Na Mapuli Kitina Misalaba
Kamishna wa Umeme Wizara ya Nishati Mhandisi
Innocent Luoga ameridhishwa na hatua mbalimbali za maendeleo katika upatikanaji
wa huduma ya Umeme Mkoa wa Shinyanga huku akipongeza kwa kuongeza makusanyo ya
mapato kutoka bilioni 8 hadi kufikia bilioni 11 katika Mwaka huu wa fedha
2023\2024.
Mhandisi Luoga ameyasema hayo leo baada ya kufanya
ziara yake ya siku moja Mkoani Shinyanga ambapo ametembelea mradi wa Umeme wa
Jua katika Wilaya ya Kishapu pamoja na
kituo cha kupoza na kusambaza Umeme Ibadakuli.
Akisoma taarifa ya miradi ya kusambaza Umeme kwa
Mwaka wa fedha 2023\2024 meneja wa shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga
Mhandisi Leo Mwakatobe amesema mradi wa Umeme wa Jua unaotekelezwa katika
maeneo ya Ngunga Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga umefikia asilimia kumi (10)
ambapo unatarajiwa kukamilika Mwezi Februari 2025.
Mhandisi Mwakatobe ameeleza zaidi kuwa hali ya
usambazaji Umeme katika Mkoa wa Shinyanga imeendelea kuimarika ambapo jumla ya
vijiji 412 kati ya vijiji 509 tayari vimefikiwa na Umeme huku akisema ipo
mikakati ya kuhakikisha vijiji 97 vilivyobaki vinafikia na miundombinu ya Umeme
mwishoni mwa Mwaka huu 2024.
“Hali
ya usambazaji Umeme imeendelea kuimarika kutokana na miradi mbalimbali ya
kusambaza Umeme inayotekelezwa na TANESCO na ile ya kusambaza Umeme vijijini
inayofadhiliwa na serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA)”.
“Jumla
ya vijiji 412 kati ya 509 vimefikiwa na Umeme na matarajio yetu ifikapo
mwishoni mwa Mwaka 2024 vijiji vyote 97 vilivyobaki Mkoani Shinyanga vitakuwa
vimefikiwa na miundombinu ya Umeme”.
“Katika
Manispaa ya Kahama vijiji 37 kata ya 45 vimefikiwa na Umeme, Halmashauri ya
Msalala vijiji 45 kati ya 92 vimefikiwa na Umeme, Halmashauri ya Ushetu vijiji
84 kati ya 112 vimefikiwa na Umeme, Manispaa ya Shinyanga vijiji 11 kati ya 17
vimefikiwa na Umeme, Shinyanga vijijini vijiji 121 kati ya 126 vimefikiwa na
Umeme na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu vijiji 114 kati ya 117 tayari
vimefikiwa na Umeme”.amesema Mhandisi Mwakatobe
Pia meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga pamoja na
mambo mengine amesema shirika hilo linasimamia miradi miwili (2) ya kimkakati
ambayo ni mradi wa Umeme wa Jua Wilaya ya Kishapu pamoja na mradi wa kuboresha
upatikanaji Umeme Bulyanhulu ikiwa lengo ni kuongeza uzalisha Umeme na
kuboresha upatikanaji Umeme.
“Mradi
wa Umeme wa Jua, kutokana na mahitaji ya Umeme kuongezeka serikali imetoa fedha
kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Umeme Jua maeneo ya Ngunga Kishapu ili kuongeza
kiwango cha upatikanaji Umeme Mkoa wa Shinyanga na maeneo mengine ya Nchi,
mradi huu unatarajiwa kuzalisha Umeme wa kiasi cha Megawati 150 ambapo mradi
unathamani ya shilingi 323, 059,197, 768.30 na umegawanyika katika awamu mbili
ya kwanza ni MW 50 na mkandarasi ni SINOHYDRO ambapo mkandarasi ameshakabidhiwa
kazi na kuanza ujenzi Mwezi Oktoba 2023, kwa sasa mradi upo asilimia 10 na
matarajio ya kukamilika ni baada ya Miezi kumi na nne (14).
“Mradi
wa kuboresha upatikanaji Umeme uliopo eneo la Bulyanhulu, serikali kupitia
shirika la Umeme kwa Mkoa wa Shinyanga kwa kuongeza mashineumba au Transfoma
yenye ukumbwa wa 90\120MVA kwenye kituo cha kupoza Umeme wa grid cha Bulyanhulu
220\33kV mradi huu una thamani ya dola
za kimarekani 5,318,800.00 (bilioni 12) na mradi unatarajia kukamilika Septemba
2024”.amesema Mhandisi Mwakatobe
Aidha Mhandisi Mwakatobe ametaja mafanikio
mbalimbali yaliyofikia na shirika la Umeme TANESCO Mkoa wa Shinyanga katika
Mwaka wa fedha 2023\2024 ikiwemo ongezeko la ukusanyaji mapato kutoka bilioni
nane (8) hadi kufikia bilioni kumi na moja (11).
