Jeshi la Polisi Mkoa wa
Shinyanga limewakamata watuhumiwa watatu wanaohusishwa na mauji ya watu wawili
waliouawa na kisha kuchomwa moto kwa tuhuma za wizi katika kata za Kitangili na
Kizumbi Manispaa ya Shinyanga.
Taarifa hiyo imetolewa
na kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa
Polisi (SACP) Janeth Magomi wakati akizungumza na Misalaba Media, ambapo amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni
mafanikio yanayotokana na msako na doria mbalimbali zinazofanywa na askari wa
jeshi hilo.
Amesema jeshi hilo
halitawafumbia macho wale wote wanaobainika kujichukulia sheria mkononi dhidi
ya watuhumiwa wa matukio ya uhalifu kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria
za nchi.
Kamanda Magomi
amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi kutoa taarifa za
matukio ya wahalifu na uhalifu badala ya kujichukulia sheria mkononi.
“Hatutakubali
matendo haya ya kikatili yaendelee ndani ya Mkoa wa Shinyanga kwahiyo jeshi la
Polisi tumeingia katika oparesheni kali kabisa kuhakikisha kwamba tunawasaka wale
wote ambao wamehusika katika matendo haya na kwa kuanzia sasahivi tunawatuhumiwa
watatu mparoni kuhusiana na lile tukio la mwanzo ambalo lilitokea katika kijiji
cha Iwelyangula na Bugayambelele kata za Kitangili na Kizumbi na hawa
watuhumiwa ni wakazi wa Mkoa wa Shinyanga sisi tutawapeleleza mpaka pale ambalo
tutahakikisha jarada lao tunalifikisha kwa wanasheria halafu tuweze kupisha
makahama”.amesema SACP Magomi
“Sisi jeshi la Polisi
bado tunaendelea kutoa elimu kwamba wananchi anayefanya kosa adhabu yake si kupigwa
na kuuawa kisha kuchomwa moto na ndiyo maana tunaendelea kuwaelimisha kwamba vipo
vyombo vya sheria mahakama zipo kwahiyo wananchi waendelee kushirikiana na
jeshi la Polisi na sisi tunaendelea kutoa elimu katika kata zetu kuna wakaguzi
wa kata kuna maaskari ambao wanashirikiana na viongozi wa vijiji, tarafa, mtaa,
vitongoji na kata”. amesema SACP Magomi
Hata hivyo baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga
wameiomba serikali kuendelea kuchukulia hatua za kisheria dhidi ya watu
wanaokutwa na tuhuma za uhalifu, badala ya kuwaachia huru hali inayochochea
hasira kwa wananchi.
Wamesema kitendo cha wananchi kujichukulia sheria
mkononi kimekuwa kikichochewa na hasira baada ya kuona watuhumiwa wa vitendo
vya uhalifu ikiwemo wizi, unyang’anyi na ujambazi wakiwa mtaani baada ya
kuachiwa huru.
Wameliomba jeshi la Polisi na mamlaka nyingine za
kisheria kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria zilizopo ili iwefundisho kwa
watuhumiwa na watu wengine wenye tabia kama hizo na kukomesha uhalifu.
Wananchi hao wametaja sababu mbalimbali
zinazochangia uhalifu kwa vijana kwamba ni hulka binafsi, hali ngumu ya maisha
inayosababishwa na ukosefu wa ajira lakini pia kujihusisha kwenye makundi
mabaya.
Misalaba
Media pia imezungumza na kamanda wa jeshi la Polisi mkoa
wa Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi Janeth Magomi ambaye ameendelea
kuonya tabia ya wananchi kujichukulia sheria mkononi ambapo amesema kwa kufanya
hivyo ni ukiukwaji wa sheria za nchi.
Post a Comment