Ticker

6/recent/ticker-posts

UTEKELEZAJI WA MRADI WA USAID KIZAZI HODARI KANDA YA KASKAZINI MASHARIKI WALETA MATOKEO CHANYA

 Na  Moshi Ndugulile

Serikali imepongeza  utekelezaji wa  Mradi wa  USAID kizazi hodari kanda ya kaskazini Mashariki  unaotekelezwa na kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania K.K.K.T Makao makuu, kuendelea kufanya kwa weledi,tija na ufanisi  katika juhudi za kukabiliana na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi

Akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali Mjini Shinyanga kando ya Mkutano wa wadau wanaotekeleza mradi huo Mkuu wa idara ya afya ,lishe,na ustawi wa jamii,ofisi ya Rais TAMISEMI,Bwana Rashid Kitambulilo,ambaye pia ni Mchumi  amesema  mradi huo kwa kushirikiana na serikali umesaidia kuyabaini  makundi au jamii  ya pembezoni hivyo kuwezesha  kuingizwa kwenye  vipaumbele vya mipango ya afya katika halmashauri husika (complesive hearth plan na concern social worker planning)

Amesema hali hiyo imewawezesha walengwa hao ambao ni watoto wanaoishi na virusi vya ukimwi wenye umri wa Miaka 0-17 kupata huduma na matunzo na tiba.

 “Tunashirikiana na Kanisa la K.K.K.T kuhakikisha kwamba shughuli ambazo zimepangwa kufanyika zinafanikiwa na ushiriki wetu mkubwa upo katika eneo la usimamizi ambapo tunahakikisha kwambwa wale walengwa wanapata zile huduma zilizokusudiwa lakini eneo lingine tunashirikiana katika kuzipitia taarifa za utekelezaji wa mradi huu, tukiangalia moja ya mafanikio ni kwamba hizi jamii ambazo zilikuwa zimesahaulika kwa sasa hivi tumeweza kuzibaini kupitia mradi wa USAID  Kizazi Hodari unaofadhiliwa na shirika la maendeleo ya kimataifa la marekani USAID kupitia mfuko wa Rais PEPFA, na tunashukuru walengwa wanaendelea kunufaika”.amesema Kitambulio

Mratibu wa kudhibiti Ukimwi TACAIDS Mkoa wa Geita  Dkt Yohane Fulgence Kyaga amesema  Mradi huo wa USAID kizazi hodari  kanda ya kaskazini Mashariki umeendelea kusaidia kufikia malengo ya serikali ambayo ni ifikapo Mwaka wa 2030 tunatarajia kutokuwa na maambukizi mapya yatokanayo na virusi vya UKIMWI

“Mradi huu hasa unasaidia kuwafikia watoto ambao kimsingi ni changamoto kubwa kwa hapa Tazania ambapo takwimu zinaonyesha kuwa Mwaka 2022 Watoto Milioni 13,laki Saba walipoteza mzazi moja au wote wawili kutokana na maambukizi ya virusi vya ukimwi,lakini pia watoto 1030, walibainika kuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi wenye umri wa Miaka 0-14 ambapo ni asilimia 57% tu wapo kwenye dawa za kufubaza virusi vya ukimwi,wakati malengo ya Dunia na Tanzania ni kuhakikisha zaidi ya Asilimia 95% wanapaswa kuwa kwenye huduma ya dawa za kufubaza ukimwi, lakini pia watoto 84 walipoteza maisha kutokana na janga la virusi vya ukimwi.

Mradi huu kwa ujuma unatusaidia sisi serikali kufikia malengo ya kufikia zile 95 tatu (95% ya watoto wanajua maambukizi yao,95% wanaanishiwa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi,na 95% nyingine watoto waweze kufubaza virusi vya ukimwi.

Kwa hiyo mradi huu unaisaidia serikali kuwatambua watoto wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi,mradi huu umeweza kuwakatia bima za afya watoto na familia zao,kuwapatia vifaa mbalimbali vya elimu ambavyo vinasaidia kuondoa chngamoto za mtoto hivyo kumwezesha kuwa mfuasi mzuri wa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi lakini pia kuhudhuria masomo kawaida.

Leo tumekutana na kujadili kuhusu takwimu mbalimbali za mradi,tumeweza kushirikishana  uzoefu na mbinu mbadala ambazo zitasaidia katika utekelezaji wa huu mradi,lakini pia tupo kwenye majadiliano kuangalia namna bora ya kuwa na  mikakati endelevu ya kuhakikisha miradi inaendelea baada ya mfadhili kuondoka” ameeleza Dkt Kyaga

 Akizungumzia kuhusu  Mradi huo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara  Dkt. Zabron Masatu ambaye ameshiriki katika Mkutano huo  unaojumuisha wadau wa Mikoa inayotekeleza  mradi huo,amesema wameendelea kushirikiana na USAID kizazi hodari  kanda ya kaskazini Mashariki kuhakikisha wanakuwa na mipango ya pamoja katika utoaji wa huduma za tiba na matunzo kwa watoto hao wanaoishi na virusi vya ukimwi,ambapo serikali imekuwa ikiainisha vipaumbele huku watekelezaji wa mradi wakitoa fedha 

Tumekuwa tukifanya ziara za usimamizi za pamoja kutembelea familia zilizopo kwenye mazingira magumu,lakini tumekuwa tukitoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kusaidia watoto waliopo kwenye mazingira magumu,lakini pia watoto waliopo kwenye mazingira magumu wameweza kutambuliwa ambapo baadhi ya familia zimepatiwa ufadhili wa kadi za bima ya afya yaani ICHF,abazozimekuwa zikiwasaidia kupata matibabu,kuanzia watoto hadi familia nzima kwa ujumla

Lakini vilevile katika kufanya mipango shirikishi sisi serikali kwa sababu tunatambua vipaumbele vinavyohitajika kwa wananchi wetu tumehakikisha kwamba watoto ambao waliokuwa  hawajatambuliwa au walikuwa hawapati matibabu toshelevu kwa sasa wamerudishwa kwenye vituo vya kutolea huduma za dawa kwa ajili ya matunzo kwenye eneo la VVU na UKIMWI

Hii imesaidia kuboresha afya za watoto na familia zao,hali inayowawezesha kuendelea na shughuli za kijamii ikiwemo kuhudhuria masomo ambayo ni haki msingi kwao,wamepatiwa tiba na matunzo vizuri hali iliyosaidia CD4 zao kuongezeka, na kuziwezesha  familia zao kuendelea na shughuli za uzalishaji ikilinganishwa na awali ambapo walikuwa wakitumia muda wao kushughulikia afya za watoto wao, kupitia   mradi huu pia vimeundwa vikundi vya kujikwamua kiuchumi,ambavyo vimesaidia kuongeza kipato cha familia.

Hayo ni mafanikio makubwa kwa serikali kupitia mradi huo,kwani kwa kuwatumia  maafisa wetu kwenye halmashauri mbalimbali tumeendelea kushirikiana na mradi huu kuhakikisha tunawapata walengwa,ameeleza”  Dkt Masatu

Naye mratibu wa Mikoa na Halmashauri kutoka tume ya kuthibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS)  Bi Amina Masoud amepongeza kwa mradi huo kuendelea kuwatambua na kuwawezesha kupata huduma zinazistahili waathirika wa virusi vya UKIMWI ambapo ameshauri mradi huo wa ‘USAID Kizazi Hodari’ kuwa endelevu ili kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi.

Mratibu huyo amesema serikali kupitia tume ya kudhibiti ukimwi Tanzania TACAIDS inatambua na kuthamini mchango wa wadau wa maendeleo katika juhudi za mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi.

