Na Mapuli Kitina Misalaba
Kuelekea kilele cha
maadhimisho ya siku ya Familia Duniani, Mei 15,2024, kampeni ya SMAUJATA Mkoa
wa Shinyanga imewakumbusa wazazi, walezi
na jamii wajibu wa kuendelea kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika shughuli
mbalimbali za kijamii.
Wito huo umetolewa na katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bwana Daniel Kapaya wakati wa kikao cha pamoja na viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu SHIVYAWATA Wilaya ya Shinyanga leo Mei 7,2024.
Pamoja na mambo
mengine Bwana Kapaya ameendelea
kuikumbusha jamii umuhimu wa kushirikiana katika hatua zote za kutokomeza
vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Aidha amesisitiza pia
umuhimu wa kuwekeza kwenye malezi na makuzi ya watoto huku akiiomba jamii
kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya ukatili ili hatua za kisheria ziweze
kuchukuliwa.
“Katika kipindi muhimu cha kuwekeza kwenye Malezi na
Makuzi ya Watoto nkuanzia umei (0) hadi miaka 8; umri
ambao ukuaji wa ubongo wa binadamu hukua kwa takribani asilimia 90; huu ni
ukuaji unaomwezesha mtoto kuwa na uwezo mkubwa wa akili ya kufikiri (darasani),
kupambanua mambo, kujieleza na kutafakari mambo wakati wa utoto hadi anapokuwa
mtu mzima”.
“Hakikisha
afya ya mama na mtoto ipo imara, kabla na baada ya mtoto kuzaliwa ikiwa ni
pamoja na kupata chanjo zote, lishe ya kutosha ya mama na mtoto, mtoto
ajumuishwe mapema ili kupata ujifunzaji na uchangamshi wa awali (shule za
awali) na mtoto alindwe asifanyiwe ukatili wa aina yoyote ikiwa pamoja na
vipigo, maneno ya maudhi na vitendo vingine kama ubakaji na ulawiti”.
“Katika
umri wa mtoto chini ya miaka 18, Mzazi au Mlezi anawajibika kuendelea kuimarisha
malezi na matunzo ya motto, unawakumbusha wazazi na walezi kumpatia mtoto
mahitaji yake ya msingi, kuimarisha ulinzi wa mtoto dhidi ya vitendo vya
ukatili na pia kujenga tabia ya kuwasiliana au kuzungumza na mtoto mara kwa
mara ili kujenga muunganiko (bond) tangu utotoni; hivyo hatua hii itawezesha
mtoto kuwa na upendo kuanzia wakati wa utotoni na siku za mbeleni anapokuwa mtu
mzima (ikumbukwe, wazazi wengi wanalalamika watoto hawawajali na wamekosa
upendo, na hayo ndiyo madhara ya kutokuwa karibu na mtoto tangu umri wa awali)”.
“Toa
taarifa ya vitendo vya ukatili wa mtoto ndani ya siku 3 kwenye vituo vya polisi
ili kupatiwa msaada. Pia unaweza kupiga simu ya bure namba 116 kwa msaada na
huduma zaidi”.
Katika kikao hicho
baadhi ya viongozi wa SHIVYAWATA wameipongeza kampeni ya SMAUJATA Mkoa wa
Shinyanga ambapo wamesema wataendelea kutoa ushirikiano kwa kampeni hiyo katika
kufanikisha malengo yaliyokusudiwa na serikali.
Akizungumza katika
kikao hicho Mwenyekiti idara ya Itifaki, uanachama na uenezi Bwana Solomon
Najulwa amesema SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga itaendelea kutetea haki za watu
wote bila ubaguzi.
Tarehe 15 Mei ya kila
Mwaka, Tanzania huungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia
ambapo maadhimisho ya Mwaka huu yanaongozwa na Kaulimbiu inayosema “Tukubali
Tofauti zetu kwenye Familia; Kuimarisha Malezi ya Watoto”.
Vyama vya watu wenye ulemavu ikiwemo chama cha wasioona, chama kwa watu wenye ulemavu wa akili, chama cha watu wenye ulemavu wa viungo, chama cha viziwi pamoja na sauti ya wanawake wenye ulemavu leo Mei 7,2024 viongozi wake wamefanya kikao cha pamoja na viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga.
Mwenyekiti idara ya Itifaki, uanachama na uenezi Bwana Solomon Najulwa akizungumza
Mwenyekiti wa chama cha watu wenye
ualbino (TAS) mkoa wa Shinyanga Yunice Manumbu akiwapongeza viongozi wa
SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga.