Na Moshi Ndugulile
Waandishi wa habari wanawake viongozi wametakiwa kuongeza kasi na kufanya mapinduzi ya kutumia teknolojia ya habari katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia katika mabadiliko hayo
Rai hiyo imetolewa na katibu mtendaji wa Baraza la habari Tanzania MCT Bwana Ernest Sungura kwenye ufunguzi wa mafunzo kwa baadhi ya waandishi wa habari wanawake viongozi katika redio na runinga,yanayofanyika Mjini Morogoro
Amesema matumizi ya teknolojia ni fursa kwa wote na kwamba itawawezesha kujenga ushawishi mkubwa katika masuala au agenda mbalimbali badala ya kubaki nyuma
Bwana Sungura amewataka waandishi wa habari wanawake viongozi katika vyumba vya habari kujitambua hali itakayowawezesha kujiamini zaidi na hivyo kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwenye maeneo ya kazi na mazingira yoyote ya aina hiyo
Amewataka kutumia nafasi hiyo, ujuzi na maarifa waliyo nayo kuwajengea uwezo wanawake wengine katika tasnia ya habari ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa na hasa ajenda ya kupambana na unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo ya kazi
Amewataka kutowekeana vikwazo na kuoneana wivu katika hatua zote za kutafuta mafanikio na badala yake amewasisitiza kukuza umoja,mshikamano na kushirikiana zaidi katika maeneo ya kazi
Amewakumbusa kuhusu umuhimu wa Mwanamke katika jukumu la kusimamia malezi na makuzi ya mtoto ambapo pia amewataka kuweka uwiano mzuri katika maisha ya kazi lakini pia maisha katika malezi ya familia.
Katibu huyo mtendaji wa MCT amesisitiza viongozi hao kuzingatia mafunzo waliyopata ili kwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo katika vyumba vya habari kuimarisa na kuanzisha madawati ya kijinsia katika sehemu za kazi,kuandika maudhui yenye mtazamo wa usawa wa kijinsia,kuanzisha vipindi maalumu vya redio,TV na mitandao vyenye maudui ya usawa wa kijinsia.
Awali afisa wa baraza la habari Tanzania MCT, Bi Ziada Mlolo ametaja malengo ya kutolewa kwa mafunzo hayo kwamba ni kuwekeza katika ujuzi na taaluma kwa maendeleo ya sekta, kuongeza ufahamu kwenye masuala ya usawa wa kijinsia na kuboresha maudhui yanayozingatia usawa wa kijinsia,kuweka bayana nafasi ya mwanamke katika vyombo vya habari ili waweze kujitambua na kujua nafasi na wajibu wao kwa maslahi ya jamii wanayoihudumia
Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa awamu ya saba kwa wanawake viongozi katika vyumba vya habari katika Mikoa ya Dar es Sakam, ,Kilimanjaro,Arusha,Zanzibar na Morogoro baada ya kufanyika utafiti kati ya MCT kwa kushirikiana na taasisi ya maendeleo ya vyombo vya habari ya Finland (VICES) 2019 ambapo ilibainika kuwa hakuna usawa wa kijinsia kati ya waandishi wa habari wanawake na wanaume hali ambayo imechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo mifumo.
Mafunzo hayo yaliyoanza Mei 29, yatahitimishwa June mosi 2024 yakihusisha waandishi wa habari wanawake vongozi wpatao 14 kutoka katika baadhi ya vituo vya redio na runinga Mikoa ya Tanzania bara na visiwani ikiwa ni mwendelezo wa mafunzo mengine yaliyofanyika tangu kuanza kutekelezwa kwa mradi huo Mwaka 2019 hivyo kufanya idadi ya washiriki kufikia 120
Kauli mbiu ya mafunzo hayo inasema “sisi wanawake pamoja tunashinda”
Post a Comment