Imeelezwa kuwa Kliniki Tembezi ya Huduma za Kinga, Tiba na Matunzo (CTC) maarufu kama MKOBA imesaidia kwa kiasi kikubwa kuwafikia wapokea huduma wanaoishi katika maeneo ya pembezoni ambayo yapo mbali na vituo vya Afya Mkoani Kigoma.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Waandishi wa Habari Mkoani humo iliyofanyika Juni 15,2024 iliyolenga kuangalia utekelezaji wa Mradi wa Afya Hatua unaotekelezwa na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (U.S. CDC).
Kitongoji cha Tandala kilichopo katika kata ya Uvinza Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma ni miongoni mwa Vituo vya Kliniki Tembezi ya Huduma za Tiba na Matunzo kwa Wapokea Huduma kinachohudumiwa na THPS kupitia Mradi wa Afya Hatua ili kuwapunguzia adha na gharama wapokea huduma kufuata huduma hizo katika kituo cha Afya Uvinza kilichopo umbali wa takribani Kilomita 50.
Mmoja wa Wapokea Huduma katika kitongoji cha Tandala, Joshua Zengo aliyebainika kuwa na maambukizi ya VVU mwaka 2018 anasema awali walikuwa wanapata huduma za tiba na matunzo katika kituo cha Afya Uvinza ambacho kipo mbali sana na eneo hilo hali iliyokuwa inapelekea baadhi kushindwa kupata huduma hizo.
“Tunawashukuru THPS kwa kuturahisishia upatikanaji wa huduma hizi ambapo tangu 2019 wanatuletea huduma hizi katika shule ya Msingi Tandala siku za Jumamosi.
Tulikuwa tunapata usumbufu wa kusafiri umbali wa kilomita 50 kufata huduma Wilayani Uvinza ambapo nauli kwenda na kurudi ni shilingi 10,000/=. Hapo bado hujala na pia ukizingatia kwamba huku kwetu bado hakuna usafiri wa uhakika sana.
Baada ya THPS kutusogezea huduma hizi katika eneo letu hatupati usumbufu huo na kila mpokea huduma anapata huduma zote vizuri”,amesema Zengo.
Naye Joseph Kulwa Nkalango mkazi wa Kitongoji cha Tandala ambaye pia ni mpokea huduma tangu mwaka 2018 anaeleza kuwa uwepo wa Kliniki hiyo umewapunguzia gharama na muda wa kufuata huduma kwenye kituo cha Afya Uvinza na hivyo kuwa wafuasi na watumiaji wazuri wa dawa za kufubaza VVU (ARV).
“Ninatumia huduma za VVU vizuri kupitia kituo hiki. Awali tulikuwa tunahangaika kufuata huduma kituo cha Afya Uvinza wakati mwingine tunakosa huduma au kuchelewa kutokana na umbali lakini pia gharama za nauli lakini baadaye THPS ilileta huduma hapa Tandala, sasa hivi hatutumii gharama yoyote kufuata huduma”,amesema Nkalango
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tandala, Ngasa Kamishe Mhamhila amesema kabla ya kuanzishwa kwa huduma ya MKOBA wananchi walikuwa hawajitambui, wengi walikuwa wanapoteza maisha kwa sababu ya umbali wa kufuata huduma hivyo baada ya kusogezwa kwa huduma wananchi wameweza kutambua afya zao na wanapata huduma kwa ukaribu na uoga na unyanyapaa umepungua.
“Licha ya eneo hili kusogezewa huduma za Tiba na Matunzo, tunaomba tujengewe Zahanati eneo hili ili tuweze pia kupata huduma zingine za afya mfano kwa mama na mtoto, wananchi wanatumia muda mrefu kufuata huduma za afya mfano kwenda Chakuru, Mliyabibi Nguruka ni kilomita nyingi mno, kwa hiyo akina mama wengi wanajifungua majumbani, hili bado linaleta changamoto kwa sababu inashauriwa kina mama wanaoishi na VVU wanapaswa kujifungulia kwenye kituo cha afya ili kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto” ,amesema Mhamhila.
Mshauri wa Huduma za Matunzo na Tiba kutoka THPS mkoani Kigoma Dkt. Nyanzige Maziku amesema Huduma MKOBA imesaidia Wapokea huduma kufika kwa wakati kupata huduma, kupata dawa kwa wakati na sasa hawaruki siku za kupata dawa hivyo kufubaza VVU na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo kama kawaida kwani afya zao zimeimarika.
