MAADHIMISHO YA SIKU YA WAJANE DUNIANI JUNI 23 , 2024.


HISTORIA; Siku ya Wajane Duniani huadhimishwa tarehe 23 Juni kila mwaka ambapo, iliasisiwa na Bw. Lord Loomba aliyeanzisha Taasisi ya Loomba mwaka 2005 baada ya baba yake kufariki tarehe 23 Juni mwaka 1954. 

UMUHIMU WA SIKU HII:  Wajane ni kundi kubwa ambalo, hukabiliwa na changamoto nyingi baada ya kufiwa na wenza wao ikiwemo, wengine kuachwa katika umaskini, kunyimwa haki zao za mirathi kama ardhi, haki za kuwalea watoto na kudhulumiwa mali nyinginezo walizochuma kwa pamoja na wenza wao.

Aidha, wajane wengine hufukuzwa nyumbani mwao, hutengwa na kunyanyaswa na ndugu wa mume pamoja na jamii na wengine hulazimishwa kuolewa na ndugu wa marehemu pasipo ridhaa yao huku wengine wakikosa huduma ya utetezi pale wanapotafuta haki zao.

Maadhimisho ya siku ya wajane nchini Tanzania hulenga pia, kukuza hamasa, mshikamano na uelewa ndani ya jamii ili kuacha ukiukwaji wa haki za binadamu kwa wajane. 

Aidha, maadhimisho haya hutoa fursa ya pamoja kwenye kutambua changamoto za wajane na namna ya kukabiliana nazo. Katika maadhimisho haya, wajane pia hutengeneza kwa upya mtandao unaowapa nafasi ya kupata taarifa mbalimbali zinazohusu fursa za kiuchumi, kijamii na uongozi kwa maendeleo na ustawi. Halikadhalika, siku hii ni muhimu katika kuongeza uhamasishaji wa kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu kwa wajane.

KAULIMBIU 2024. “Imarisha Mifumo ya upatikanaji wa Nishati: Kukuza Uchumi wa Wajane na Familia”.

Previous Post Next Post