“Katika
utekelezaji wa miradi ya kusambaza Umeme kwa Mwaka wa fedha 2023\2024
tumefanikiwa kuunganisha wateja mpaka kufikia wateja 95,206 lakini pia
tumefanikiwa kuongeza mtandao wa usambazaji Umeme hadi kufikia kilomita
2,331.05 kwa msongo wa kati na kilomita 2,328.72 kwa msongo mdogo, tumefanikiwa
kufikisha Umeme kwenye jumla ya vijiji 412 kati ya vijiji 509 lakini pia
tumefanikiwa kuongeza makusanyo ya mapato hadi kufikia bilioni 11”.amesema
Mwakatobe
Akizungumza kamishna wa Umeme Wizara ya Nishati Mhandisi
Innocent Luoga amempongeza meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga na menejimenti
yake kwa usimamizi mzuri wa miradi ya Umeme huku akiwasisitiza wakandarasi
kukamilisha kwa wakati miradi inayoendelea ili kufikia malengo yaliyokusudiwa
na serikali
“Kwanza
nikupongeza meneja pamoja na menejimenti yako yote kwa usimamizi mzuri kwa
sababu hali ya Umeme sasa hivi Mkoa umetulia makusanyo yameongezeka kwa sababu
kipimo cha utendaji wa menejimenti moja wako ni ongezeko la mapato kwahiyo
nawapongeza sana kwa kuongeza mapato kingine nawapongeza kwa kuongeza wateja hapo
hapo niwasisitiza tujitahidi sana kuongeza kasi ya kuunganisha wateja wapya ili
kuongeza mapato”.
“Pia
tuwe na mikakati maalum ya kuhakikisha tunazuia au tunapunguza upotevu wa Umeme
sasahivi tunasisitiza sana matumizi bora ya nishati safi lakini pia tuendelee
kudai madeni ya taasisi zinazodaiwa na tuweke mikakati ya kukusanya madeni hayo
tutumie njia ambazo zinawezekana ikiwemo kukaa vikao nao ili kuweka maazimio ya
pamoja pamoja na kwa wale wateja wadogo wadogo”.
“Lakini
pia kuongeza usimamizi kwa wakandarasi maana mkandasi ukimsimamia hawezi kuacha
kufanya kazi mara nyingi sana wakandarasi wanazembea au wanakimbia ni kwa
sababu tu haupo usimamizi mzuri kwahiyo mi nashauri tuhakikishe tunaongeza
usimamizi kwa hao wakandarasi wetu ikiwa ni pamoja na kufanya nao vikao vya
mara kwa mara ili kujua changamoto na maendeleo ya miradi”
“Yapo
masuala ya usimamizi kwenye miundombinu na uharibufu unaofanyika ni wamaksudi
au wengine kutokujua tu kwahiyo tuendelee kutoa elimu hasa kwa wananchi kuwaelezea
madhara ya kuharibu miundombi ya Umeme wakati mwingine mnapanga ratiba kwenda
kutoa elimu kwenye maeneo ambayo ni korofi zaidi”.
“Mradi
wa Umeme wa Juan i muhimu sana mradi huu wa Kishapu ukija kukamilika maana yake
wakati wa mchana tutakuwa tunatumia mradi wa Kishapu halafu wakati wa usiku
hakuna Jua hakuna upepo tunawasha mitambo ya Maji na hii unakuwa mradi wa
kwanza Tanzania wa kusalisha Umeme kwa kutumia Jua kwahiyo niwatake tu
wakandarasi wa mradi huu wahakikishe wanamaliza mradi kwa wakati, kuchelewa
chelewa kusiwepo na mradi huu ukamilike kwa kiwango kinachotakiwa”.amesema
Mhandisi Luoga
TANESCO Mkoa wa Shinyanga inahudumia jumla ya Wilaya
tatu ambazo ni Kahama, Kishapu na Shinyanga ambapo mpaka kufikia mwishoni mwa
Mwezi Mei 2024 Mkoa unajumla ya watumiaji umeme 95, 206 na kwamba matumizi ya juu
ya umeme yaliyofikiwa kwa Mwaka wa fedha 2023\2024 ni megawati 78.1.
Meneja wa shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Leo Mwakatobe upande wa kulia akiwasilisha taarifa ya miradi ya kusambaza Umeme kwa Mwaka wa fedha 2023\2024 na mipango ya huduma ya Umeme kwa Mwaka wa fedha 2024\2025 Mkoa wa Shinyanga.
Meneja wa shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Leo Mwakatobe akiwasilisha taarifa ya miradi ya kusambaza Umeme kwa Mwaka wa fedha 2023\2024 na mipango ya huduma ya Umeme kwa Mwaka wa fedha 2024\2025 Mkoa wa Shinyanga.
Kamishna wa Umeme Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga akimpongeza meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga kwa usimamizi mzuri hali iliyosababisha kuongezeka kwa makusanyo ya mapato katika Mwaka wa fedha huu 2023\2024.
Kamishna wa Umeme Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga akipokea maelezo kuhusu hatua mbalimbali katika kituo cha kupoza na kusambaza Umeme Ibadakuli.
Kamishna wa Umeme Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga akipokea maelezo kuhusu hatua mbalimbali katika kituo cha kupoza na kusambaza Umeme Ibadakuli.