NA AMINA SAIDI,TANGA
Vijana 64 kutoka mikoa mbalimbali wamekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoani Tanga wakijihusisha na biashara isiyo halali ya kimtandao ijulikanayo kwa jina la Q - net.
Akizungumza Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama (KU) ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian mara ya kufika kituoni Polisi Chamgageni, amesema vijana hao wamekuwa wakipigia simu wazazi na kuwataka watoe pesa ili vijana wao waweze kupata ajira kupitia bidhaa wanazoziuza.
Dkt Batilda amesema viongozi wa Mtandoa huo wanatokea mkoa wa Dar es salaam na huku mikoa mingine wakiwatuma vijana kufanya kazi hiyo.
"Tumeona vijana ambao ndiyo nguvu kazi miaka kuanzia 19 hadi 24 na wengine wamefika hadi vyuo vikuu lakini hakuna chochote wanachokifanya"
Dkt Batilda ametoa rai kwa wazazi kuwa makini endapo wanapigiwa simu na watu kwa ajili ya ajira za vijana wao hasa biashara za kimtandao.
"Huu utaratibu wazazi ambao mnapigiwa simu za kazi na nyie mnawaruhusu watoto wanaenda ni utapeli mtupu tuwe makini na mitandao" aliongeza Dkt. Batilda
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Batilda amesema vijana hao wote waliokamatwa watasaidiwa kupata mafunzo ya ufundi katika vyuo vya veta ili waweze kupata elimu ya ujasiriamali itayowasaidia kupata ujuzi kwenye maeneo yao
Dkt Batilda amesisitiza kuwa Tanga ni Mkoa salama na hauna nafasi ya kufanya biashara ambazo hazitambuliki huku akisisitiza vijana hao watarudishwa kwenye maeneo yao kwa uangalizi maalumu.
CHANZO - MATUKIO DAIMA