Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Mhe. Emmanuel Ntobi, akionyesha majibu ya barua za zuio la kutumia uwanja wa Zimamoto uliopo Nguzonane mjini Shinyanga.
Na Mapuli Kitina Misalaba
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la
Shinyanga Mjini kimelalamikia kunyimwa eneo la kufanyia mkutano wa hadhara
katika uwanja wa Zimamoto Nguzonane Manispaa ya Shinyanga.
Hayo yamebainishwa na viongozi wa chama hicho leo
Juni 8,2024 wakati wakizungumza na waandishi wa habari ambapo wamelilalamikia
jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Shinyanga kwa kuwanyima nafasi ili kufanya
mkutano wao wa hadhara katika uwanja wa
jeshi hilo na kwamba mara nyingi uwanja
huo hutumika kwa ajili ya mikutano mbalimbali.
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Mhe. Emmanuel
Ntobi, pamoja na mambo mengine amewasisitiza wananchi wote kujitokeza kwenye
mkutano huo wa hadhara Jumatano Juni 12,2024 huku akieleza malengo ya mkutano
huo wa hadhara.
“Tumeazimia
wiki ijayo siku ya Jumatano tarehe 12,06,2024 tutafanya mkutano eneo hilo hilo watake
au wasitake tumeona hili ni shambulio la demokrasia na sisi ni wadau namba moja
chama kikubwa cha upinzani kiweze kuzuiliwa kufanya mikutano kwa sababu ambazo
hazina miguu wala kichwa, tumeanziamia na tunawaomba wananchi na watanzania
watuelewe na wajitokeze kwa wingi siku ya Jumatano tarehe 12 tutafanya mkutano
mkubwa wa hadhara kwenye eneo hilo hilo ambalo wanataka kutuzuia tumejiridhisha
sababu walizozitoa hazina mantiki wala hazina kitu chochote cha kisheria”.
“Lengo
na madhumini ya mkutano wetu huu ni kutoa elimu ya uraia tunapoelekeza kwenda
kuandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura lazima tutoe elimu ya uraia
wananchi waweze au wapenzi wa CHADEMA waende wakajiandikishe lakini jambo la
pili ni maandalizi ya serikali za mitaa mtakumbuka mwaka huu tunaenda kuchagua
viongozi katika serikali za mitaa”.amesema Mhe. Ntobi
“Ukiangalia
Barua hizi Mbili za Zimamoto zina Majibu Tofauti, hapa inaonyesha kuna kitu au
wamepokea maelekezo kutoka Juu, hata Tundu Lissu tumeshuhudia amekuwa wakinyiwa
Viwanja vya kufanya Mikutano ya hadhara kwenye baadhi ya Mikioa, ina wezekana
kuna Mikakati inatengezwa chini kwa chini,”.
“Mbona
Mwaka jana tulifanya Mkutano wa hadhara kwenye Viwanja hivyo, kwa nini sasa
hivi tuzuiwe hasa kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikaliza Mitaa, hivyo basi
pamoja na mazuio yao sisi siku hiyo ya Jumatano ambayo ni Juni 12 tutafanya
Mkutano hapo watake wasitake sababu zao hazina Mantiki wala Kisheria,”.
amesema Ntobi
Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga Mjini,
Hamis Ngunila ameeleza kuwa Juni Mosi
mwaka huu waliandika barua kuliomba Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa
Shinyanga kuutumia uwanja wa jeshi hilo Juni 7, lakini katika barua yao
wakajibiwa siku hiyo Uwanja huo utakuwa na matumizi mengine.
“Tarehe
1,06,2024 tuliandika barua kwenda katika jeshi la zimamoto kwa ajili ya kuomba
kutumia uwanja wa Zimamoto ambao kiuhalisia uwanja huu ni uwanja wa umma kwahiyo
tuliomba uwanja ule ili tuweze kufanya mkutano wa hadhara lakini majibu yaliyotolewa
ni kwamba uwanja ule Tarehe 7 ambayo ilikuwa ni siku ya Ijumaa ni kwamba uwanja
ule utakuwa na matumizi mengine, tukapokea majibu hayo lakini tukafikiri kwamba
kwamba kwa sababu uwanja huo siku ya Ijumaa utakuwa na matumizi tukafikiri
kusogeza mbele mkutano wetu tukaandika barua nyingine kuwaomba jeshi la
zimamoto kwamba badala ya siku ya Ijumaa ambayo ni tarehe 7 tufanye mkutano
wetu wa hadhara wa jimbo basi tukausongeza mbele, tutaufanya wiki ijayo siku ya
Jumatano tarehe 12, 06,2024 lakini cha ajabu majibu yaliyotoka ni kwamba uwanja
ule wa jeshi la Zimamoto hauruhusiwi tena kufanyiwa mikutano ya kisiasa”.amesema
Ngunila
“Sasa
tunaujulisha umma kama kiongozi wa jimbo nikiambatana na viongozi wengine wa
Mkoa kwamba ratiba ambayo tumeomba kuutumia
uwanja ule tarehe 12 wiki ijayo siku ya Jumatano iko pale pale na tumesema hivo
kwa sababu kiwanja kile tumekuwa na rekodi nacho mara kwa mara tunafanyia
mikutano ya hadhara lakini tambueni kuwa hatuna taarifa yoyote baada ya kuweka
zuio la kufanyia mikutano ya hadhara kwenye kile kiwanja hawajawahi
kutufahamisha”.
“Mambo
haya yametupa mkanganyiko sana na tumeanza kuamini kuwa yawezekana ukandamizaji
wa kidemokrasia kwenye taifa hili unaendelea itoshe kusema sauti hii iende kwa
umma na watanzania wajue kwamba sisi kama viongozi ambao wametupa dhamana hatuwezi
kukubali lazima mkutano wetu ufanyike”.amesema Ngunila
Naye Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Mkoa wa Shinyanga Martin Nyambala, amekili kuwazuia CHADEMA kufanya mkutano wao
wa hadhara katika eneo hilo
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Mhe. Emmanuel
Ntobi, akilalamikia changamoto ya kunyimwa uwanja kwa ajili ya mkutano wa
hadhara wa chama hicho katika jimbo la Shinyanga mjini.
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Shinyanga Mhe. Emmanuel Ntobi, akionyesha majibu ya barua za zuio la kutumia uwanja wa Zimamoto uliopo Nguzonane mjini Shinyanga.
Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga Mjini, Hamis Ngunila akielezea hatua mbalimbali ambapo amelilalamikia jeshi la Zimamoto na uokoaji kwa kuwazuia kutumia uwanja huo kwa ajili ya mkutano wao wa hadhara.
Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga Mjini, Hamis Ngunila akielezea hatua mbalimbali ambapo amelilalamikia jeshi la Zimamoto na uokoaji kwa kuwazuia kutumia uwanja huo kwa ajili ya mkutano wao wa hadhara.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga Martin Nyambala akifafanua kuhusu malalamiko ya CHADEMA Mkoa wa Shinyanga.
TAZAMA VIDEO YOTE YA CHADEMA NA MAJIBU.