Azindua Sera ya Taifa ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu zikae pamoja na Wizara ya Fedha na kuandaa mpango wa kitaifa wa kuwawezesha kujikimu vijana wanaoachana na matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Amesema kutekelezwa kwa agizo hilo kutawawezesha vijana hao kupata mitaji ambayo itawawezesha kushiriki kwenye shughuli za ujasiriamali ambazo zitawasaidia kukuza kipato chao.
Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Juni 30, 2024) wakati akizungumza na wananchi na wadau mbalimbali walioshiriki kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Nyamagana, jijini Mwanza.
“Wako wengine wanaohitaji kilimo, Wizara ya Kilimo itoe utaratibu; wapo wanaohitaji ufundi, Wizara ya Elimu itoe utaratibu, lengo ni kuhakikisha vijana hawa wakitoka huko wanakuwa na shughuli ya kufanya ili kujikimu.”
“Kamishna Jenerali pamoja na timu yako ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya endeleeni kufanya operesheni dhidi ya dawa za kulevya kwenye mabasi, ndege, bandarini, vituo vya reli, masoko, maeneo yenye watu wengi, kote nchini ili kuhakikisha kuwa tunaendelea kubaki salama.”
“Niwahimize wananchi wote wakiwemo wazazi, walezi, viongozi wa dini na taasisi za afya, tuendelee kupiga vita dawa za kulevya kwa vitendo na kuhakikisha jamii yetu haijihusishi na biashara, haifanyi uzalishaji wala matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo kutokomeza kilimo cha bangi na mirungi,” amesisitiza.
“Sote tunao wajibu wa kuwafundisha watoto wetu namna bora ya kuishi kwa kufuata maadili na kujiepusha na tabia na makundi rika yanayoweza kuwashawishi kuingia kwenye janga la matumizi na biashara ya dawa za kulevya,” amesema.
Pia ametoa pongezi kwa viongozi wa taasisi hiyo kwa jitihada zilizofikiwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ambapo hadi sasa Serikali imefanikiwa kujenga zaidi ya vituo 16 vinavyohudumia waraibu 16,460 kutoka vituo vitatu vilivyokuwepo mwaka 2017.
“Leo hii ni siku muhimu sana katika historia ya Taifa letu kwani tutashuhudia uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Mwaka 2024. Mheshimiwa Waziri amesema pia sera hii mpya inaweka msisitizo kwenye jukumu la kila mmoja wetu kuanzia ngazi ya kaya hadi taasisi za Serikali na asasi za kiraia. Hivyo, napenda kuwahimiza sote tujitolee kikamilifu kutekeleza Sera hii ya Taifa. Tuwe walinzi wa vijana wetu na tukishirikiana, tunaweza kufanikisha lengo la kuwa na jamii salama na yenye afya njema.”
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia imefanya uwekezaji mkubwa ikiwemo ununuzi wa mashine kubwa na ya kisasa yenye kufanya uchunguzi wa haraka wa viashiria vyote vinavyotakiwa kupatiwa sampuli na kuthibitisha uwepo wa matumizi ya dawa za kulevya.
Amesema mashine hiyo iliyopo kwenye maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imepata ithibati ya Umoja wa Mataifa na ina uwezo wa kuchukua zaidi ya sampuli 250 kwa saa 24.