Ticker

6/recent/ticker-posts

CCM IGUNGA YAAPA KUSHINDA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA KWA KISHINDO


Katibu wa CCM wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Ebenezer Ole Mainoya (kulia) akifafanua jambo kuhusu ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.Aliyemshikia kipaza sauti ni Mbunge wa jimbo hilo; Nicholaus Ngassa.

Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Igunga mkoani Tabora, kimesema kuwa kipo tayari, imara na timamu kabisa kushiriki na kushinda kwa kishindo uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.

Akizungumza mbele ya Wenyeviti wa CCM wa kata, Wenyeviti na makatibu wa CCM wa Jumuiya zote za chama, katibu wa CCM wilaya hiyo, Ebenezer Ole Mainoya, alisema kuwa chama hicho kipo tayari kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaaa, huku kikiwa kimejipanga kushinda vijiji na vitongoji vyote wilayani Igunga.

"hatuna hofu, tupo tayari kushiriki na kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa tukiwa na imani kuwa tutashinda kwa kishindo." Alisema Ebenezer.

Aliongeza kusema kuwa CCM wilayani Igunga imetekeleza ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 kwa asilimia kubwa hivyo wanayo ya kuwaeleza wananchi.

Aliwataka viongozi wa ngazi zote za chama kuendelea kuisimamia serikali katika maeneo yao.

Aidha aliwataka viongozi hao wa CCM kuunda na kushirikiana kikamilifu na kamati za ushindi kwenye maeneo yao ili mipango na mikakati ya ushindi itimie kama ilivyopangwa.

Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Igunga, Mafunda Temanywa, alisema kuwa chama hicho kinaingia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kifua mbele kwa kuwa kina viongozi wachapa kazi ambao wamefanya jitihada kubwa kutimiza ilani ya chama ya uchaguzi.

"Mbunge wetu, Nicholaus Ngassa, amepambana na angali anapambana sana kuhakikisha miradi ya maendeleo inaendelea kumiminika kwenye jimbo lake." Anasema.

Mafunda anaongeza kuwa chama hicho kina uhakika wa kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwa kero nyingi za wananchi zimetatuliwa ikiwemo kero za maji, miundombinu ya barabara, elimu, afya, maji na umeme.

Naye Mbunge wa jimbo la Igunga, Nicholaus Ngassa amesema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imekiheshimisha CCM wilayani hapo kwa kuwa imepeleka mabilioni ya shilingi, yaliyoimarisha sekta muhimu kwa maendeleo ya wananchi.

"Zimejengwa zahanati za kutosha, vituo vya afya vya kisasa na hospitali ya wilaya imepanuliwa na kunobereshwa huduma zake. "Anasema.

Anaongeza kuwa vijiji vyote kwenye jimbo hilo vina umeme huku huduma za maji safi na salama ya kunywa zinapatikana kwa asilimia kubwa.

"Miradi ya elimu, barabara ni miongoni mwa miradi iliyotia fora jimboni hapa, hivyo tunapo angazia chaguzi zijazo, ule wa serikali za mitaa na uchaguzo mkuu mwakani, tunaona kabisa hakuna mpinzania atakayeweza kuzuia ushindi wa CCM jimboni Igunga." Anasema Ngassa.

Post a Comment

0 Comments