MAJALIWA: MIUNDOMBINU YA MICHEZO KUENDELEA KUBORESHWA







Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza kwenye ufunguzi wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISSETA) katika uwanja wa Alli Hassan Mwinyi mkoani Tabora Juni 8.2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

……………..

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kuboresha miundombinu ya michezo katika shule teule 56 nchini.

Amesema hadi kufikia Machi 2024 imeshapeleka shilingi billioni nne kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika shule za sekondari 26 za amali.

Ameyasema hayo  alipofungua Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi na Sekondari Tanzania, Tabora. Amefungua mashindano hayo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha na kuhamasisha ufundishaji wa michezo katika shule za Msingi na Sekondari nchini.

Waziri Mkuu amesema shule 10 zilizopelekewa fedha za maboresho ni za michezo na sanaa na ni miongoni mwa shule teule 56 za michezo.

Amesema lengo la Serikali ni kuendelea kuboresha na kuweka mazingira mazuri ya michezo na sanaa nchini kwa ajili ya kuandaa wataalam na wanamichezo mahiri.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inaamini kwenye uwekezaji katika michezo ya wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari kwani unasaidia kwenye maandalizi ya mchezaji kuwa mahiri na kufanya vizuri ndani na nje ya nchi.

“Hii ndio sababu ya uwepo wa mashindano haya ya michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA ambayo yanasaidia kuibua vipaji mbalimbali vya wanamichezo watakaoweza kucheza michezo mbalimbali kwa ngazi za kitaifa na kimataifa”

“Michezo ina manufaa makubwa katika maisha yetu. Kwanza kabisa, michezo husaidia afya ya mwili na akili, amani ya nafsi, kupata pesa na uongeza umaarufu.”

“Kwa upande wa wazazi na walezi, hakikisheni na himizeni ushiriki wa watoto katika michezo au sanaa ili wasijitenge na fursa zinazopatikana katika dunia ya sasa.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI amesema kwa mwaka huu mashindano ya UMITASHUMTA yamehusisha wanamichezo 3188, na walimu na viongozi 805 kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Ameongeza kuwa Mashindano ya UMISSETA yatahusisha wanamichezo 3360, na walimu na viongozi 900.

Naye, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt Damas Ndumbaro amesema katika kutekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu la kuitaka wizara hiyo imepeleka wataalam kwenye mashindano hayo, ikihakikisha baada ya mashindano hayo kutakuwa na timu za taifa zinazotokana na michuano hiyo.

“Pia ulituelekeza tuwe na shule maalum ambazo timu hizo zitawekwa, hivyo kwenye bajeti tuliyoipitisha hivi karibuni tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule 10 maalum za michezo.”
Previous Post Next Post