WAZIRI HARUNA AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KUHUSIANA NA WIKI YA MSAADA WA KISHERIA

 

Na Fauzia Mussa 


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika maadhimisho ya tano ya wiki ya msaada wa kisheria ifikapo Juni 28 , mwaka huu .

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na wiki hiyo huko Mazizini Waziri wa Nchi OR Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Mhe.Haroun Ali Sleiman amesema maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa sheikh Idrissa Abdul wakil Kikwajuni Wilaya ya Mjini na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi na watendaji wa Serikali ,Taasisi binafsi ikiwemo Shirika la legal Services Facility (LSF), Shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), UNICEF, UN WOMEN pamoja na watoa na wataka huduma za msaada wa kisheria.

Ameeleza kuwa katika maadhimisho hayo namba maalum ya upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi itazinduliwa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo ndani ya jamii.

Aidha amesema katika kutambua mchango wa wasaidizi wa kisheria tuzo za mwaka za kitaifa za watoaji wa msaada wa kisheria kwa Zanzibar zitatolewa katika maadhimisho hayo.

Mbali na hayo amesema wiki hiyo itajumuisha shughuli mbalimbali hadi kufikia kilele chake ikiwemo kampeni ya vyombo vya habari kuhusu wiki ya msaada wa kisheria,kongamano la vyuo vikuu kuhusu masuala ya msaada wa kisheria, kongamano la malezi ambalo litahusisha ujengaji wa kiimani na utoaji wa Elimu ya ushauri nasihi pamoja na utoaji wa huduma za msaada wa kisheria Unguja na Pemba.

Takribani washiriki 300 wanatarajiwa kuhudhuria katika maadhimisho ya siku hiyo yaliyoratibiwa na Idara ya Katiba na msaada wa kisheria kwa kushirikiana na LSF na UNDP yakiwa na kauli mbiu "TUMIA TEKNOLOJIA KURAHISISHA UPATIKANAJI WA HAKI".


Previous Post Next Post