MAMBO MATATU YA KUZINGATIA KABLA YA KUFANYA UWEKEZAJI WA MAJENGO ILI UEPUKE “BOMOABOMOA”

 

Nimelazimika kuandika Makala hii kutokana na msukumo mkubwa wa watanzania wengi kutaka kujua hali ya usalama wao katika uwekezaji wa majengo.

Nimepokea simu nyingi kutoka kwa wote waliowekeza na wale ambao bado lakini wapo kwenye mchakato au mipango ya kuhakikisha wanawekeza katika Ardhi na majengo. Mara nyingi katika mazungumzo ya kutaka watanzania wabadilike na waanze kutumia wataalamu katika mambo yao huwa ni jambo la kawaida sana na si rahisi kulizingatia, lakini unapokutana na mkono wa sheria katika eneo ulilowekeza na kuonekana kuna mapungufu au ukiukwaji wa baadhi ya taratibu za ujenzi, hakika hakuna tofauti na kukutana na “shetani mtoa uhai”.

Sheria za ardhi zinapohukumu huwa haijali kuwa ulikosea kwa kujua au kwa kutokujua. Ujenzi ni gharama sana, hugharimu fedha na muda mwingi kufikia mafanikio kamili na yenye tija kwa mmiliki na mtumiaji. Inasikitisha na kuhuzunisha kuona nyumba iliyogharimu fedha nyingi ikibomolewa kwa sababu ambazo zingeweza kuzuilika ikiwa mmiliki angepata taarifa sahihi za ujenzi na taratibu zilizopaswa kufuatwa kabla na wakati wa ujenzi.

Hii ni hasara kwa mmiliki na watumiaji wa majengo hayo. Katika Makala zilizopita nilitoa angalizo mbalimbali ambazo naziona kuwa ni hatari sana kwa siku zijazo kwa watu wengi kukumbwa na “majanga ya bomoabomoa”. Lengo kuu la Makala hii ni kukumbushana umuhimu wa kutumia wataalamu na kufuata taratibu na sera za ujenzi ili kuondokana na ubomoaji usikukumbe.

1. Fanya Utafiti Wa Eneo Lako La Uwekezaji 
Napenda nikukumbushe tena mtanzania mwenzangu kuwa hakuna kipande cha ardhi isiyo na matumizi au isiyo na mmiliki. Pia ardhi yote ya Tanzania na ulimwengu wote inafahamika kwa vipimo mbalimbali na hupangiwa matumizi mbalimbali. Ni serikali pekee kupitia wizara na halmashauri mbalimbali za miji na wilaya ndiyo yenye mamlaka kisheria kupanga matumizi ya ardhi katika eneo husika, haijalishi ardhi imepimwa au haijapimwa.

Hivyo matumizi yeyote ya ardhi lazima yapate kibali kutoka mamlaka husika. Jitahidi sana kufahamu na kuzingatia matumizi sahihi ya sehemu ya ardhi unayomiliki kupitia mamlaka husika katika eneo lako. Ndivyo ilivyo hata katika ujenzi wa majengo, huwa ni jambo la kwanza kufika na kutafiti ili kujiridhisha na maelezo ya umiliki wa eneo kabla ya kuanza uchoraji wa ramani na hatimaye ujenzi.

Hata maeneo rasmi yaliyopimwa kwa ajili ya majengo huzingatia ukubwa na aina ya majengo yanayopaswa kujengwa kwa kila kipande cha ardhi, zingatia matumizi rasmi ya eneo lako kabla ya hatua yeyote ya ujenzi ili kuepuka “bomoabomoa” inayowakumba baadhi ya watanzania. Pia watembelee halmashauri husika na mamlaka nyingine kupata utaratibu na kibali cha ujenzi ambao utazingatia sera na taratibu rasmi za ujenzi. Kwenye maeneo yaliyopimwa kila mmiliki anapewa hati halali ya umiliki wa kipande cha ardhi ndani ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sera na sheria za ardhi. Hati hiyo huwa inaeleza matumizi rasmi ya ardhi hiyo na endapo kuna mabadiliko ya matumizi ni vema ukawajulisha mamlaka husika ili wakusaidie.

2. Andaa Michoro Na Mpango Fedha 
Baada ya kufanya tafiti iliyojitosheleza mahitaji ya taarifa sahihi za umiliki na matumizi ya sehemu hiyo ya ardhi, sasa utakuwa umefahamu ni aina gani ya majengo unapaswa ujenge ili kutimiza adhma yako ya uwekezaji. Na kama ardhi hiyo ipo kinyume na matumizi uliyokuwa umepanga ni vema ukatafuta namna nyingine au mbadala wa uwekezaji huo. Ni vema hatua hii ukajipanga vizuri na zingatia sana utulivu ili mwili na akili vishirikiane kwa umakini katika kupata jibu ni aina gani ya uwekezaji ambao ungependa kufanya kulingana na ndoto zako na aina ya eneo ulipo. Jipe muda wa kutosha wa kujitathmini na kuweka mipango mkakati ya namna ambavyo ungependa kumiliki aina fulani ya majengo itakayokidhi mahitaji husika.

