Ticker

6/recent/ticker-posts

SHEIKH WA MKOA WA MWANZA AMEWATAKA WATANZANIA KUJITOKEZA KUGOMBEA


Na Neema Kandoro,MWANZA
    
SHEHE mkuu mkoani Mwanza Alhaj Shabaan Kabeke amewataka watanzania kujitokeza kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi ili kuweza kupata viongozi watakaoweza kuchochea maendeleo kwenye taifa na kuendeleza misingi ya amani nchini.

Wito ametoa jana Jijini Mwanza, alipokuwa akizungumza kwenye sikukuu ya Eid al adha ambapo sherehe za kuchinja na waislamu wote kushiriki kwa pamoja kula na kugawa nyama kwa familia mbalimbali zisizo na uwezo zilifanywa.

Alisema amani ni tunda la furaha kwa mwanadamu yoyote hapa duniani hivyo aliwaomba watanzania kulinda kwa gharama yoyote ile na kwa vile nchi inaelekea kwenye zoezi la kupiga kura ushiriki wa wananchi katika mchakato huo ni njia sahihi ya kudumisha amani.

Aidha Shehe Kabeke aliwaomba wananchi wote kuepuka siasa za matusi kwani ni kinyume cha utamaduni wa mtanzania na kwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani na kuleta vurugu zisizo na sababu yoyote.

Shehe Kabeke vilevile alisisitiza juu ya umuhimu kujisajiri kuchangia mfuko wao ambao utasaidia katika maendeleo ya kijamii kwenye eneo hilo.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Nyamagana Peter Bega alisema hivi kumeibuka baadhi ya watu wakitumia mtandao wa X zamani twitter kutukana na kutaka kusambaza picha zisizo na maadili hivyo kushauri kufungwa.

Alisema endapo kutaendelea  kuwepo kwa habari zenye kuleta taharuki hapa nchini zitafifisha amani ya nchi ambayo imedumu kwa muda mrefu na hivyo kusababisha taifa kushindwa kudumisha mushikamano wake uliodumu muda mrefu hapa nchini.

"Hivi karibuni Mkurugenzi wa mtandao wa X zamani twitter  amesikika akisema kuwa ipo haja ya kuwekwa kwa maudhui ya habari zote na zile ambazo zinaendeleza mmomonyoko wa maadili ambazo ni kinyume na utamaduni wetu hivyo hakuna haja ya kuendelea kutazama mtandao huo ni bora tufunge" alisema Bega.

Bega aliipongeza kazi kubwa inayofanywa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) ya kuunganisha waumini wa dini hiyo na kuwa misingi mizuri ya kuimarisha umoja na mshikamano hapa nchini.

Alisema taasisi za dini zimefanya kazi kubwa muda wote nyakati ambapo zimetokea changamoto za magonjwa hapa nchini kwa njia za maombi na kuwezesha taifa kuondokana nazo kwa haraka.








Post a Comment

0 Comments