MWANAFUNZI CHUO CHA SAUTI MWANZA AFARIKI AKIOGELEA






Aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo Cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Kampasi ya Mwanza Boaz Sanga

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza Mrakibu Kamila Labani

Kikosi cha uokoaji kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza wakiwa ndani ya ziwa Victoria kwaajili ya kuutafuta mwili wa aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo Cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Kampasi ya Mwanza Boaz Sanga.
………………

Na Hellen Mtereko, Mwanza

Aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo Cha Mtakatifu Augustino( SAUT) Kampasi ya Mwanza Boaz Sanga, amefariki dunia baada ya kuteleza kwenye mwamba na kuzama ndani ya maji wakati akiogelea ziwa Victoria.

Hayo yamebainishwa  Alhamisi Mei 2, 2024 na Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Mrakibu Kamila Labani wakati akitoa taarifa ya tukio hilo kwa waandishi wa habari.

Amesema Boaz Sanga (22) alienda na wenzake wawili mtaa wa Sweya Kata ya Luchelele Wilaya ya Nyamagana kwaajili ya kupiga picha kisha wakaingia ndani ya maji kwaajili ya kuogelea ndipo akazama kutokana na kina cha maji kuwa kirefu.

Mrakibu Labani ametoa wito kwa watumiaji wa ziwa Victoria pamoja na mabwawa kuchukua tahadhari pindi wanapokuwa katika maeneo hayo.

Japhet Njaule ni Mlezi wa wanafunzi katika Chuo hicho, amesema wanajitahidi sana kutoa elimu hususani kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza kuepuka kuogelea kwenye maeneo ambayo hawayajui.

Aidha, ametoa shukrani kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza kwa jitihada walizozifanya za kuutafuta mwili wa Boaz Sanga.
Previous Post Next Post