Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt Jabiri Bakari amewasisitiza waandishi wa habari na watoa huduma za utangazaji kuzingatia maadili,kanuni na sheria za kutoa huduma hiyo kwani sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kujenga jamii bora na kuleta maendeleo ya jamii na Taifa.
Dkt. Bakari amesema hayo Jumatano Mei 29,2024 katika warsha kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Mwanza iliyoandaliwa na TCRA ili kuwajengea uwezo na kuwakumbusha kanuni za utangazaji na maudhui mtandaoni.
Dkt. Bakari amesema lengo la TCRA ni kukuza ubunifu na kuwapa nafasi ya kuanzia vijana wasio na ajira rasmi hivyo watumie fursa ya mtandao katika kujenga jamii bora.
Aidha Dkt. Bakari amesema TCRA imeshaanza mchakato wa kuwatambua watoa huduma za utangazaji, blogs na maudhui mtandaoni wanaofanya vizuri katika kufuata kanuni na ubunifu
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari akitoa maelekezo kwa waandishi wa habari.
“Sisi tunaozalisha na kusambaza taarifa zinazoenda kwa watu walio wengi, wapokeaji taarifa wanatengenezwa kutegemeana na taarifa ambayo wameipokea,” amesema Dkt Bakari.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Imelda Salum amesema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inahimiza ushindani katika utoaji wa huduma bora ili kuchangia ustawi wa wananchi na maendeleo.
"TCRA itaendelea kushirikisha wadau katika kutatua changamoto katika ukuaji wa sekta ya utangazaji lakini pia tutaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha sekta ya Utangazaji inatoa mchango katika maendeleo ya nchi",amesema Mhandisi Imelda.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Imelda akizungumza.
"Endapo namba ya simu, email unayotumia kuwasiliana na TCRA haipo, tafadhali weka taarifa ili iwe rahisi kwa mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kuwasiliana na watoa huduma, sisi hatuhitaji kumuacha mtu nyuma, tunataka kila mmoja wetu atumie mfumo wetu wa Tanzanite Portal. Tunataka tufanye mawasiliano kupitia mfumo huu".
"Uhalisia ni kwamba Teknolojia imebadilisha mambo mengi, hivyo Vyombo vya habari vinatakiwa kuwa wabunifu ili vipate Matangazo. Vipindi vyenye viashiria vya kuhamasisha Ushoga haviruhusiwi, tusiiachie mamlaka, ukiona kuna kipindi chenye viashiria vya ushoga kwenye chombo cha habari, toa taarifa TCRA", ameongeza Mhandisi Imelda.
Meneja huyo pia amesisitiza waandishi wa habari kujikita zaidi katika kuchakata na kusambaza maudhui ya ndani ili kujenga jamii imara.
Kikao cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na waandishi
wa habari kikiendelea jijini Mwanza ambapo kimelenga kuwakumbusha
watoa huduma ya maudhui mtandaoni kuzingatia kanuni na kujadili namna
bora ya kuboresha urushaji wa maudhui mtandaoni pamoja na Kanuni za Utangazaji
wa Uchaguzi kwa vya Siasa.