Na Mwandishi wetu, Zanzibar
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kupitia
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kwahani-Zanzibar Bi.Safia Iddi Muhammad
imemtangaza Bw.Khamis Yussuf Mussa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa
mshindi wa Kiti cha Ubunge katika Jimbo la Kwahani.
Mussa almaarufu Pele ameibuka mshindi wa kiti hicho
baada ya kupata Kura 7,092 Kati ya Kura halali 7,383 zilizopigwa na kuwabwaga
wagombea wenzake 13 waliokuwa wakichuana katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo uliofanyika tarehe 8 Juni, 2024.
Jimbo la Kwahani lilikuwa na wapiga kura 11,936 na
waliojitokeza kupiga kura ni 7,522 ambapo kura 139 zilikataliwa hivyo kufanya
kura halali zilizopigwa kuwa ni 7,383.
Vyama 14 vilisimamisha wagombea katika Uchaguzi huo
mdogo wa kiti cha Ubunge jimbo la Kwahani lililopo Wilaya ya Mjini Mkoa wa
Mjini Magharibi.
Wagombea wengine na kura walizopata katika mabano ni
pamoja na Bi. Jarade Ased Khamis wa AAFP
(06), Bi. Madina Mwalim Hamad wa ADA TADEA (49), Bi. Shara Amran Khamis wa ADC (83), Bi. Zainab Maulid Abdallah wa CCK (21), Bw. Abdi Khamis Ramadhan wa
CUF(79), Bw. Bashir Yatabu Said wa Demokrasia Makaini (14) na Bi. Nuru
Abdulla Shamte wa DP(07) .
Wengine ni Bw. Kombo Ali Juma wa NRA (05), Bi. Mwanakombo Hamad Hassan wa NLD (08),
Bw. Amour Haji Ali wa SAU(07),
Bi. Naima Salum Hamad wa UDP(01), Bi.
Mashavu Alawi Haji wa UMD(05) na Bi.
Tatu Omary Mungi wa UPDP(06).
Uchaguzi katika Jimbo la Kwahani umefanyika kufuatia
kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM),
Ahmed Yahya Abdulwakil (65) kufariki dunia mwezi Aprili mwaka huu.