ASKOFU WOLFGANG PISA RAIS MPYA TEC


Mhashamu Wolfgang Pisa

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania-TEC limetangaza safu mpya ya uongozi baada ya kufanya uchaguzi, Rais mpya wa baraza hilo akiwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi Mhashamu Wolfgang Pisa, OFMCap.

Rais wa TEC aliyemaliza muda wake Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga ametangaza safu hiyo katika Misa Takatifu ya shukrani kwa Mungu kwa kupata uongozi mpya iliyoadhimishwa katika Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili, Makao Makuu ya TEC, Kurasini Dar Es Salaam.

Askofu Mkuu Nyaisonga amesema Makamu Mpya wa Rais wa TEC ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda Mhashamu Eusebius Nzigilwa.

Baraza hilo limeridhia Katibu Mkuu Padri Dkt. Charles Kitima na Naibu Katibu Mkuu Padri Chesco Msaga kuendelea na nyadhifa zao ambao wameapishwa katika adhimisho hiyo misa na Mwanasheria wa TEC Padri Daniel Dulle.

Askofu Nyaisonga amewataja maaskofu wanaounda Kamati Tendaji yenye wenyeviti wa kurugenzi kuwa ni Askofu Mkuu Isaack Amani (Uchungaji), Askofu Eusebius Nzigilwa(Mawasiliano), Askofu Anthony Lagwen(Fedha), Askofu Agostino Shao ALCP/OSS(Ukaguzi) na Askofu Henry Mchamungu(Sheria).

Rais mpya wa TEC Askofu Pisa amemshukuru Mungu na Maaskofu kwa kumpa jukumu hilo akisema yeye na wenzake wapo tayari kutekeleza.

Ameahidi kuendeleza pale walipoishia Askofu Mkuu Nyaisonga na Makamu wake Askofu Flavian Kassala na kuomba ushirikiano na mwongozo wao.

Previous Post Next Post