Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKALA: VYAMA MASIKA KIANGAZI HAVIPO

 



Adeladius Makwega-MWANZA

Mwaka 1996 Mwanakwetu alifika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam kumsindikiza baba yake Mwalimu Francis Makwega ambaye alikuwa anasafiri kuelekea Dublin-Ireland. Kwa upande wa familia yao alikuwepo Mwalimu Doroth Mlemeta (mama wa Mwanakwetu), Modestus Makwega(mdogo wake Mwanakwetu) na Canon Kedimon Mlemeta(Mjomba wa Mwanakwetu).

Hili linalosimuliwa ni tukio la miaka karibu 28 iliyopita, wakiwa pale uwanjani majira ya jioni, kabla ya abiria kuingia ndani kukaguliwa, akafika marehemu Bob Makani ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa CHADEMA ile ya awali, ambapo alikuwa amevalia suti nadhifu ya rangi bluu na shati jeupe, tai na chini viatu vyeusi.

Bob Makani naye siku hii alikuwa anasafiri kwenda ng’ambo alikuwa ameambatana na vijana wa kiume wadogo wanamsindikiza huyu mzee, huku wakiwa wamebeba masanduku yake.Vijana wa Bob Makani wakamuacha baba yao kando wakaja tulipo sisi kutusalimia hilo lilimshangaza Mwanakwetu kijana,

“Shikamoo Mr Makwega!”

Mwalimu Francis akaitikia ,

“Marahaba.”

Bob Makani nayeye akaja hapo tulipo akatusalimu, alafu akauliza,

“Mwalimu Makwega unakwenda wapi?”

Mwalimu Makwega akajibu kuwa anakwenda masomoni ughaibuni. Bob Makani akauliza sasa Mr. Makwega watoto wetu watabaki na nani? Mwalimu Makwega akajibu wapo walimu wengine wengi na wazuri na wataendelea kuwafundisha.

Bob Makani akaaga na akaingia ndani kuelekea kwenda kukaguliwa, hapo hapo wale vijana wake wakarudi na kumuaga mwalimu wao wa Shule ya Msingi Bunge na kuondoka kurudi nyumbani kwao katika gari lao binafsi.


 

Bob Makani anakaguliwa kule ndani, sisi huku nje bado tupo na Mwalimu Makwega tunaongea. Kumbe hawa ni wanafunzi wako? Eeeh wanafunzi wangu Bob Makani huwa anakuja katika vikao vya shule, Mwalimu Makwega anajibu.

“Huyu mzee wana Chama chao, kipo vizuri, chama chao ni cha wasomi, wengi wanaona Mrema angeingia chama hiki na siyo NCCR MAGEUZI,CHADEMA kimeanzishwa na watu wengi makini waliyotoka serikalini kama Edwin Mtei na wanafahamu vizuri namna mambo yanavyoendeshwa.”

Mzungumzaji mzuri alikuwa Modestus Makwega maana alikuwa na uelewa mzuri wa hawa CHADEMA na NCCR MAGEUZI kuliko watu wote siku hiyo, baadaye Mwalimu Makwega aliingia katika chumba cha ndani kukaguliwa na baadaye kupanda ndege kuondoka zao huku wasindikizaji kurudi kwao Mbagala siku hiyo.

“Siku chache kabla ya safari hiyo, Mwalimu Makwega na Mwanakwetu walipita kwa Mustapha Mkulo kuchukua tiketi ya ndege ambapo huyu Mustapha Mkulo ambaye alikuja kuwa Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yeye alikuwa anasafiri mno nje ya nchi hivyo alikuwa anapewa ofa ya tiketi kadhaa za bure za ndege kwa kuwa mteja wao mzuri na

Muda mwingine mzee Mkulo hakuwa na safari hivyo tiketi zile za ofa alikuwa anawapa wahitaji na hasa ndugu zake wenye safari za Ulaya na Marekani hususani wale wenye asili na mkoa wa Morogoro, hapa hata wazo la yeye kuwa mbunge halipo akilini mwake.

Kwa leo itoshe tu kwa Mwanakwetu kusema BURIANI MUSTAPHA MKULO.”

Katika siasa za Tanzania NCCR MAGEUZI wakaingia katika migogoro tele na baadaye Augustine Mrema akakimbilia TLP na kupoteza kiti cha ubunge wa Temeke. Hoja ya Mrema kwenda TLP ikaibua maswali huku wakisema Mrema angeenda tu CHADEMA. Mwaka 2000 hali ilikuwa mbaya hata kwa wale waliyopata Udiwani na Ubunge kupitia mgongo wa Mrema chini ya NCCR-MAGEUZI mwaka ule wa 1995 na mwaka 2000 wengi wao walipoteza nafasi zao. Japokuwa miaka kadhaa baadaye Mrema alipata tena Ubunge kupitia TLP mkoani Kilimanjaro.

