katika Katiba lakini huko nyuma wakati wananyimwa kwani haikuwepo kwenye Katiba?.
 
“Katiba ilikuwepo, uhuru ulikuwepo lakini walikatazwa kwenda barabarani. Amekuja Rais muungwana ameondoa kifungo. Akisema kuanzia leo hakuna maandamano, watafanya? Wanamkejeli na kumtuhumu Rais amekaa kimya.
 
“Waamuzi ni wao. Wana CCM dawa yao kwenye sanduku la kura, wenzetu wanatafuta nguvu katika sanduku la kura
 
Watanzania hawapendi kejeli. Nina uhakika adhabu watakayopata watajutia.
 
Kinana alisema kuwa wakati Rais Samia anachukua madaraka ujenzi wa reli ya SGR ulikuwa asilimia 21 lakini sasa umefikia asilimia 96 na ujenzi wa makao makuu Dodoma ulikuwa asilimia 31, sasa ni asilimia 83.
 
“Waliojenga makao makuu ya Dodoma ni watu wawili Rais Magufuli na Rais Samia. Tangu mwaka 1973 kila Rais alipotaka kujenga makao makuu ya Dodoma hoja iliyojitokeza ni gharama.
 
“Amekuja Rais Maguful amesema songa mbele, wakati Rais Samia anachukua uongozi ujenzi ulikuwa asilimia 31, angeweza kukaa na baraza lake la mawaziri na kusema twende polepole , lakini alisema kila alichoanza mwenzake atahakikisha anamalizia,” alieleza.
 
Akijibu hoja ya Katiba, sheria mpya ya uchaguzi na muungano Kinana alisema ukisikiliza kwa makini utabaini wanataka kuleta mfarakano kati ya bara na Zanzibar.
 
“Wamekuwa wakizunguka na ajenda ya kuligawa taifa katika majimbo, hii ni sera ambayo wamekuwa nayo kwa muda. Msimamo wa CCM Watanzania tusikubali kugawanywa kwa namna yoyote,” alisema Kinana.
 
Alifafanua kuwa CHADEMA wamekuwa wakitumia kanuni ya tengeneza uongo na kisha urudie mara kwa mara hadi watu waamini. “CHADEMA wanasema uongo wanarudia kila wakati ili Watanzania waamini lakini hakuna shaka Watanzania hawataamini.”
 
Kuhusu Hoja ya Katiba mpya, Kinana alisema kulifanyika mazungumzo kwa mwaka mzima baina ya CHADEMA na CCM na kwa maoni yao walisema si ajenda yao ya sasa, lakini wakashawishiwa na Kamati Kuu wakakubali.
 
“Ina maana ukiwa na hoja tunakusikiliza na tunaikubali, tunachobishania ni lini lakini sio hivyo tulikuwa katika Baraza la vyama vya siasa ambalo linahusisha vyama vyote, tulikubaliana.
 
“Kimsingi Katiba hatukatai lakini wenzetu wanataka Katiba ipatikane leo, katika kile kikao walituambia tunaelewa Katiba hii haitakuwa leo lakini tunawasihi mkubali uwepo wa Katiba, tukatoa tamko na muda mwafaka tutakubaliana. Rais wakati anaondoa zuio la mikutano ya hadhara alisema tunakubali kutakuwa na Katiba.
 
“Lakini alishauri tutaangalia je tuchukue Katiba mpya na tume mpya, au tuchukue Katiba iliyopendekezwa na tuifanyie marekebisho au tuchukue mchanganyiko ili tupate Katiba mpya.
 
“Wenzetu wanasema wanataka Katiba sasa, katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam Rais alisema Katiba mpya haiwezi kuwa ya vyama vya siasa peke yao,”alisema na kuongeza Katiba ya sasa imefanyiwa marekebisho mara 14 na sababu ukiangalia sio mambo yaliyohusu wananchi bali ni Siasa, madaraka na uchaguzi,”alisema.
 
