Waziri Mkuu Kassim Majakiwa amesema Serikali inaendelea kujikita katika kuhakikisha
inaimarisha na kuwashirikisha wavuvi na wafugaji katika mipango ya maendeleo.
Amesema hayo leo Juni 03, 2024 alipoweka jiwe la
msingi la ujenzi wa soko la samaki la kisasa la Chato Beach, Chato mkoani
Geita.
Amesema kuwa Mradi huo unaotoa fursa kwa yeyote
aliyeanza na anayetaka kujikita kwenye sekta ya uvuvi kunufaika na kujiingizia
kipato. “Kitendo cha Serikali kuleta soko hili hapa ni kuhakikisha wanasogeza
fursa kwa wavuvi wa eneo hili, soko hilo
ni lenu, imarisheni uchumi wenu kupitia soko hili”.
Ameongeza soko hilo litakuwa na uwezo wa kukausha
hadi tani 10 za dagaa kwa siku kwa kuwa kutawekwa mtambo wa kukausha samaki.
“Tutaweka mafriji makubwa mawili ya kutunzia samaki, pamoja na chumba maalum
cha kuzalisha barafu”
Ujenzi wa soko hilo ambalo umefikia asilimia 90 utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.75 na utasaidia kupunguza kero zilizopo.