Hii Ndio Huduma Bora Na Muhimu Unayopaswa Kuitoa Kwa Mteja Wako

 

Habari ya wakati huu mpendwa rafiki na msomaji wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu hujambo na unaendelea vizuri kuboresha maisha yako hatimaye kufikia kile kiwango unachokipenda uwe.

Endelea kufanya kile unachokipenda bila kujali kelele za watu wanasema nini kwani ukisikiliza ya watu ni kuidharau sauti yako ya ndani.

Njia bora ya kuwa abisha wakatisha tamaa ni kuwaaibisha kwa kuendelea kufanya kwa vitendo na kuwa kiziwi yaani unakuwa husikilizi kelele zao bali wewe unaendelea kudumu kwenye kile unachofanya.

Mpenzi msomaji, napenda kukualika katika makala yetu ya leo nzuri niliyokuandalia ili tuweze kujifunza kwa pamoja. Rafiki, katika makala yetu ya leo tutajifunza somo zuri la kutambua muda mzuri unaopaswa kumsaidia mtu . Karibu rafiki uungane nami katika safari hii ya kujifunza mwanzo hadi mwisho wa somo letu ili tuweze kujifunza kwa pamoja makala nzuri niliyokuandalia.
Katika maisha ya binadamu huwa tunapitia mapito mengi sana ambayo mengine huwezi kuelezea.

Watu wamegeuka kuwa wakatili kama vile wanyama wa porini na utu unazidi kutoweka kulingana na matukio ya ajabu yanayotokea katika jamii yetu. Hakuna sheria ya dini au serikali inayoruhusu mtu kumuua au kukatisha uhai wa wenzake kwa makusudi kabisa pasipo mapenzi ya Mungu. Uhai ni zawadi na ni mali ya Mungu hivyo basi hatupaswi kufanyiana unyama katika jamii yetu.

Katika karni hii ya 21 bado watu wanaendelea na vitendo vya ubakaji ,ushirikina na kuamini mambo ya giza katika jamii yetu ya leo wakati jamii ya Ulaya hakuna kitu kama hicho. Watu wanawaza watavumbua vitu gani ili kufanya dunia kuwa sehemu bora ya kuishi lakini jamii yetu bado inawaza mambo ya uchawi, laana na vitendo vya ajabu ambavyo haina nafasi katika karni hii.

Je msaada gani mzuri unaopaswa kumsaidia mtu? Rafiki, msaada mzuri unaopaswa kumsaidia mtu pindi amepatwa na matatizo ni kumsaidia kwa wakati. Kwa mfano, unakuta ndugu anaumwa na ana hali mbaya kweli hivyo anahitaji kupatiwa matibabu mazuri katika hospitali nzuri za uhakika ili aweze kuokoa uhai wake .

Sasa ndugu huyo anakuomba msaada aidha ni msaada wa mali au hali hapo ndio wakati au muda mzuri wa kumsaidia mgonjwa. Sasa unakuta ndugu ni mgonjwa kweli na anaomba msaada lakini hakuna mtu anayejigusa kumsaidia kwa hali wala mali. Mtu anateseka na matatizo lakini wako watu wa kumsaidia lakini kila mtu anajali yake hakuna mtu wa kumsaidia wakati mgonjwa anahitaji msaada na uwezo wa kumsaidia anao. Wengine wanasema ni bora tu afe anatumalizia fedha zetu.

Rafiki, mgonjwa atateseka ili hali wako watu wanaoweza kumsaidia ili aokoe uhai wake. Sasa wakisikia mgonjwa amefariki ndio wataanza kutoa msaada, utasikia kuhusu suala la jeneza niachie mimi nitalishughulikia, kuhusu suala la chakula na vinywaji niachie mimi nitalishughulikia. Sasa je kipindi mtu anaumwa yuko hai umeshindwa kushiriki naye hata kumsaidia kumnunulia panado ili uweze kuokoa uhai wake unakuja kujitoa wakati mgonjwa ameshafariki? Ndio maana nasisitiza sana msaada mzuri ni ule unaotolewa kwa wakati.

Msaada wako unakua hauna maana kama umeshindwa kumsaidia mtu kwa wakati kama tulivyoona hapo juu kuwa unamsubiri mtu mpaka apoteze uhai wake ndio uanze na wewe kujitoa katika msiba wakati sehemu muhimu uliyopaswa kujitoa ni pale kwa kutetea uhai wake. Unakuta watu wanalia kabisa kwa unafiki eti tutakumbuka daima wakati alipokuwa mgonjwa ulikuwa hujitoi kwa moyo ili kuokoa uhai wake.

Kwa hiyo, ndugu msomaji, katika jamii yetu kuna matatizo ya aina nyingi ambayo yanahitaji msaada wa wakati ili uweze kutatua tatizo na siyo mpaka pale unapojisikia ndio utoe msaada. Imekuwa ni tabia watu kujitoa katika mambo ya starehe lakini siyo kujitoa katika mambo ya kusaidiana wakati wa shida. Wakati mtu ana matatizo ndio wakati sahihi kabisa wa kumsaidia siyo unakuja kutoa msaada wakati msaada hauhitajiki tena. Maisha ya kutosaidiana katika changamoto mbalimbali siyo maisha tunayopaswa kuishi hapa duniani.

Mwandishi shaban Robert katika moja ya mashairi yake aliwahi kusema kujitegemea siyo kujitosheleza ni kweli licha ya kujitegemea lakini huwezi kujitosheleza bado unahitaji msaada wa watu wengine ili kufanikisha kupata kile unachokitaka. Hata kama unajitegemea lakini kumbuka kujitegemea kwako siyo kujitosheleza bila kuwa na mahusiano mazuri na watu. Maisha ni mahusiano hivyo tunatakiwa kuishi kwa kusaidiana kwa kujenga uhusiano bora.

Hatua ya kuchukua, kama ulikuwa humsaidii mtu kwa wakati basi msaidie kwa wakati na jitoe kwa moyo pale mtu anapohitaji msaada wako kwa wakati. Kama wewe ni daktari mgonjwa pale anapokuwa anahitaji huduma ya haraka na wakati basi msaidie kwa wakati kwani watu wengi wanapoteza ndugu zao kutokana na uzembe wa kutomsaidia mtu kwa wakati sahihi vifo kama hivi huwa vinaumiza sana watu wanapenda kutoa huduma kwa kujisikia bila kuangalia utu na wakati wa kuokoa uhai. Sehemu yoyote uliyopo tafadhali toa huduma kwa wakati sahihi na kwa falsafa ya ufagio ambayo ni unyenyekevu.

Hivyo basi, somo letu la leo lilitualika sisi sote kusaidiana kwa wakati pale mtu anapohitaji msaada wako au huduma yako. Huduma nzuri ni ile huduma inayotolewa kwa wakati pale mtu anashinda. Tukumbuke ya kwamba kujitegemea siyo kujitosheleza na maisha ni upendo tutumie falsafa ya upendo katika kuifanya dunia kuwa sehemu ya kuishi kwa kila mmoja wetu.
Previous Post Next Post