Aliongeza CHADEMA wanataka Katiba mpya lakini CCM imekubali , inasema Katiba itakuja lakini jambo kubwa wanalishughulika nalo ni uchaguzi. Serikali imetunga sheria na tayari Rais ameweka sahihi lakini kabla ya sheria haijapita wadau waliitwa kwenda kutoa maoni.
 
“Walitoa maoni mengi, hoja ya msingi zikakubaliwa.CHADEMA walikwenda kama Chama, BAVICHA na BAWACHA wakatoa maoni lakini bado hawaridhiki.”
 
Hoja zilizotolewa rais asiteue tume serikali ya CCM imekubali maoni yale, wanasema haitoshi, majina yapendekezwe serikali imekubali rais amesema sawa pendekezeni leteni majina.
 
“Wamesema tume isitegemee bajeti, hakuna lililopendezwa la msingi ambalo tumelikataa, bado wanasema rais asihusike kwa namna yoyote kumpata mwenyekiti wa tume na makamu wake.
 
 
 
Sijawai kuona duniani rais hana kauli kuhusu tume…sijui wanataka malaika wa kuongoza tume hizi,”alisema.
 
Kwa mujibu wa Kinana, sheria iliyopitishwa na Bunge ni bora kuliko iliyotumika mwaka 2015 na 2020.
 
“Kwa sheria hii nawahakikishia tume itafanya vizuri,”alieleza,
 
Alisema kuwa wanachofanya CHADEA wanacheza na akili za watu, wanatunga uongo na kwenda mbele za watu
 
“Wenzetu wameng’ang’ania katiba na sheria ya uchaguzi kama njia ya ushindi.
 
Sera nzuri, kukubalika kwa chama, wagombea na kujipanga kuna mchango mkubwa katika ushindi,” alisema na kuongeza kuwa hakuna tume duniani ambayo Rais hana nguvu, wanachotaka CHADEMA kwa namna yoyote Rais asihusike, hilo jambo haliwzekani.
 
Kinana alisema CHADEMA wanataka kama jambo hawalitaki Watanzania wengine nao walikatae ambpo alisema kuwa lazima taifa likatae utaratibu huo.
 
“Ukiwasikiliza CHADEMA huwezi kujua wanataka katiba, sheria ya mpya ya uchaguzi, wanajiandaa kwa uchaguzi au wanataka mabadiliko madogo katika katiba.
 
“CHADEMA tuwaulize wanataka nini
 
Katiba, tume nyingine, mabadiliko ya katiba na hapo hapo wanasema tujiandae,” alihoji.
 
 
 
KUHUSU MUUNGANO
 
Akizungumzia hoja ya muungano, aliwapongeza Watanzania kwa kuadhimisha miaka 60 ya muungano ambao umekuwa wa mfano duniani.
 
Alisema muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulozaa Tanzania, umepitia kashikashi nyingi, mambo mengi lakini waasisi wa taifa walijenga misingi imara ya kuulinda.
 
“Hakuna mtu wa kutufarakanisha, wapo waliojaribu kuuvuruga muungano lakini hawakufika mbali. Baada ya kushindwa kuvuruga umoja wetu sasa wameanza hoja nyingine wanasema mbona Zanzibar ni ndogo inakuaje na wabunge wengi,” alisema.
 
Akifafanua kuhusu hoja ya CHADEMA kuigawa nchi katika majimbo, alisema haina afya kwa kuwa ni kudhoofisha umoja wa kitaifa uliopo.
 
“Ajenda hiyo wamekuwa nayo tangu kuzaliwa kwa CHADEMA, Watanzania wameikataa, tusikubali hilo. Baadae watataka Waislamu wawe na eneo lao, Wakristo wawe na eneo lao. Moja ya sifa ya nchi yetu ni umoja wa kitaifa,” alieleza.
 
“Chadema wanajua mambo yote lakini wanataka kutukoroga, nchi imetulia inakwenda vizuri. Watanzania tukatae migawanyiko, tuko tayari kusikiliza hoja za chama chochote au taasisi yoyote lakini tusikubali kugawanywa,” alisema.
Previous Post Next Post