Naye Meneja Mradi wa THPS Afya Hatua Wilaya ya Uvinza Dkt. Gabriel Max amesema mradi huo katika Halmashauri hiyo unahudumia vituo vya afya 16 vinavyowezeshwa na THPS ambapo miongoni mwa huduma zinazotolewa ni huduma za tiba na matunzo, Upimaji, Uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama wanaoishi na VVU kwenda kwa mtoto na Tohara Kinga.
“Kwa Jiografia ya Uvinza asilimia kubwa ya wananchi na wapokea huduma wetu ni wakulima, wafugaji na wavuvi, shughuli za kiuchumi ambazo wakati mwingine zinawafanya wanakuwa mbali na maeneo ya kutolea huduma za afya. Kwa hiyo kwa kutambua hilo na katika kuunga mkono jitihada za Serikali, tumesogeza huduma za afya kwa wananchi wanaoishi mbali na maeneo ya kutolea huduma za afya”,amesema Dkt. Max.
“Kwa Huduma MKOBA ambazo ni huduma zinazosogezwa kwa jamii, Uvinza tuna maeneo 36 yanayotoa huduma hizi na hazina tofauti na huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya kwa sababu watoa huduma ni wale wale, vitendea kazi, vipimo na dawa ni zile zile”,ameeleza.
Amesema kwa Halmashauri ya Uvinza wanahudumia jumla ya wapokea huduma 6,000 kwenye vituo 16 lakini wapokea huduma 2,000 kati hao wanapokea huduma ya MKOBA.
“Tunashukuru kwa ushirikiano tunaopata kutoka Serikalini na katika jamii kwani maeneo mengi tunayotumia ni majengo ya shule, ofisi za serikali na tumeweza kushirikiana pamoja kuwafikia wananchi na kuimarisha afya zao na kuendelea kuchangia kwenye shughuli za uchumi wanazofanya hivyo kuchangia pato la taifa”,ameongeza Dkt Max.
Kwa Mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Kigoma, Dkt. Isaya Mapunda amesema hali ya Maambukizi ya VVU kwa mkoa wa Kigoma kwa sasa ni asilimia 1.7 hali inayotokana na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya THPS na Serikali katika kutoa huduma za afya ikiwemo kuhamasisha jamii jinsi ya kujikinga na VVU, Upimaji, huduma za kinga, matunzo na tiba.
Meneja Mradi wa THPS Afya Hatua Mkoa wa Kigoma, Dkt. Julius Zelothe anasema THPS inafanya kazi na Timu za Usimamizi wa Afya Mkoa na Halmashauri chini ya Mradi wa Afya hatua katika jitihada za kuboresha utoaji wa huduma za kinga, matunzo na tiba kwa wapokea huduma mkoani Kigoma.Meneja Mradi wa THPS Afya Hatua Mkoa wa Kigoma, Dkt. Julius Zelothe
“Tunatekeleza mikakati ya kuhakikisha wapokea huduma wanabaki katika huduma za ART katika vituo 69 vya afya. Ili kufikia wapokea huduma katika maeneo ya pembezoni, mradi huu unawezesha huduma za kupatiwa dawa za ART katika ngazi ya jamii ambapo kuanzia Juni 2023 hadi Juni 2024 mradi wa Afya Hatua umeweza kufanya Kliniki 961 za kutoa ART katika jamii kupitia vijiji 89 mkoani Kigoma”,anaeleza Dkt. Zelothe.
Ameongeza kuwa THPS inalenga katika kushughulikia changamoto mbalimbali za afya ya umma ikiwa ni pamoja na VVU na UKIMWI, Kifua kikuu, ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, huduma za afya ya uzazi, uzazi, watoto wachanga, watoto na vijana, maabara na mifumo ya taarifa za usimamizi wa afya, UVIKO 19 na tathmini za afya ya umma.
MRADI WA CDC/PEPFAR AFYA HATUA
Mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua (Oktoba 2021- Septemba 2026) unatekelezwa na Shirika la THPS katika mikoa minne (Kigoma, Pwani, Tanga na Shinyanga) kwa lengo la kutoa huduma za hali ya juu za kinga, matunzo na tiba ikijumuisha Tohara Kinga kwa wanaume (Kigoma na Shinyanga) na Mpango wa DREAMS ambao unalenga wasichana rika balehe na kina mama wadogo kwa kuwapa afua za msingi ili kupunguza uwezekano wa kuambukizwa VVU.