Ticker

6/recent/ticker-posts

BAJETI YA 2024/25 KUJENGA UCHUMI SHINDANI NA VIWANDA KWA MAENDELEO YA WATU – DKT. MWIGULU






Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25 imelenga kutekeleza vipaumbele vilivyozingatia maeneo yaliyoainishwa kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye dhima ya “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu” pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25.

Hayo yemebainishwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25 huku akiongeza kuwa maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa katika Mpango ni pamoja na kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu, na kuendeleza rasilimali watu.

“Baadhi ya maeneo mahsusi yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na kukamilisha miradi ya kielelezo na ile ya kimkakati, kuimarisha sekta za uzalishaji, kuimarisha rasilimali watu hususani katika sekta za huduma za jamii, kuongeza matumizi ya Tehama, na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji wa sekta binafsi,”, amesema.

Aidha, amesema maeneo mengine ya muhimu katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25 ni kugharamia mishahara ya watumishi wa umma, deni la serikali, uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024, maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, maandalizi ya dira ya taifa ya maendeleo 2050, na maandalizi ya michuano ya mpira wa miguu ya mataifa ya afrika (afcon) ya mwaka 2027 ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja.

Post a Comment

0 Comments