Siku moja niliwakuta walimu watatu wakibishana kuhusu uwezo wa wanafunzi wao. Mmoja alisema John ana akili zaidi kuliko Ali.
Wenzake walipomuuliza kwa nini akasema ni kwa sababu katika mtihani yeye huwa anashika nafasi ya kwanza. Mwalimu mwengine akampinga mwenzake kwa kusema kuwa John hana akili sana kwa sababu yeye hutumia karibu wakati wake wote kwa kusoma wala huwa hana muda wa kushiriki katika shughuli nyingine za nje ya darasa.
Alisisitiza kuwa Ali ana akili zaidi kuliko John kwa sababu yeye huwa wala hatumii muda wake kwa kufungua kitabu na kusoma. Mwalimu anapofundisha yeye husikiliza kwa makini na kushika maudhui ya mambo aliyofundishwa. Tena kwenye majadiliano yeye huweza kutoa hoja na kuchambua mawazo na maudhui.
Mwalimu wa tatu aliyekuwa akiwasikiliza akabisha kuwa wote wawili hawana akili kama Maganga kwani ana akili za kufanya vitendo.
Akaendelea kusema kwa mfano umeme unapokatika ghafla yeye huweza kuchunguza akatambua kama ni shoti au umezimwa na Shirika la Umeme (Tanesco). Kama ni kasoro katika nyumba huweza kuchunguza na kugundua tatizo na hata pengine kulirekebisha kama ni dogo. Mwalimu huyu akamalizia kwa kusisitiza kuwa hii ndiyo akili ya kweli kuliko wenzake wale wawili.
Wakati walimu hawa watatu wakijadiliana kulikuweko mwalimu mwingine kando aliyekuwa akiwasikiliza. Yeye akaingilia kati majadiliano yao kwa kusema. “Wote hawa mliowataja hawana akili kama mtoto wa miaka saba aliyeko katika shule ya jirani.
Yeye ingawa bado yuko katika shule ya chekechea akimsikiliza mtu anasoma ubeti mmoja au miwili na hata beti tatu za shairi akarudia mara tatu yeye anaweza kurudia kuzisema beti hizo bila kukosea hata neno moja”.
Mwalimu huyu ndiye aliyesababisha ubishaji mkubwa zaidi.
Wale walimu wote watatu wakakataa kuwa itawezekanaje mtoto wa miaka saba akawazidi watoto wakubwa wa takribani miaka 12 na zaidi. Wakaishia kusema hiyo siyo akili ni kipaji maalumu.
Lakini yule wa kwanza akaongezea kwa kusema, “Hivi hamjui kwamba binadamu huanza kujifunza mambo mbalimbali anayofanya tangu alipokuwa angali mdogo na pengine hata hujifunza tangu akiwa ndani ya tumbo la mama yake”
Mtoto anapozaliwa tu huweza kuanza kupumua, kumeza maji, maziwa au vyakula, kulia na vitendo vingine kadha wa kadha. Vitendo hivi mtoto huvifanya kutokana na silika ya asili.
Yaani uwezo uliomo katika mwili wa binadamu au kiumbe kingine chenye uhai unaokiwezesha kufanya vitendo vya kukifanya kibaki hai na kiweze kuishi.
Lakini kabla hujaendelea kusoma hebu jiulize wewe mwenyewe. Hivi kweli wewe unakubali kuwa John ana akili kuliko wenzake kwa sababu huwa anafaulu mitihani? Je, wewe unaamini kabisa kuwa Ali amewazidi wote kwa sababu yeye huwa anasikiliza kwa makini yale anayofundishwa wala hahitaji kukaa kuyasoma peke yake ili aweze kuzingatia? Au wewe unaridhika kuwa Maganga anawazidi kwa akili kwa sababu anaweza kufanya kwa vitendo akachunguza tatizo kwenye mtambo, akabaini sababu na kisha akarekebisha kasoro iliyopo kwa kufanya ufundi wake yeye mwenyewe. Au unafikiria nini kuhusu mtoto wa umri mdogo anayeweza kusikiliza shairi mara mbili au tatu halafu akalirudia kwa usahihi bila kusoma.
Ni dhahiri siyo rahisi kuamua yupi aitwe ana akili kuliko wenzake.
Hata wale walimu wanaweza kubishana siku nzima wasifikie muafaka wa pamoja. Hata hivyo, ni vyema tuendelee kusoma makala haya.
Natumaini tutakapofika mwisho tutaweza kupata sababu za msingi.
