WATANZANIA wameshauriwa kufuga kuku wa kisasa wanaotaga mayai na wale wa nyama ili waweze kujiongezea kipato chao kwa kuwa ni wepesi kukua hivyo itamwezesha mfugaji kuuza na kujipatia kipato haraka.
Wito huo umebainishwa leo Jijini Mwanza na Mkurugenzi wa Misenani Agri Services Dk Cuthbert Kivuyo akisema ufugaji huo hauna gharama kubwa hivyo watu wenye kipato cha chini ambao wanazo changamoto za kimaisha wanaweza kuchangamkia fursa hiyo na kuongeza vipato vyao.
Alisema kuku hao wanaweza kuwa tayari kwa kuuzwa baada ya wiki tano tangia kutotolewa kwa vifaranga huku wale watagao nao wanaanza kutaga mayai.
Dk Kivuyo alisema kuwa mara baada ya kutotolewa kwa vifaranga wanatakiwa kuanza kupata chanjo wiki ya kwanza dhidi ya ugonjwa wa new kasto, wiki ya pili kukabiliana na ugonjwa gumburo na wiki ya tatu kukabiliana na ugonjwa wa ndui.
Alisema ufugaji wa kuku unaweza kuwasaidia watanzania wengi kujiongezea kipato chao kwani uhudumiaji wake wa vyakula ni mwepesi kwani gharama zake ni ndogo.