-Wawatuhumu kuogopa kuulizwa uuzaji wa ardhi

Na Mwandishi wetu, Simanjiro 

WAKAZI wa Kijiji cha Loiborsiret Wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamewashukia Mwenyekiti wa kijiji hicho  Kimaai Saruni na Mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo Aloyce Teme kwa kukacha mkutano wa Diwani wa kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga (Maridadi).

Wananchi hao wamedai kuwa viongozi hao wamegoma kushiriki mkutano wa Diwani wao wa kusoma taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa kuhofia kuulizwa maswali magumu juu ya uuzwaji wa ardhi ya kijiji hicho.

Mmoja kati ya wakazi hao Lazaro Lambagi amesema hofu ya kuulizwa maswali magumu kutokana na kuuza ardhi kumesababisha viongozi hao kutohudhuria mkutano huo.

"Aliyekuwa DC Simanjiro Dkt Suleiman Serera aliagiza viongozi kusimamisha uuzaji ardhi hadi uchaguzi wa serikali za mitaa upite ila hawa wao wameendelea kuuza kwa kificho na kuogopa mikutano," amesema.

Mkazi mwingine Kalai Mollel amesema viongozi hao wameshiriki kuuza eneo la ardhi ya kitongoji cha Oltepelek kwa kuong'oa vibao vya eneo la malisho na kuviweka ofisi ya kijiji cha Loiborsiret.

" Tumelalamikia suala hili la uuzwaji ardhi kwa muda mrefu ila viongozi hawa wamekuwa wabishi ila mwisho wao umefika kwani wauza ardhi wote tumewabaini,"  amesema Mollel.

Kwa upande wake Leronjo Lembaji amesema amesikitishwa na viongozi hao kususia mkutano wa Diwani anayetokana na CCM.

Naye, Mwenyekiti wa kijiji cha Loiborsiret, Kimaai Saruni amesema hakuwa na taarifa ya kufanyika kwa mkutano huo wa Diwani ndiyo sababu hakuweza kuhudhuria.

Kimai hakuwa tayari kuzungumza juu ya tuhuma za yeye kuuza ardhi akieleza kuwa atazungumza suala hilo siku nyingine.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM kata ya Loiborsiret, Aloyce Teme amesema hakuweza kuhudhuria mkutano huo kutokana na kutokuwa na taarifa.

"Suala la kuuza ardhi ya kijiji anayetakwa kuulizwa ni Mwenyekiti wa kijiji ila nilishindwa kufika kwenye mkutano kwa sababu sikualikwa," amesema Teme.

Afisa mtendaji wa kata hiyo, Mary Chisoji amesema taarifa za kuwepo kwa mkutano huo zilishatolewa kwa barua kwa viongozi wote wa eneo hilo.

Chisoji amesema kuhusu suala la uuzwaji ardhi holela wenyeviti wote walishapewa onyo la kutouza ardhi hadi uchaguzi wa serikali za mitaa utakapofanyika.

"Hili la kurejeshwa kwa vibao viling'olewa vya malisho kitongoji cha Oltepelek tutavirejesha baada ya wiki moja wananchi msijali kuhusu hilo," amesema Chisoji.

Afisa mtendaji wa kijiji hicho Upendo Menaki Sawaki ambaye ameshiriki mkutano huo amesema viongozi wote walipewa taarifa ya kuwepo mkutano huo hivyo kitendo cha kudai kuwa hawana taarifa siyo sahihi.

Hata hivyo, Diwani wa Kata hiyo Ezekiel Lesenga Maridadi amesema kitendo cha viongozi hao kususia ziara yake kimemkwaza na kumsikitisha kwani kimeonyesha ni siasa chafu.

"Nimekuja kuelezea utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kupitia mikutano ili tuone mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan na kusikiliza kero na changamoto za watu ila viongozi hao hawakufika," amesema.

Amesema suala la kung'olewa vibao vya eneo la malisho atalisimamia ipasavyo kwani yeye hakuwepo wakipanga matumizi bora ya ardhi kupitia mkutano wa kijiji chao.

"Kwa sababu mliamua wenyewe eneo hilo liwe la malisho nitaweka miguu yangu hapo kutetea hilo na kama viongozi hao wameshiriki kuuza watakuwa wamejiharibia," amesema Maridadi.