Na. James Mwanamyoto, OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde amesema, mwalimu ni mtumishi mwenye hadhi kama walivyo watumishi wenginge hivyo ni lazima ajibiwe kwa staha na viongozi wote wakiwemo wakurugenzi wa halmashauri, maafisa elimu wa ngazi zote pamoja na watumishi wengine wa Serikali.
Dkt. Msonde ametoa wito huo kwa nyakati tofauti kwa viongozi na watumishi wa umma nchini, wakati wa vikao kazi vyake na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika halmashauri za wilaya ya Kasulu, Kasulu Mji na Buhigwe.
“Mwalimu akija na changamoto zake, ni wajibu wetu sisi tunayemuhudumia kumjibu kwa staha kama tunavyowajibu watumishi wengine tunaowathamini,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Dkt. Msonde amesema, ukiwa wewe ndio afisa elimu au afisa taaluma kuna ubaya gani ukampokea na kumuhudumia vizuri mwalimu kwani hautopungukiwa na chochote na cheo chako utabaki nacho.
Dkt. Msonde amefafanua kuwa, kupitia azimio la Tabora iliafikiwa kuwa, mwalimu ni lazima aishi kwa amani na wala asinyanyaswe au kunyanyasika ili aweze kutekeleza kikamilifu jukumu la kufundisha na kulea watoto ambalo alipewa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere ambaye alithamini na kutambua mchango wa walimu katika maendeleo ya taifa.
“Tuliamini kwamba, viongozi wa elimu katika ngazi ya mkoa, halmashauri, kata na shule wakijenga utamaduni wa kupendana na kuheshimiana, ni wazi kuwa na wengine wataunga mkono kwa kuuishi utamaduni huo,” Dkt. Msonde amefafanua.
Dkt. Msonde amefanya vikao kazi na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika Halmashauri za Wilaya ya Kasulu, Kasulu Mji na Buhigwe, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake mkoani Kigoma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa maafisa hao.