Ticker

6/recent/ticker-posts

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA SHINYANGA YATOLEA UFAFANUZI HATIMA YA KESI YA UBAKAJI WA MTOTO


Ofisi ya taifa ya Mashtaka (NPS) mkoa wa Shinyanga, imetoa ufafanuzi juu ya hatima ya kesi ya mtoto mwenye umri wa miaka 3 aliyedaiwa kubakwa na kijana wa nyumba ya jirani katika Kijiji cha Jomu kata ya Tinde Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, mnamo mwezi Februari mwaka jana 2023.

Mkuu wa Mashtaka wa mkoa wa Shinyanga Bi. Ajuaye Bilishanga ameiambia Redio Faraja kuwa, kesi hiyo iliyofunguliwa mnamo tarehe 04.04.2023, ilisikilizwa na kutolewa hukumu kwenye Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga mnamo tarehe 27.09.2023.

Amesema kesi hiyo ilikuwa ikisimamiwa na Wakili Goodluck Saguya ambapo baada kukamilika kwa utaratibu wa kuaandaa ushahidi, Mama wa mtoto na mtoto mwenyewe waliitwa na kufika Mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi wao, lakini tokea siku hiyo hawakufika tena Mahakamani mpaka kesi ilipotolewa hukumu.

Bilishanga amebainisha kuwa, Ofisi ya Mashtaka haikuwa na sababu ya kumwita tena Mlalamikaji kwa sababu alikuwa tayari amekwishatoa ushahidi wake Mahakamani na kwamba, jukumu la kufuatilia mwenendo na hatima ya kesi ni haki ya Mlalamikaji mwenyewe.

Mkuu huyo wa Mashtaka mkoa wa Shinyanga amefafanua kuwa, Ofisi ya Mashtaka ilifanya jitihada kubwa ili kuhakikisha haki ya mtoto huyo inapatikana, lakini Mahakama ilimwachia huru Mshtakiwa kutokana na utetezi aliowasilisha Mahakamani ikiwemo umri wake kuwa chini ya miaka 18.

Amesema Mahakama ilimwachia huru Kijana huyo baada ya kuwasilisha Mahakamani hapo cheti chake cha kuzaliwa ambacho kilionesha alikuwa na umri wa miaka 17 wakati huo badala ya miaka 19 iliyokuwa imeandikwa kwenye hati ya Mashtaka na kwamba, kwa mujibu wa sheria alipaswa kushtakiwa katika Mahakama ya watoto kama mtoto badala ya mtu mzima.

Hoja nyingine iliyotolewa na Mahakama na kuchangia Mshtakiwa kuachiwa huru ni ushahidi wa Madaktari ambao ulionesha kuwa, mtoto huyo alikuwa akifanyiwa vitendo hivyo (kubakwa) kwa muda mrefu na hivyo Mahakama ikashindwa kuthibitisha pasipo shaka endapo alifanyiwa kitendo hicho siku ya tukio na Mshtakiwa aliyetajwa.

Ufafanuzi huo wa Ofisi ya Mashtaka unakuja kufuatia Mama wa mtoto anayedaiwa kufanyiwa ukatili kueleza kutojua hatima ya kesi ya mwanae baada ya kufikishwa Mahakamani tangu mwaka jana 2023, wakati akizungumza kupitia kipindi cha Mwanamke na maisha ambacho kinaandaliwa na Redio Faraja kwa kushirikiana na Mfuko wa Ruzuku kwa wanawake Tanzania (WFT-T) kinacholenga kusaidia mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA)

Ofisi hiyo imeahidi kuendelea kutoa elimu zaidi kwa umma kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo Redio Faraja, ili wananchi wafahamu namna inavyotekeleza majukumu yake na namna ambavyo wananchi wanapaswa kushiriki katika mwenendo wa kesi.

Post a Comment

0 Comments