Mkurugenzi mshiriki matokeo ya Asasi zinazotekeleza mradi wa  USAID kizazi hodari kanda ya kaskazini Mashariki  Bwana Aminiel Allen Mongi,ametaja mafanikio  yaliyofikiwa katika utoaji wa huduma kipindi cha nusu ya Mwaka kwamba mradi  umefanikiwa kufikia malengo  katika utoaji wa huduma  za Afya ambapo walengwa 157,974 wamefikiwa  ambayo ni asilimia 105%  wakati  idadi  iliyokuwa imetarajiwa katika nusu ya Mwaka  ni  kuwafikia walengwa 157,110

ikiwa ni pamoja na kuwafikia walengwa 62,162 kwenye shughuli za  kiuchumi zaidi ya lengo lililokuwa limekusudiwa la kuwafikia walengwa 59,162

Bwana Mongi ameeleza kuwa  mafanikio hayo ni matokeo mazuri ya utekelezaji wa mradi huo katika kipindi cha nusu Mwaka  2023/2024 Machi ambapo umefanyika kwa kiwango kizuri zaidi

“matokeo ya ushirikiano mzuri baina ya serikali na watekelezaji hao kwenye ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya Wizara zinazoshirikiana moja kwa moja na mradi  huo,  ikiwemo ofisi ya Rais TAMISEMI,wizara ya maendeleo ya jamii,jinsia,wanawake na makundi maalumu,TACAIDS,Wizara ya Elimu,lakini  kwenye ngazi ya Mikoa na Wilaya tumekuwa na ushirikiano mzuri zaidi na wenzetu wa kamati za afya lakini pia kwenye ngazi za kata tunao wasimamizi wa mashauri ya watoto kama FHI  na wadau wengine” ameeleza Mkurugenzi huyo

Ameyataja malengo ya mradi huo kuwa ni kuboresha Afya,ustawi na ulinzi wa watoto walio katika mazingira hatarishi na vijana kuanzia umri wa Miaka 0 hadi 17 ili kufikia malengo ya kidunia ya kupambana na virusi vya ukimwi

“kwa maana ya 95, 95, 95 (wenye maambukizi waweze kujua hali zao,waliofahamu kuwa wana maambukizi waweze kuunganishwa na vituo vya tiba na matunzo kwa ajili ya kuanzishiwa dawa,na walioanzishiwa dawa waweze kuhudhuria kwenye vituo vya tiba na matunzo ili kufubaza maambukizi)”

Ameyataja makundi yanayofikiwa na katika  mradi huo kuwa ni pamoja watoto wanaoishi na maambuki ya virusi vya ukimwi,kaya zinazosimamiwa na watoto,lakini kuna  watoto wa wanawake wanaoishi katika mazingira hatarishi,watoto waliookolewa kwenye  matukio ya unyanyasaji  na ukatili wa kijinsia

“Tunatoa huduma mbalimbali baada ya kuwatambua  na kuwaunganisha na vituo vya kutoa huduma wanaweza tunaongeza afua mbalimbali ambazo zinazuia na maeneo makuu tunayoyalenga  katika utoaji wa huduma  ni pamoja na kutoa bima za afya kwa walengwa ili waweze kupata matibabu wanapopata changamoto za kiafya,haki ya elimu na afya ya uzazi, huduma ya Elimu ambapo tunahakikisha wamesaidiwa ili wahudhurie masomo,ambapo tunawasaidia vifaa vya elimu ili wahudhurie masomo kwa uhakika,elimu ya biashara na fedha kuweka na kukopa,kuwapa vifaa anzilishi vya biashara  ili waweze kuanzisha biashara ndogondogo, lakini pia kuna Nyanja ya ulinzi na usalama kuhakikisha tunawalinda dhidi ya matukio ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia”amesema Mongi

Wadau wanaotekeleza Mradi wa mradi wa USAID kizazi hodari kanda ya kaskazini Mashariki  kutoka Mikoa minne ya Singida,Mwanza,Geita na Mara wamekutana Mjini Shinyanga kutathimini mafanikio,changamoto na matarajio katika nusu ya Mwaka wa fedha 2023/2024

Kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania K.K.K.T Makao Makuu linatekeleza mradi wa USAID kizazi hodari kanda ya kaskazini Mashariki  katika Mikoa tisa ya Tanzania Bara ambayo ni Mwanza,Mara,Geita,Singida,Tanga,Arusha,Kilimanjaro,Manyara na Dodoma,kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya kimataifa la Marekani USAID.

MWISHO



Post a Comment

0 Comments