SERIKALI imesema imebuni miradi
mbalimbali ya kimazingira inayosaidia jamii kuweza kuhimili athari za
mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Pamoja na hatua hizo pia,
imeendelea kuihimiza jamii kutumia nishati mbadala na majiko banifu ili
kupungunguza kasi ya ukataji wa misitu ambayo husababisha uharibifu wa
mazingira.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri
Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas
Katambi wakati akijibu maswali bungeni kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo bungeni jijini
Dodoma leo tarehe 06, 2024.
Akijibu swali la Mbunge wa Mwera
Mhe. Zahor Mohammed Haji aliyetaka kujua mpango wa Serikali kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi katika kuwakinga wananchi na madhara yanayoweza
kutokea, Mhe. Katambi amesema Serikali inatekeleza miradi ya upandaji miti,
usambazaji wa maji safi kwa matumizi ya majumbani na mifugo na ujenzi wa
miundombinu ya umwagiliaji.
Ametaja ujenzi wa kuta katika
maeneo ya fukwe za bahari yanayokabiliwa na mmomonyoko wa ardhi, ujenzi matuta
na mabwawa kudhibiti mafuriko, kuwezesha jamii kubuni miradi mbadala ya
kuongeza kipato na iliyo rafiki kwa mazingira pamoja na urejeshaji wa maeneo ya
ardhi yaliyoharibika kuwa ni jitihada zingine za kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi.
Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe.
Katambi amesema Serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na
Mabadiliko ya Tabianchi (2021), Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (2022-2032) na Mchango wa Taifa katika Kukabiliana na Mabadiliko ya
Tabianchi (2021) ambayo ina mchango katika kukabiliana na changamoto hiyo.
Ameongeza kuwa Serikali
inashirikiana kikamilifu na jumuiya ya kimataifa katika kubuni mikakati na
hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika ngazi zote
ikiwemo kuridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi,
Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris.
Aidha, Naibu Waziri Katambi amesema
Serikali inaendelea kuelimisha wananchi kuhusu madhara yanayotokana na
mabadiliko ya tabianchi ili waweze kuchukua tahadhari na kujilinda na maafa
yanayosababishwa na changamoto hizo, ambapo uelimishaji hufanyika kabla ya
maafa kutokea.