SERIKALI KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUONGEZA MIUNDOMBINU ILI KUPOKEA MELI KUBWA ZA GESI YA LPG







Na Gideon Gregory, Dodoma.

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea na uwekezaji wa ujenzi wa mabomba ya kusafirisha na kusambaza gesi majumbani ambapo kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, ina mpango wa kuongeza miundombinu ili kupokea meli kubwa za gesi ya LPG na hivyo kushusha gharama za bidhaa hiyo.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Juni 3,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Neema Lugangira aliyetaka kujua kama Serikali haioni haja ya kupunguza gharama ya gesi ili lengo la kufikia 80% ya Watanzania kutumia Nishati safi ya kupikia ifikapo 2033/34.

“Serikali inaendelea kuhamasisha Sekta Binafsi zinazojihusisha na usambazaji na uuzaji wa gesi ya LPG na gesi asilia pamoja na kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya kujaza gesi vinavyohamishika na visivyohamishika kwa kila Wilaya”, amesema.

Pia ameongeza kuwa Serikali inafanya jitihada kuhakikisha bei ya Nishati safi ya kupikia inapungua ambapo kwa upande wa mitungi ya Gesi inayopatikana kutoka kwenye viwanda vya kusafisha mafuta (LPG – Liquified Petroleum Gas), ruzuku imetolewa kwa mitungi 83,500 yenye thamani ya shilingi Bilioni 3.5.

“Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali itatoa ruzuku kwa mitungi 452,445 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 10”,amesema.
Previous Post Next Post