NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
AJALI iliyotokea mchana wa Juni 05, 2024 huko jijini Mbeya na kusababisha vifo vya watu 13, Jeshi la polisi Mkoa wa Mbeya limesema chanzo cha ajali hiyo ni baada ya Dereva kushindwa kulimudu gari alilokuwa aliendesha hususani mteremkoni hatua iliyosababisha kugonga vyombo vingine kadhaa vya moto na kusababisha kukatisha ndoto za nguvu kazi hiyo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya kamishna msaidizi wa Polisi SACP Benjamin Kuzaga, ajali hiyo imetokea Juni 05, 2024 mwendo wa saa 7 mchana huko katika eneo la Mbembela, Kata ya Iyunga Jijini Mbeya katika barabara kuu ya Mbeya Tunduma, baada ya Gari lenye namba za usajili T.979 CVV likiwa na tela lenye namba T.758 BEU Scania likiendeshwa na Dereva aliyefahamika kwa jina la Ross Mwaikambo [40] likitokea Shamwengo likiwa limepakia kokoto, liligongana na Gari lingine lenye namba za usajili T.167 DLF Toyota Coaster lililokuwa likiendeshwa na dereva asiyefahamika kisha kugongana na Gari lenye namba T.120 DER Toyota Harrier lililokuwa likiendeshwa na Dokta.Robert Francis Mtungi [48] Mkazi wa Isyesye.
Kamanda Kuzaga, amesema Lori hilo liliendelea kugonga Guta namba MC 660 BCR iliyokuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika kisha kugonga Pikipiki namba MC 889 CKX iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ambaye pia hajafahamika na kusababisha vifo vya watu kumi na tatu (13) kati yao wanawake 5, wanaume 8 na majeruhi kumi na nane [18] kati yao wanawake 4 na wanaume 14 na uharibifu wa vyombo vya moto.
Polisi inasema majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu na miIli ya marehemu imehifadhiwa Hospitalini hapo kwa ajili ya kusubiri kutambuliwa na ndugu zao.
Kuhusu chanzo cha ajali Kamanda Kuzaga amesema ni uzembe wa Dereva wa Gari namba T.979 CVV/T.758 BEU kushindwa kulimudu gari kwenye mteremko.
Amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Dereva wa Gari hilo ambaye anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya akiwa chini ya ulinzi.
CHANZO - MATUKIO DAIMA MEDIA