Na Mapuli Kitina Misalaba
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro
amezuia kuendelea kwa huduma za ibada katika kanisa la "Church of God"
lililopo Kijiji cha Mendo kata ya Ilola Halmashauri ya Shinyanga kwa tuhuma za
Mchungaji wa kanisa hilo kuwazuia Waumini wake kwenda kujifungua katika kituo
cha afya.
Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni siku kadhaa tangu
kutokea kwa tukio la Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Neema Juma
kuzalishwa Kanisani na wahudumu wa Kanisa hilo hali iliyosababisha mtoto
kupoteza maisha.
DC Mtatiro pamoja na mambo mengine amemzuia
mchungaji Endrew Charles Mussa wa kanisa hilo la Church of God kufika katika
kijiji cha Mendo mpaka pale uchunguzi utakapokamilika na kupewa taarifa.
“Wakiti
tunaendelea na hili jambo, hii Nyumba ya ibada ninaifunga kuanzia leo siwezi
nikawa na Nyumba ya ibada kwenye Wilaya yangu inaendesha kazi za kuwazalisha
akina Mama, inawakataza waziende kliniki inawalazimisha kuwazalisha ndani ya
hiyo Nyumba kwahiyo tunaifunga rasmi halafu tutaendelea na taratibu zingine baada
ya kuwa tumeifunga na hakutakuwa na mamlaka nyingine yoyote itakayopaswa kuja
kuifungua aidha ni mamlaka yangu au mamlaka ya juu yangu kwahiyo asije
akajitokeza mtu mwingine yoyote akaingilia jambo hili tutamchukulia hatua kali
na kwa sababu hiyo hakuna tena mtu anaruhusiwa kuingia tena humo ndani ya
NYumba ya Kanisa hili ili tufanye uchunguzi wa masuala mbalimbali ambayo
yamebakia”.
“Lakini
pia Mchungaji Endrew wakati uchunguzi huu unaendelea na mpaka utakapopewa
taarifa usikanyage kwenye kijiji cha Mendo kuanzia leo kwahiyo utakapotoka hapa
usikanyage tena kwenye hiki kijiji fanya shughuli zako sehemu zingine hapa
usikanyage ili tuendelee na uchunguzi”.
“Jambo
la tatu hii Nyumba ya ibada nimeambiwa iliwahi kuanguka upande mmoja ikanyanyuliwa
kwahiyo katibu tawala we unda timu yako ipitie maana hii Nyumba ya ibada ni
Nyumba ya umma inautaratibu wa ujenzi wake kwahiyo katibu tawala unda timu iwe
na mainginia wa Mkoa, mainjinia wa Wilaya, weka timu ya TAKUKURU na vyombo
vingine na wataalamu wa Halmashauri kwahiyo unda timu kama ya watu saba waje
wafanye utaratibu wote ili tujiridhisha, tujue tofali zilizoweka hapa zimepimwa
kwa mujibu wa sheria kwahiyo kama havikufuata utaratibu jengo itabidi libaki
kama bagare”amesema DC Mtatiro
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro pia
amemuagiza afisa utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kumuondoa
kwenye kijiji cha Mendo mtendaji wa kijiji hicho Bi. Christina Mgeni ambapo DC
Mtatiro amesisitiza mtendaji huyo apangiwe majukumu yake kwenye kijiji kingine
na siyo tarafa hiyo.
Awali DC Mtatiro kabla ya kuchukua maamuzi hayo
ametoa nafasi ya kumsikiliza kila mtu katika mkutano huo wa hadhara ambapo
wakazi wa kijiji cha Mendo wameeleza mambo mbalimbali yanayosadikika kufanyika
katika kanisa hilo la Church of God.
Wakazi wa kijiji hicho wamesema kilifanyika kikao
cha kijiji ambapo kwa pamoja waliazimia kuwa hawataka kuona huduma zikiendelea
katika kanisa hilo ambapo waliiomba serikali kulifunga kanisa hilo pamoja na
mchungaji ili kuepusha athari zaidi kwa wananchi.
Wananchi hao wameeleza kuwa mchungaji Mussa aliwahi
kuwazuia waumini wa kanisa hilo kuwa wasifanye shughuli za kilimo Mwezi wa kumi
na moja na kumi na mbili 2024 ambaye aliwaambiwa kuwa maji hayo siyo ya baraka
na kwamba waanze kulima Mwezi wa kwanza
2024 ambapo imeelezwa kuwa baada ya waumini wao kuanza kulima Mwezi wa kwanza
hawajafanikiwa kuvuna chochote.
Wananchi hao pia wamesema watoto wa wazazi wanaosali
katika kanisa hilo wameshazuiliwa kuhudhuria kwenye chanjo zote za serikali lakini pia imeelezwa kuwa waumini wa kanisa
hilo wamezuiliwa kuwaita majina ya ukoo watoto wao.
Pia wananchi hao wamesema akina Mama wanaosali
katika kanisa hilo wamezuiliwa kuhudhurika kliniki zao pamoja na kliniki za
watoto chini ya umuri wa Miaka mitano.
Wakazi wa kijiji hicho wameendelea kusema kuwa toka
awali walilikataa jengo la kanisa hilo ambapo wamesema jengo hilo limejengwa
kwa kiwango cha chini na kwamba limewahi kudondoka upande mmoja, likaunganishwa
ili ibada ziendelee kwahiyo wamehofia usalama wa waumini wa kanisa hilo.
Wananchi wamesema kanisa hilo limesababisha vifo vya
watu takribani wane kwa nyakati tofauti ambapo wamezitaka mamlaka husika
kuchukua hatua za kisheria kwa mchungaji wa kanisa hilo ili iwe fundisho na kwa
watu wengine.
Hata hivyo Mchungaji Endrew Charles Mussa wa kanisa
hilo la Church of God baada ya kuulizwa ameyakana madai yote ya wananchi kuwa
siyo kweli.
Aidha pamoja na mambo mengine wananchi wa kijiji hicho wameeleza kuwa kanisa hilo la Church of God limekuwa likiendesha ibada zake kuanzia saa nane mchana hadi saa nne usiku na ibada nyingine ni kuanzia saa kumi usiku hadi saa mbili asubuhi na kwamba jambo hilo limekuwa ni kero kwa wakazi wa kijiji cha Mendo kata ya Ilola Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akizungumza.DC MTATIRO ALIFUNGA KANISA LA MCHUNGAJI ANAYEDAIWA KUZALISHA WANAWAKE WAJAWAZITO KATA YA ILOLA