Wakati chama cha Wananchi (CUF) kinaingia katika mgogoro wake baina ya Profesa Ibrahimu Lipumba na Maalim Seif Sharifu, mara wabunge mahakamani,mara lile, walio wengi walitazama kuwa kama Maalim Seif anaondoka CUF basi aenda CHADEMA, lakini hali ilikuwa sivyo Maalim Seifu Sharifu alikwenda kujiunga na chama kipya cha ACT WAZALENDO.

Watu wanajiuliza hawa akina SALIM BIMANI wajuzi wa siasa za upinzani wa Tanzania inakuwaje wanafanya hivyo ? Mbona wanapeleka nguvu kwingine? Hali hiyo ilikuwa hivyo hivyo kwa ndugu yetu Bernad Membe mwaka 2020 na yeye akaingia ACT WAZALENDO na kukikacha CHADEMA na hapo hapo Mzee Membe hakuweza kufurukuta kabisa katika Ulingo wa Siasa za Tanzania na kuonekana kiongozi dhaifu kuliko wote waliokimbilia upinzani toka CCM katika historia ya Tanzania.

Ukiyatazama yote hayo vizuri lile la Mrema mwaka 1995 kwenda NCCR MAGEUZI na Mrema wa 1997 kwenda TLP, Maalim Seifu Sharifu kwenda ACT WAZALENDO, Bernad Membe kwenda ACT WAZALENDO lakini Ndugu Edward Lowassa mwaka 2015 yeye alipita njia ya kipekee kabisa na kuingia CHADEMA ambapo hali ilikuwa tofauti na msomaji wangu unatambua kilicho tokea,umma wa Watanzania ulivyofurika CHADEMA. Japokuwa Lowassa alirejea CCM huku CCM ikiwakumbatia waliyounga juhudi na kumpinga Lowassa CHADEMA akiwamo Dkt. Wilbroad Silaa.

Swali ni je wanaokikwepa CHADEMA ni watu sahihi katika kujenga siasa za ushindani wa kweli nchini Tanzania?

Ukiwa unatafakari hilo kumbuka na haya vijana kadhaa wa CHADEMA waliounga mkono juhudi CCM walipewa vyeo kadhaa CCM, rejea pia wabunge 18 wanawake wa CHADEMA wamefurushwa CHADEMA lakini hadi kesho bado wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia rejea moyo wa Tundu Lissu kupigwa Risasi bado anasimama katika majukwaa ya kisiasa hadi leo hii, yote hayo CHADEMA bado ipo pale.

Swali lengine kwako msomaji wangu je CHADEMA ni chama madhubuti?

“Kitu madhubuti ni kile kinachokutana na misukosuko mingi na kinastahamili na kubaki salama.”

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwaka 1995 CHADEMA haikuonekana kuwa na nguvu huku akina Dkt. Masumbuko Lamwai wa NCCR MAGEUZI walichachama sana majukwaani lakini mwisho wa siku hao hao walirudi CCM chama cha Mwanakwetu na kupewa vyeo kumbe walikuwa nguvu ya soda, wakati CHADEMA ilijitahidi kuwa kimya huku wakijenga mifumo ya kitendaji ndani ya chama chao.

Zipo hoja oooh kuna chama kipya hiki na kile hizo ni hoja dhaifu ambazo Watanzania lazima wawe makini, kama mpinzani wa kweli aende CHADEMA, aungane nao hao waliyopo kwa miaka karibu 30 maana historia inaonesha namna wanavyovuka vingingi, hivyo vyama vipya ni Vyama Masika Kiangazi Havipo. Vitakuwa vyama vya msimu tu. Hilo linawahadaa wananchi na hususani wapiga kura ambalo Mwanakwetu anapinga hadaa kwa Wapiga kura. Ndiyo maana Mwanakwetu amekumbuka maneno yale pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam;

“Huyu mzee wana Chama chao, kipo vizuri, chama chao ni cha wasomi, Mrema angeingia chama hiki na siyo NCCR MAGEUZI,CHADEMA kimeanzishwa na watu wengi makini waliyotoka serikalini kama Edwin Mtei na wanafahamu vizuri namna mambo yanavyoendeshwa.”

Tukiwa na chama pinzani madhubuti wananchi wenyewe wanapima, hizi ni pumba na zile mchele,wanakuwa na chagua  lingine kama siyo CCM basi ni CHADEMA hilo litasaidia nchi kuwa na utulivu na siyo wananchi wakikwaza na chama tawala wanafanya maandamano, migomo na vurugu mara jeshi limeingilia kati kama zile za Misri wakati wa Hosni Mubarak mwaka 2012, haya mambo ya vurugu hayana tija na yanatokea kama wananchi hawana chaguo la lingine. Hili chaguo lingine linapaswa lipewe heshima zote kwa manufaa ya kulinda utaifa na kulinda amani na wananchi wafikirie shughuli za maendeleo


 

Mwanakwetu Upo ?

 

Kumbuka,

“Vyama Masika Kiangazi Havipo.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




Post a Comment

0 Comments