Ticker

6/recent/ticker-posts

UCHAGUZI NACONGO MUDA WA KUCHUKUA FOMU WATANGAZWA, SIFA KWA WAGOMBEA ZATAJWA






Mwenyekiti kamati ya mpito ya kuratibu uchaguzi wa Baraza la taifa la NGOs Bi.Christina Ruhinda,wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 1,2024 jijini Dodoma kuelekea katika uchaguzi wa mashirika yasiyo ya kiserikali NaCoNGO

……………

KAMATI ya mpito ya kuratibu uchaguzi wa mashirika yasiyo ya kiserikali NaCoNGO wametangaza muda wa kuchukua fomu pamoja na vigezo vya kugombea nafasi za uongozi kwa wanachama wake wanaotaka kugombea ngazi ya mkoa.

Hayo yameelezwa leo Juni 1, 2024 jijini Dodoma na Mwenyekiti kamati ya mpito ya kuratibu uchaguzi wa Baraza la taifa la NGOs Bi.Christina Ruhinda,wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema wagombea waliopita kutoka katika uchaguzi wa wilaya, moja kwa moja wamefuzu kushiriki katika uchaguzi wa ngazi ya mkoa ili kupata mshindi 1 kwa kila mkoa atakaekuwa sehemu ya wajumbe wa NaCoNGO ngazi ya Taifa.

Amesema anayajulisha mashirka yasiyokuwa ya kiserkali na umma wa watanzania kuanza kwa mchakato wa uchaguzi wa baraza ngazi ya mkoa ambao utaenda pamoja na uchaguzi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, kimataifa na wawakilishi wa makundi maalum (Watoto, Vijana na Watu wenye Ulemavu).

“Sifa za mgombea wa nafasi za uongozi anatakiwa awe kiongozi au mwanachama katika NGO iliyosajiliwa chini ya sheria ya NGOs na mwenye uzoefu na uelewa mpana wa sera, sheria, kanuni na miongozo ya NGOS, awe mtanzania isipokuwa kwa mwakilishi wa NGOs ya kimataifa lakini mwenye kibali cha kufanya kazi Tanzania, awe na umri usiopungua miaka 18 na usiozidi miaka 70, asiwe alishawahi kupatikana na makosa ya jinai, awe na elimu ya kidato cha nne au zaidi, awe na uwezo mzuri wa kuzungumza lugha ya kiswahili na kiingereza na awe na akili timamu,”

“Vigezo vya shirika kushiriki katika uchaguzi liwe limesajiliwa kwa mujibu wa sheria ya NGOs, sura ya 56 ya sheria za Tanzania, liwe linatekeleza shughuli zake katika eneo au afua husika, liwe katika orodha ya msajili msaidizi wa halmashauri au Wilaya au mkoa husika, liwe linatekeleza shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia NGOs, ikiwemo ulipaji wa ada na wasilishaji wa taarifa na kila NGO lililokidhi vigezo tajwa hapo juu litakuwa na kura moja.” amesema Ruhinda.

Aidha ameeleza kuwa kamati wamejipanga kuhakikisha inapambana na kudhibiti viashiria vya rushwa kwenye uchaguzi wa baraza ngazi ya mkoa na uwakilishi wa makundi maalum.

Amesema fomu ya maombi ya kugombea nafasi ya viongozi wa baraza itatolewa bure na msimamizi wa uchaguzi huku zoezi la kuchukua na kurudisha fomu za maombi katika ngazi ya mkoa litaanza saa 2 kamili asubuhi na kumalizika saa 9 kamili alasiri.

Pia ameainisha fomu hiyo ya mgombea itaambatanishwa na nakala ya kitambulisho cha taifa, barua ya utambulisho wa shirika analotoka mgombea, picha mbili za mgombea, vivuli vya vyeti vya taaluma na mafunzo mbalimbali, maelezo binafsi ya mgombea (CV), nakala ya cheti cha shirika analotoka mgombea, mgombea atakosa sifa ya kupigiwa kura endapo maombi yake yatabainika kutokujaza fomu za maombi kwa usahihi na ukamilifu, kutokuwa na viambatanisho vinavyotakiwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, kutokuwa na sifa za msingi zilizoainishwa kwa
mujibu wa kanuni za uchaguzi.

“Zoezi la kampeni na kupiga kura wagombea watanadi sera zao kwa wapiga kura katika kila mutano wa uchaguzi, zoezi la upigaji wa kura litafanyika kwa siri, wapiga kura ni wawakilishi wa NGOs ziliyokidhi vigezo, wagombea wataonesha barua ya uthibitisho kutoka NGOs wanazoziwakilisha na nakala ya cheti cha usajili, wagombea katika ngazi ya mkoa ni wawakilishi watatu waliochaguliwa katika ngazi ya wilaya, uchaguzi wa makundi maalum utahusisha mwakilishi wa mashirika ya kimataifa na NGOs yanayotekeleza afua za watu wenye ulemavu, vijana na watoto.”amesema

Pia amesema kura zitahesabiwa baada ya upigaji kura kumalizika katika ngazi husika na kura zitahesabiwa chini ya msimamizi wa uchaguzi na mwangalizi wa uchaguzi pia kila gombea atakuwa na mwakilishi wake atakayehakiki kura za mgombea wake, mgombea ataandika maelezo na kuyawasilisha kwa msimamizi wa uchaguzi ikiwa
hajaridhia matokeo.

Zoezi la kuchukua fomu za kugombea litaanza Juni 3 hadi 4 2024 huku fomu zitarudishwa Juni 5 hadi 6 2024, uchakataji wa fomu utafanyika Juni 7 hadi 8 2024 huku kampeni na zoezi la upigaji kura, kutangaza matokeo na kuapisha washindi litafanyika Juni 11, 2024.

Kamati hiyo ya mpito ya kuratibu uchaguzi wa baraza la taifa la mashirika yasiyo ya kiserkali inatoa wito wa viongozi na wanachama wa NGOs kujitokeza kugombea nafasi ya ongozi wa baraza ngazi ya mkoa na uwakilishi wa makundi maalum na NGOs ya kimataifa kwa maendeleo ya sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini.

Post a Comment

0 Comments