Ticker

6/recent/ticker-posts

DC MTATIRO AWATAKA WANANCHI KUWA MAKINI NA DINI ZINAZOIBUKIA KUEPUKA MADHARA

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro, amewataka wananchi kuwa makini na madhehebu ya dini yanayoibuka na kutoa mafundisho yanayowapotosha watu, hali ambayo inasababisha madhara katika jamii.
Amewatadharisha wananchi kuwa makini na watu hao ambao wanaanzisha Makanisa na kwenda kinyume na Sheria za nchi, ikiwemo kuwakataza waamini wao kupata huduma mbalimbali muhimu ikiwemo za kiafya, jambo ambalo lina madhara makubwa kwa jamii.
Mtatiro ametumia nafasi hiyo kueleza hatua iliyochukuliwa siku mbili zilizopita na Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Shinyanga ya kulifunga Kanisa la Church of God lililopo kijiji cha Mendo Kata ya Ilola Halmashauri ya Wilya ya Shinyanga, kutokana na Kanisa hilo kwenda kinyume na sheria za nchi ikiwemo mchungaji wa Kanisa hilo kuwakataza waamini kwenda Hospitali kupata huduma za afya, hali iliyosababisha muumini mmoja wa Kanisa hilo kujifungulia Kanisani na mtoto wake kufariki dunia wakati akijifungua kutokana na kukosa huduma za kitaalam.
Amesema Mchungaji wa Kanisa hilo alikuwa ameligeuza Kanisa lake kama Hospitali na kutoa huduma mbalimbali ikiwemo za ukunga (huduma za wajawazito kujifungua) ambapo waamini wa Kanisa hilo walikuwa wakienda kujifungulia Kanisani badala ya Hospitali, kinyume cha sheria na Katiba ya nchi.
Mtatiro amesema serikali itaendelea kuwachukulia hatua wale wote wanaoanzisha madhehebu ya dini na kwenda kinyume na sheria za nchi pamoja na kufundisha mafundisho potofu yanayokwenda tofauti na maadili pamoja na taratibu za kiimani ambazo zinakubalika.
Aidha, amekemea tabia za baadhi ya wanganga wa kienyeji ambao bado wanaendelea kupiga ramli chonganishi, ambazo zinaifarakanisha Jamii na kuwataka kuacha mara moja jambo hilo.
Awali, kupitia Mahubiri yake, Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, aliwasisitiza waamini wakatoliki kuacha kukimbilia mafundisho ya uongo, ambayo badala ya kufundisha watu neno la Mungu yamejikita katika kufanya miujiza na kuleta mafanikio ya kimwili pekee.

 

Post a Comment

0 Comments