WAKAZI WA ISELAMAGAZI WASHAURI ELIMU ITOLEWE KUHUSU HAKI NA USALAMA WA MTOTO BAADA YA WAZAZI KUACHANA

 Baadhi ya wananchi wa Kata ya Iselamagazi katika Halmashauri Wilaya ya Shinyanga, wameishauri Serikali pamoja na wadau wengine kuendelea kutoa elimu kuhusu haki na msalahi ya watoto pale wazazi (Baba na Mama) wanapotengana au kuachana ili kuepuka madhara yanayowapata watoto pale yanapotokea mazingira ya namna hiyo.

Wananchi hao wametoa ushauri huo wakati wakichangia hoja katika mjadala ulioandaliwa na Redio Faraja kwa kushirikiana na Mfuko wa Ruzuku kwa wanawake Tanzania (WFT-T) kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika, uliowashirikisha watoto na wazazi juu ya Nani anayepaswa kubaki na mtoto pale wazazi wanapotengana au kuachana kwa kuzingatia maslahi ya watoto.
Wanachi hao wamebainisha kuwa, mapokeo ya kimila kwa kabila la Wasukuma ambalo linajumuisha jamii kubwa ya wakazi wa mkoa wa Shinyanga, wazazi wanapoachana kwa mtoto au watoto ambao Mama yao ametolewa mahari bila kujali umri wao wanapaswa kubaki kwa Baba, lakini pale wazazi wa kike wanapoamua kuwaacha kwa kuzingatia mila hiyo changamoto kubwa inayotokea ni wazazi wa kiume kushindwa kuwalea na kulazimika kuwaachia jukumu hilo Bibi zao ambao ni wazee pamoja na Mama wa kambo ambao wengi wao huwanyanyasa na kuwatesa, hali inayosababisha wakumbane na shida nyingi kiwemo kuathirika kimwili, kiafya na Kisaikolojia na wakati mwingine kupoteza maisha.
Wamesema pamoja na sheria zilizopo kuwapa ulinzi wa watoto pale wazazi wao wanapoachana au kutengana, bado jamii kubwa inaendelea kufuata utaratibu wa kilimila wa Baba kubaki na watoto bila kuzingatia ustawi na usalama wao, jambo ambalo linawaweka katika hatari ya kukosa haki muhimu wanazostahili kupata ikiwemo athari za kimalezi na makuzi, ambapo kwa wale wadogo wanaohitaji uangalizi wa karibu madhara wanayoyapata ni makubwa huku wale wanaoanza kujitambua baadhi yao hushindwa kustahimili na kulazimika kuzikimbia changamoto wanazozipata kwa kutoroka na kwenda kuishi kwenye mazingira hatarishi.
Kwa upande wao watoto walioshiriki mjadala huo wakiwemo wale ambao wazazi wao wameachana, wamependekeza hali hiyo inapotokea ni vema wakaishi na Mama zao ambao wanaweza kuwahudumia, kuwajali zaidi na kutimiza mahitaji yao, badala ya kubaki kwa Baba ambaye ana majukumu mengi yanayomfanya awakabidhi chini ya uangalizi wa watu wengine ambao wengi wao siyo salama kwa ustawi wa maisha yao.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Iselamagazi Bi Joyce Chawala amebainisha kuwa, sheria ya mtoto inaelekeza watoto wote wa umri wa chini ya miaka saba wabaki chini ya malezi ya Mama pale wazazi wanapotengana au kuachana hata kama wametolewa mahari na pale wanapofikisha umri wa miaka saba na kuendelea wanaweza kwenda kulelewa kwa baba ingawa kinachozingatiwa zaidi ni mslahi ya mtoto ikiwemo usalama wake.
Mjadala huo umefanyika kufuatia kifo cha mtoto mmoja wa umri wa chini ya miaka mitano kilichodaiwa kutokana na kukosa huduma mbalimbali ikiwemo chakula na matibabu katika Kijiji cha Mwang’osha Kata ya Nyamalogo, baada ya wazazi wa mtoto huyo kuachana na kubaki chini ya malezi ya Baba ambaye pia alimkabidhi mtoto huyo kulelewa na Bibi yake wa kambo.
Aidha Mtoto mwingine wa chini ya umri wa miaka mitano alinusurika kufa baada ya kuokolewa na majirani kwa kushirikiana na Serikali ya Kijiji katika Kijiji cha Nsalala, baada ya afya yake kudhoofika kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni manyanyaso aliyokuwa akiyapata kutoka kwa Mama yake wa Kambo ikiwemo kupigwa, kukanyagwa, kulazimishwa kulala kwenye mlango wakati wa usiku kama mlinzi, kunyimwa chakula na kutopelekwa Hospitali pale anapougua.
Pia vipo visa kadhaa vilivyoripotiwa kuhusu watoto kufanyiwa ukatili wa kingono na Baba zao wa kuwazaa pale wazazi wanapoachana au kutengana na Mama kuamua kuondoka na kuwaacha chini ya malezi ya Baba.
Previous Post Next Post