Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, amewataka wanautume wa chama cha watangaza neno la Mungu kumtangaza Kristo kwa maneno na matendo yao, wakiongozwa na neno la Mungu.
Askofu Sangu amezungumza hayo leo wakati akiongoza Misa ya Jumapili ambayo ilikwenda pamoja na kuwasimika wanautume wa chama cha watanganza neno la Mungu 20 wa Parokia ya Ndembezi mjini Shinyanga.
Amewataka kuwa mfano kwa wengine katika kumtangaza Kristo, huku akiwakumbusha wakristo wote wajibu walionao wa kuhakikisha wanasoma Biblia na kuwalea watoto wao katika maadili ya Kikristo, ikiwemo kuwafundisha neno la Mungu.
Askofu Sangu amewaasa wakristo kutokuwa wabinafsi na badala yake wanapaswa kuwajali watu wengine na hasa wenye shida.
Wakati huohuo, Askofu Sangu amewasisitiza waamini wa Parokia ya Ndembezi kuendelea kujitoa kupitia kidogo wanachokipata, ili waweze kukamilisha mambo muhimu yaliyosalia katika ujenzi wa Kanisa lao.
Wanautume wa chama wa watangaza neno la Mungu waliosimikwa katika Parokia ya Ndembezi ni pamoja na Emmanuel Zengo, Suzana Festus, Christina Mwinuka, Joseph Mayala, James Masaba, Phebelina Makaranga, Victoria Lucas Jackrine Charles, Edina Makunga na Augustino Kisuda.
Wengine ni William Masalla, Grace Kabyemela, Maria Martine, Maria Paulo, Frola Mashaka, Josephine Charles, Eva Peter, Veronica Leonard, Felister Laurent, Edina Mbasu na Leticia Charles.