Katika hatua hii mtafute msanifu majengo ambaye ni mtaalamu wa ramani za majengo (Architect), mshirikishe mawazo na mahitaji yako na namna ambavyo ungependa mwonekano wa nyumba iliyo ndani ya akili yako, msanifu majengo atakusaidia kuiweka katika picha ya karatasi kiufasaha na kitaalamu zaidi. Hakikisha mnashirikiana kwa karibu sana ili aweze kukidhi hitaji lako halisia. Naamini kabisa kupitia michoro hiyo ni rahisi kufahamu makisio ya gharama za ujenzi huo ambao utakusaidia kujitathmini kifedha na muda utakao tumia kufanya ujenzi huo.

Pia kwa wale wanaotegemea vyanzo vingine vya fedha kama vile mikopo kutoka benki, mashirika ya hifadhi ya jamii na misaada kutoka kwa wahisani mbalimbali mara nyingi michoro hiyo huambatana na makadirio ya gharama ya ujenzi huo ili kufahamu ni gani kiasi cha fedha zitakazohitajika. Makadirio haya hukuwezesha wewe kujipanga na kufahamu thamani halisi ya nyumba yako ambayo utaitumia kwenye bima na kodi za majengo, pia kwa wawekezaji wakubwa hii husaidia hata pale unapohitaji kuomba msaada wa kusamehewa kodi kulingana na uwekezaji wako wenye tija kwa jamii na taifa kwa ujumla. Pia makadirio ya ujenzi (BOQ) ambayo mara nyingi huandaliwa na mkadiriaji majenzi (QS) huwa ni msaada sana kwa wale wanaojenga kwa hatua ili kuwaongoza kupanga bajeti zao kulingana na kipato. Hakikisha michoro hiyo unaipeleka mamlaka husika kwa ajili ya ukaguzi na kulipia ada mbalimbali kabla ya ujenzi kuanza.

3. Andaa Mpango Mkakati Wa Uwekezaji 
Uwekezaji wa majengo hauna tofauti sana na uwekezaji mwingine katika maendeleo yeyote ya kiuchumi. Hii ndiyo sababu kuu ya kutoa elimu hii kwa watanzania ili waongeze umakini katika kazi hii na waepuke hasara na hatari zinazoweza kuwakabili. Uwekezaji huu upo kwenye ushindani mkubwa sana na uwekezaji wa hisa katika soko la fedha. Uwekezaji huu upo kwenye ushindani kwa kuwa aina hii ya uwekezaji unafanana kwa karibu, ukishawekeza kiasi fulani cha fedha baada ya muda kadhaa huanza kupata faida kulingana na uwekezaji wako pasipo wewe kushiriki kwa ukaribu sana.

Hii ndiyo faida kubwa ya uwekezaji wa aina hii na kivutio kwa wawekezaji wengi kuwekeza katika sekta hizi. Jambo muhimu hapa ni kuwa na maono/malengo makubwa ya aina ya uwekezaji unaotarajia kuwekeza (master-plan), vyanzo mbalimbali vya fedha vitakavyo wezesha uwekezaji huo (Mshahara, Biashara, mkopo au msaada) na muda rasmi utakaotumia kuanza hadi kukamilika kwa ujenzi huo, tathmini ya namna gani na baada ya muda gani uwekezaji huo utarejesha fedha halisi zilizotumika, na faida itapatikana baada ya muda gani wa uwekezaji huu. Kutokuwa na mpango fedha kutasababisha ufeli ka urahisi na kama ulikopa benki utakuwa kwenye hatari Zaidi. Endapo utawashirikisha wengine tafadhali zingatia sana makubaliano yenye usawa kwa pande zote mbili ili endapo mambo hayatoenda vema ni hatua gani zifuatwe ili kila mmoja ajilizishe. Pata muda mwingi wa kuandaa na kuhakiki makubaliano yenu kabla ya kuwa pamoja kuendesha uwekezaji huu.

Ndugu msomaji wa Makala hizi, nimeandika hayo machache lakini kuna mengi ya kuzingatia, binafsi nimekutana na mengi sana kwenye harakati hizi, yameniumiza moyo sana. Ikiwa wewe unafahamu kuwa ulijenga bila kibali au umejenga pasipo kupima eneo, tambua kuwa ipo siku utakutana na majanga haya. Ili maisha yaendelee ni lazima watu wote waweze kufikiwa na huduma zote za kijamii, lakini wengi hawapati haki hii kutokana na ujenzi holela ulioachwa uendelee kwa miaka mingi iliyopita.

Pia ili upate huduma za kijamii ni lazima ulipe kodi/ushuru ili uzipate kwa ubora unaotakiwa, katika mfumo wa ujenzi usio rasmi ni vigumu kwa serikali kukusanya kodi za majengo hivyo utailazimisha serikali kufumua baadhi ya nyumba ili ipate kuweka mfumo rasmi wa kukusanya mapato yake. Haya ni matokeo ya udhaifu mkubwa kwa serikali iliyopita kwa kushindwa kuwajibika na hatimaye kuwaacha watanzania kutumia rasilmali pesa kujenga pasipo utaratibu rasmi hali ambayo itawagharimu siku za usoni. Ni kosa kubwa kwa mamlaka husika kusubiri mtu amalize ujenzi baadae uje kubomoa ikiwa uwezo wa kumzuia hapo awali ulikuwepo.
Previous Post Next Post