WANANCHI KUSHIRIKIANA NA POLISI UJENZI WA KITUO CHA POLISI KATUNGURU

Wananchi wa kata na Tarafa ya katunguru wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza wamejitoa kushirikiana na Jeshi la Polisi  kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa kituo cha Polisi kilichoanzishwa kwa nguvu za wananchi.

Hayo yamejiri wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu kamishina wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa alipotembelea kukagua Maendeleo ya kituo hicho  na kuzungumuza na wananchi wa Kata hiyo.

Akizungumza wakati wa mkutano na wananchi hao, kamanda Mutafungwa amewahamasisha kumalizia ujenzi wa kituo hicho kwa wakati ili kiweze kuhudumia wananchi wa eneo hilo na maeneo jirani.

Aidha, kamanda Mutafungwa amechangia kiasi cha Sh milioni moja na kuahidi kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kituo hicho kinakamilika na kuanza kutumika.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Katunguru Sadiki mola  amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wananchi katika ujenzi wa kituo hicho.

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Katunguru Lukas Lushoshaga amesema ili Polisi wafanye kazi kwa uadilifu wanatakiwa kuwa na mazingira Bora ya kufanyia kazi hivyo kituo hiki kitakapo kamilika kitakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Kata ya Katunguru na Kata za jirani.

Previous Post Next Post