Hebu kwanza tuwaulize wataalamu maana ya akili. Nini maana halisi ya akili?
Wanasaikolojia hulitafakari neno akili kwa kuzingatia mtazamo wa kisayansi badala ya dhana, fikira au mawazo matupu.
Fikara au dhana kama vile kupata alama nzuri katika mitihani, au kuwa na stadi za kufikiri na kudadavua mawazo au fikira au ustadi wa kifundi au kiteknolojia na hata uwezo wa kukumbuka mambo mengi, kimsingi yote haya yanahusiana na ukomavu wa ubongo wa mtu, urithi wa kiukoo na hasa umri.
Akili siyo rahisi sana kuitafsiri kwa maana moja inayokubalika kwa wote. Katika kamusi ya kishwahili sanifu maana ya akili imeelezwa kwa kutaja maneno kadhaa kama vile akili ni fahamu, hekima, ujuzi, welekevu, busara, maarifa, werevu. Vilevile wameongezea maneno mengine kama maana ya pili ya neno akili.
Maneno haya ni uwezo, ujanja, uamuzi na uteuzi. Hapana shaka orodha hii ya maneno haituwezeshi kuelewa maana ya akili.
Kwa mukhtadha wa makala hii akili ni “Uwezo au weledi wa kutafuta jibu au utatuzi wa tatizo au changamoto”.
Hata hivyo, changamoto nyingi ni nyepesi na zinahitaji uwezo mdogo tu; Lakini kuna changamoto nyingine ngumu zinazohitaji kiwango kikubwa cha akili. Hii ndiyo maana pia kuna viwango vinavyotofautiana vya akili kama vile viwango vya haiba. Baadhi ya watu huonyesha kiwango kidogo aidha, wengine huonyesha uwezo mkubwa wa akili hadi wakaitwa watu wenye akili nyingi.
Waliobakia ambao ndiyo kundi kubwa ni wale ambao kutokana vitendo vyao vinaonesha kuwa uwezo wao wa kiakili unatandawaa kati ya wale wenye kiwango cha chini sana cha akili na wale wenye kiwango cha juu.
Lakini ili tukamilishe uelewa wetu wa akili inabidi turudi kwenye walimu watatu niliowaeleza mwanzo wa makala hii. Wao walikuwa wakibishana juu ya maana tuliyonayo tunaposema mtu fulani ana akili. Hebu tuligeuze swali lao liwe mtu asiye na akili yukoje? Tunaweza kumueleza mtu wa namna hii kwa vigezo viwili. Kwanza mtu asiye na akili ni yule ambaye hana uwezo wa kubaini au kutambua wazo kuu kuhusu jambo fulani lililomo katika kichwa chake au maelezo ya mtu mwingine au hata kuchanganua jambo fulani. Pili ni yule anayerudiarudia tena na tena kosa fulani na akashindwa kujifunza kutokana na uzoefu. Kwa hakika, mtu mpumbavu ni yule anayeshindwa kutumia alichojifunza zamani kwa kukabiliana na changamoto mpya inayomkabili. Kufuatana na dhana hii tunaweza kuipamba tafsiri ya akili kwa kusema “Ni uwezo wa kuitambua changammoto na kuweza kuitatua au kuipatia jibu kutokana na kile amabcho mtu aliwahi kujifunza zamani.
Je wanyama wana akili?
Kila mara wanasaikolojia wanapozungumzia akili hupenda kuelezea kuhusu wanyama ili kukazia maarifa. Inatubidi tujaribu kidogo kuchanganua tofauti kati ya akili ya binadamu na mnyama.
Tunapotaja wanyama tunajumuisha pia wadudu na ndege. Kiumbe chochote kama ni binadam, au mnyama chenye uwezo wa kujifunza kina kiwango fulani cha akili.
Lakini inabidi tukumbuke kama nilivyoeleza mwanzoni mwa makala hii iko tofauti ya kutenda kutokana na akili na kutokana na silika. Mtoto mchanga anapolitafuta ziwa la mama yake na akalenga kwa usahihi kwenye chuchu ili anyone siyo kwamba anatumia akili ya kujifunza bali ni uwezo wa silika.
Ukilichunguza sega la asali la nyuki utastaajabu jinsi lilivyotengenezwa kwa ustadi na jinsi maumbo yake yalivyotengenezwa na nyuki kwa vipimo na maumbile ya kufanana kabisa. Licha ya kutofundishwa namna ya kutengeneza vitu hivyo wala nyuki huwa hana vifaa hata kama rula ya kipimia vipimo au kunyooshea msitari.