Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga na nje ya Manispaa, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri mkuu, kazi, vijana, Ajira na Wenye ulemavu Paschal Patrobas Katambi, kwa namna anavyofanya juhudi kuwezesha miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imeubadilisha mji wa Shinyanga.
Katambi amepongezwa wakati wananchi wakichangia maoni yao kupitia kipindi cha Shinyanga Mpya ya Katambi kinachorushwa na Redio Faraja, ambacho Mbunge huyo anakitumia kuwashirikisha wananchi wa Jimbo lake kuhusu namna anavyofanya Juhudi kuwezesha miradi mbalimbali ya maendeleo inayowagusa moja kwa moja ikiwemo Miradi mikubwa ya Kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Wananchi hao wamebainisha kuwa, kazi anayoifanya Mheshimiwa Katambi inaonekana, ambapo amegusa maeneo muhimu ambayo yalikuwa changamoto kubwa kwa siku nyingi ikiwemo Sekta ya Elimu, miundombinu ya Barabara, maji, huduma za afya na umeme pamoja na kuboresha madhari ya mji wa Shinyanga.
Hata hivyo wamemuomba Mbunge huyo kuendelea kuwasaidia ili kufikiwa na mtandao wa maji, barabara na umeme kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hizo, huku wakazi wa Kata ya Chamaguha ambao baadhi yao ni wakulima wakimuomba kuwawezesha kupata chanzo cha maji kwenye eneo la Sanjo ili kuwezesha kilimo cha umwagiliaji cha zao la Mpunga.
Katika ufafanuzi wake, Katambi amebinisha kuwa kwenye kipindi chake amewezesha kuongezeka kwa fedha za mfuko wa jimbo kutoka Shilingi Milioni 200 hadi kufikia Shilingi Bilioni 1.5, ambazo zote ikiwemo ruzuku kutoka Serikali kuu na zile za makusanyo ya ndani ya Halmashauri ambayo yameongezeka kwa kiasi kikubwa, wanazipeleka kwenye miradi ya maendeleo.
Katika upande wa Miundombinu ya barabara, Katambi ameeleza juhudi alizozifanya kuhakikisha madaraja yanajengwa kwenye maeneo ambayo yalikuwa yakisababisha adha kubwa kwa wananchi ikiwemo kukatika kwa mawasiliano na hasa katika kipindi cha mvua, ambayo ni pamoja na Daraja la Ibinzamata-Kitangili, Daraja la Dome-Mwanoni kuelekea Machinjioni, Daraja la Ndala-Mwasele, Daraja la Ndembezi-Seseko, Daraja la Old Shinyanga-Mwamalili, Daraja la Tambukareli (kwa Mchungaji Machimu) na Daraja la Uzogore-Bugwandege.
Katambi ameahidi kuendelea kutumia uwezo wake kutafuta fedha kwa kushirikiana na Serikali ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga , ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ambayo bado haijakamilika, ikiwemo kukijenga kwa kiwango cha Lami kipande cha Barabara ya kutoka Ndala/Masekelo hadi katika Hosptali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga-Mwawaza, ili kuwaondolea adha wananchi.
Miradi mingine ambayo ameahidi kuhakikisha inatekelezwa ni pamoja na Ujenzi wa Kituo kipya na cha kisasa cha Mabasi katika eneo la Kizumbi, kuendelea kuwezesha na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za Afya, kupanua mtandao wa maji ikiwemo kuchimba visima kwenye maeneo ambayo wananchi hawawezi kumudu gharama za maji ya kulipia, pamoja na kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara hasa kwenye maeneo yenye uhitaji.
Aidha ameleeza kuhusu namna anavyoshirikiana na Serikali kuhakikisha Shinyanga inakuwa na taasisi nyingi za Elimu ya Kati na Elimu ya juu ikiwemo uanzishwaji na chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo tawi la Shinyanga, pamoja na kukipandisha hadhi chuo cha Ushirika Moshi tawi la Kizumbi kuwa chuo kikuu, hatua ambayo ameitaja kuwa itasaidia kuongeza mzukunguko wa fedha katika Manispaa ya Shinyanga na kuinua kipato cha wananchi.
Kipindi cha Shinyanga mpya ya Katambi kinarushwa na Redio Faraja kila Jumatano kuanzia saa 3:00 usiku na kurudiwa Ijumaa kuanzia saa 7:00 mchana, ambacho kinakwenda sanjari na kinyang’anyiro cha Funguka ushinde na Katambi kinachowawezesha wananchi kujishindia zawadi mbalimbali ikiwemo nyongeza ya mtaji kwa makundi maalum ya Wanawake, Vijana, wazee na wenye Ulemavu kwa njia ya kujibu maswali yanayohusu utekelezaji wa Miradi ya maendeleo katika Jimbo la Shiyanga mjini ikiwemo ile inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Kipindi hicho ni mwendelezo wa mpango wa Redio Faraja wa kuwakutanisha wananchi na viongozi wao.