MAAFISA UNUNUZI WAASWA KUTUMIA MIFUMO YA UNUNUZI KIELETRONIKI





Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Chande (Mb.) amewaasa maafisa ununuzi wa taasasi za Serikali kuhakikisha kuwa shughuli zote za ununuzi wa umma zinafanyika katika mfumo wa ununuzi wa umma kieletroniki (NeST) ikiwa ni pamoja na kutumia moduli ya kuwasilisha malalamiko kieletroniki.
Agizo hilo limetolewa na Mhe. Chande wakati wa ufunguzi wa mafunzo siku mbili Jijini Dar es Salaam kuhusu moduli ya uwasilishaji wa malalamiko/rufaa kwa njia ya kieletroniki yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa mikoa ya Dar es Salaam, Tanga Morogoro na Pwani.

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Chande amezielekeza Taasisi zote za serikaali kutumia mfumo wa ununuzi kieletroniki bila kuwa na kisingizio chochote kile.

“Napenda kuzielekeza taasisi nunuzi zote nchini kuhakikisha wanatumia mfumo wa NeST na endapo yatatokea malalamiko basi mshikamane kwa pamoja kati ya mlalamikaji, mtoa haki na mlalamikiwa na kuhakikisha haki inapatikana,” alisema Chande.

Kadhalika, Mhe. Chande amewaelekeza wazabuni kuhakikisha kuwa wanazingatia taratibu za ununuzi wa umma kwa umakini na endapo kunakuwa na ukiukwaji wa taratibu za ununuzi katika michakato husika, wahakikishe malalamiko au rufaa zinazotokana na ukiukwaji wa taratibu hizo, zinawasilishwa kwa kuzingatia muda ulioainishwa kwenye sheria.

“PPAA kwa kushirikiana na PPRA hakikisheni kuwa mnatoa uelewa/mafunzo ya kutosha kuhusu Moduli hii mpya ya kupokea na kushughulikia malalamiko ya wazabuni kwa njia ya kielektroniki ili kuisaidia Serikali kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika katika miradi mbalimbali,” ameongeza Mhe. Chande.

Aidha, Waziri Chande iameielekeza PPAA kuhakikisha kuwa inashirikiana na PSPTB katika maamuzi mnayotoa ili PSPTB waweze kuwachukulia hatua stahiki wataalamu wa ununuzi na ugavi pindi wanaokiuka maadili ya taaluma yao.

Awali Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), Bw. James Sando alisema kuwa Mamlaka ya Rufani iliundwa ili kutatua migogoro itokanayo na michakato ya ununuzi wa umma kwa muda mfupi zaidi tofauti na Mahakama za kawaida ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli, huduma na miradi ya Serikali kwa wakati. “Sambamba na hilo kupitia malalamiko na rufaa zinazoshughulikiwa, Mamlaka ya Rufani inaisaidia Serikali kwa kuhakikisha Sheria ya Ununuzi wa Umma inazingatiwa ili kupata thamani halisi ya fedha zake kupitia ununuzi,” alisema Bw. Sando

Bw. Sando ameongeza kuwa Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mamlaka ya Rufani imeendelea kutekeleza jukumu lake kuu la utatuzi wa migogoro itokanayo na michakato ya Ununuzi wa Umma kwa haki, uwazi, uadilifu na kwa muda mfupi ili kuwezesha upatikanaji wa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi. Aidha, katika kipindi cha miaka mitatu, Mamlaka ya Rufani imefanikiwa katika maeneo ya falsafa ya R nne (4R) za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aakiongelea kuhusu Usuluhishi wa Migogoro (Reconciliation), Bw. Sando amesema kuwa PPAA kushughulikia jumla ya mashauri 150 katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mheshimiwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yaliyotakana na michakato ya Ununuzi wa Umma. Kupitia mashauri hayo yaliyosikilizwa na kutolewa uamuzi, Mamlaka ya Rufani imeweza kudhibiti utoaji wa tuzo kwa wazabuni ambao walipendekezwa kupewa zabuni bila kuwa na sifa stahiki.

Pamoja na mambo mengine, Bw. Sando ameongeza kuwa muda wa ushughulikiaji malalamiko au rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma umepungua kutoka siku saba (7) hadi siku tano (5) za kazi. Kadhalika, muda wa Afisa Masuuli kushughulikia malalamiko ya zabuni kutoka siku saba (7) za kazi hadi siku tano (5) za kazi na pale ambapo Afisa Masuuli ataunda jopo la mapitio ya malalamiko basi atakuwa na siku saba (7) za kazi na atatakiwa kuwajulisha washiriki wote wa zabuni hiyo kuundwa kwa jopo; na muda wa Mamlaka ya Rufani kushughulikia malalamiko au rufaa umepunguzwa kutoka siku arobaini na tano (45) hadi siku arobaini (40).


Previous Post Next Post