Na Respice Swetu,
Kasulu
Mkuu wa mkoa
wa Kigoma Thobias Andengenye, ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Kasulu kwa
kupata hati safi katika ukaguzi wa fedha na hesabu za serikali uliofanyika kwa
kipindi cha miaka minne mfululizo.
Pongezi hizo
amezitoa wakati wa kikao maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri ya
wilaya ya Kasulu kilichokutana kujadili taarifa hiyo.
Akisoma
taarifa hiyo kwenye kikao cha baraza la madiwani, mweka hazina wa halmashauri
ya wilaya ya Kasulu Sarah Kibona amesema kwa kipindi cha miaka minne,
halmashauri ya wilaya ya Kasulu imepata hati safi.
Taarifa hiyo
imebainisha kuwa, katika ukaguzi wa mdhibiti mkuu wa fedha na hesabu za
serikali uliofanyika mwaka wa fedha wa 2019/2020, 2020/2021, 2021/2022 na 2022/2023
halmashauri ya wilaya ya Kasulu ilipata hati safi.
Kufuatia
taarifa hiyo mkuu wa mkoa wa Kigoma aliyekuwa mgeni rasmi katika kikao hicho, ameipongeza
halmashauri ya wilaya ya Kasulu kwa mafanikio hayo na kuwataka watendaji na
madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu, kuyalinda mafanikio hayo.
Amesema
halmashauri ya wilaya ya Kasulu inatakiwa kuhakikisha kuwa hakuna hoja zitakazokuwa
zinajirudia wakati wa ukaguzi ujao, kufungwa kwa hoja zilizopo na kuzidisha umakini wakati
wa zoezi la kujibu hoja hizo.
Aidha mkuu
wa mkoa wa Kigoma amewataka wakuu wa idara na vitengo kulipa umuhimu suala hilo
kwa kushirikiana na kushiriki kikamilifu katika kujibu hoja hizo badala ya
kukaimisha jukumu hilo kwa watu wengine au kuwaachia waidizi wao.
Maelekezo
mengine aliyoyatoa Andengenye wakati wa kikao hicho ni kukamilisha majibu ya
hoja za nyuma na kutekeleza maagizo yaliyotolewa katika kikao cha tawala za
mikoa na serikali za mitaa LAAC.
“Ukaguzi unaofanyika ni muhimu na ni matakwa
ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukaguzi huu unafanywa na watu waungwana
sana hatupaswi kuwaona ni maadui bali tuwaone kuwa ni marafiki zetu na kushirikiana”,
amesema.
“Ni
matumaini ya serikali kuwa, kufikia mwaka wa fedha wa 2025/2026 idadi ya hoja zitapungua
na kufikia tarakimu moja kuliko vilivyo sasa”, ameongeza.
Awali akimkaribisha
mkuu wa mkoa kuzungumza na wajumbe wa kikao hicho, katibu tawala wa mkoa wa
Kigoma Hassan Lugwa, amewaahidi madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu kuwaletea
wataalamu watakaowapa mafunzo kuhusu ukaguzi wa hoja hizo.