Ticker

6/recent/ticker-posts

BODA BODA WANUFAIKA NA MIKOPO YA ASILIMIA 10 YA MAPATO YA HALMASHAURI








Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI anayeshughulikia Afya Mhe. Dkt. Festo Dugange (Mb) amesema kundi kubwa la vijana ambao ni Boda Boda Ni miongoni mwa makundi ambayo yamekuwa yakinufaika na Mikopo ya asilimia 10 itokanayo na mapato ya Ndani ya Halmashauri.

Dkt.Dugange amesema hayo Bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha Maswali na Majibu wakati akijibu swali la Mheshimiwa Nicodemus Henry Maganga, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe aliyeuliza Je, kuna mkakati gani wa kuwapatia Bodaboda mikopo midogo midogo itakayowasaidia kuwainua kiuchumi?

“wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo mama na baba lishe, waendesha bodaboda na bajaji wanajulikana kama kundi maalum na shughuli zake zinaratibiwa na kusimamiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum”

Aidha Mhe. Dkt. Dugange amesema kundi la waendesha pikipiki kibiashara wanaojulikana kwa jina la bodaboda tayari lilianza kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayoratibiwa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI ambapo katika mwaka 2022/23 mamlaka za serikali za mitaa zilitoa mikopo kwa vikundi 5,217 vya wanawake, vijana na watu wenye Ulemavu. Aidha, kati ya vikundi hivyo, vikundi 589 vilikuwa ni vikundi vya bodaboda venye jumla ya wanachama 3,096 sawa na asilimia 11 ya vikundi vyote vilivyonufaika na mkopo wa shilingi bilioni 8.63.

“serikali inaendelea kuratibu na kuhakikisha wafanyabiashara ndogondogo wakiwamo bodaboda wanajisajili kupitia mfumo wa wafanyabiashara ndogo ndogo (WBN-MIS), pamoja na kuhakikisha mwongozo wa uratibu na usimamizi wa wafanyabiashara ndogondogo (machinga) na huduma zisizo rasmi unasambazwa kwenye mamlaka za serikali za mitaa kote nchini ifikapo Julai, 2024.”

Amesema vijana Boda boda wanapaswa kujinga katika vikundi ili waweze kupata Mikopo hiyo kwani serikali imedhamiria kuwakopesha Boda Boda ili wawe na uwezo wa kununua piki piki na kufanya biashara wao wenyewe.

Post a Comment

0 Comments